Fahamu Chanzo Cha Magonjwa Ya Moyo
LEO tutaelezea kwa kina chanzo cha magonjwa ya moyo ambayo husumbua watu wengi. Chanzo kikubwa ni watu kutozingatia kanuni za ulaji bora, ni moja ya mambo yanayoongeza uwezekano wa mtu kupata magonjwa ya moyo. Kwa mfano, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi nyingi na lehemu nyingi, huku ulaji wa mbogamboga na matunda ukiwa ni wa kiwango cha chini, huongeza uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya moyo.
Lakini pia hali ya kuwa na uzito uliozidi kiasi au kuwa na unene uliopitiliza pamoja na kutofanya mazoezi ya mwili na viungo mara kwa mara, huchochea uwezekano wa mtu kukumbwa na magonjwa ya moyo. Wakati mwingine magonjwa ya moyo huweza kutokana na historia ya ugonjwa huo katika familia. Umri unapozidi miaka 50 kuna uwezekano pia wa kupatwa na magonjwa haya ya moyo, huku wanaume wakiwa kwenye hatari zaidi ya kupatwa na tatizo hili mapema zaidi ikilinganishwa na wanawake.
Magonjwa ya moyo huanza kumwandama mtu pale mambo fulani yanaposababisha sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa. Mambo hayo ni pamoja na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha aina fulani za mafuta na lehemu katika damu.
Hali hiyo inapompata mtu, mishipa ndani ya moyo huweza kufungamana kwa mafuta, hivyo kuleta Mshtuko wa Moyo kitaalamu Heart Attack) au kupooza kwa maana ya kiharusi, yaani Stroke. Aidha, ongezeko la lehemu huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
Kiujumla, wingi wa lehemu unakadiriwa kusababisha vifo vya watu takriban milioni 2.6 duniani kila mwaka.
Kuwepo kwa sukari nyingi katika damu, husababisha ugonjwa wa Kisukari, ambao unamweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa Moyo au kupooza au kiharusi mara mbili zaidi ya asiye na Kisukari. Aidha, kuwa na sukari nyingi kwenye damu kwa muda mrefu, husababisha kuganda kwa mafuta kwenye mirija ya damu. Kuganda huku kunaweza sababisha kupungua kwa mtiririko wa damu kwenye mishipa.
Shinikizo Kubwa la Damu, maana yake ni kwamba moyo unalazimika kusukuma damu kwa nguvu ili kutosheleza mahitaji ya mwili. Kuulazimisha moyo kufanya kazi kuliko kawaida yake, kunasababisha moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure).
Uvutaji wa sigara au utumiaji wa tumbaku kwa kutafuna au kunusa (ugoro), husababisha pia sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa, hivyo kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo. Kemikali zinazopatikana kwenye tumbaku, huweza kuharibu seli za damu.
Uharibifu huo wa seli, huingilia muundo na utendaji mzuri wa mishipa ya damu. Aidha, kuharibika kwa mishipa ya damu, kunachochea mafuta kuganda kwenye mishipa ya damu (Atheroskerosisi). Unywaji pombe kupita kiasi na utumiaji wa dawa za kulevya ni hatari tena kwa hili. Unywaji pombe mara kwa mara huongeza uzito wa mwili, hali inayoweza kusababisha Shinikizo la Damu kupanda.
Aidha, pombe na dawa za kulevya hudhoofisha misuli ya moyo na mishipa ya damu. Misuli na mishipa ya damu ya moyo ikishadhoofika, huweza kusababisha moyo kutofanya kazi katika ubora wake (Heart Failure). Lakini pia, ikitokea mishipa ya damu ikaharibiwa, mafuta mwilini hujikusanya katika sehemu ya mishipa iliyoharibiwa, hivyo kutengeneza utando wa mafuta (plaque).
Kadri muda unavyoendelea ndivyo mafuta haya yanavyozidi kujijenga katika sehemu hiyo hadi kufanya mishipa hiyo kuwa myembamba, hivyo kupunguza kiasi cha damu kinachobeba hewa ya oksijeni na virutubishi kwenda kwenye misuli ya moyo.
Kitendo hicho kitaalamu, huitwa Atherosklerosisi, ikimaanisha kukakamaa kwa mishipa ya ateri kutokana na mkusanyiko wa mafutamafuta ndani ya ateri.
Hatimaye sehemu hiyo ikipasuka, sehemu ya seli za damu zinazoitwa pleteleti za damu (chembe ndogo mviringo ambazo zinahusika na kuganda kwa damu) ambazo husaidia mwili kuponya kidonda, hujigandisha kwenye mpasuko, hivyo kuanza kujikusanya.
Hali hii huongeza mkusanyiko, hivyo kuendelea kufanya mishipa hiyo kuwa myembamba zaidi, hivyo kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure) na mtu kupata ugonjwa wa Mshtuko wa Moyo (Heart Attack). Mkusanyiko wa mafuta na pleteleti za damu wakati mwingine, huweza kumeguka katika mfumo wa mabonge na kusafiri kwenda kuziba mishipa midogo ya damu kichwani. Hali hii ikitokea, mtu hupata Kiharusi (Stroke/ Cerebrovascular Accident). Itaendelea wiki ijayo.
Dk. Marise anapatikana Marise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta. Simu: 0713 252 394
Post a Comment