Bei mpya ya mafuta ya Petroli itakayoanza kutumika leo Februari 7, 2018 kote nchini
Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za
mafuta zinazoanza kutumika leo Februari 7, 2018 huku bei za petroli,
dizeli na mafuta ya taa zikipanda.
Taarifa
kwa umma iliyotolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa
Mchany imesema bei za rejareja zimeongezeka kwa petroli ikiwa ni Sh59
sawa na asilimia 2.70, dizeli Sh46 (sawa na asilimia 2.30), na mafuta ya
taa kwa Sh24 (sawa na asilimia 1.17).
Amesema
bei za jumla nazo zimeongezeka ambazo kwa petroli ni Sh58.57 sawa na
asilimia 2.85, dizeli kwa Sh46.48 (sawa na asilimia 2.44) na mafuta ya
taa kwa Sh23.75 (sawa na asilimia 1.24).
Mchany amesema ongezeko hilo linatokana na bei kuongezeka katika soko la dunia.
“Bei
za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli yaliyoingizwa
nchini kupitia Bandari ya Tanga nazo zimeongezeka ikilinganishwa na
toleo lililopita la Januari 3. Bei za mafuta ya taa hazijabadilika kwa
sababu hakuna yaliyoingizwa nchini kupitia bandari hiyo Januari,”
amesema Mchany.
Amesema
bei za rejareja katika mikoa ya Kaskazini zimeongezeka, ambazo petroli
ni kwa Sh15 sawa na asilimia 0.70 na dizeli kwa Sh47 sawa na asilimia
2.29. Bei za jumla zimeongezeka petroli ikiwa ni kwa Sh15.36 sawa na
asilimia 0.73 na dizeli Sh47.18 sawa na asilimia2.42.
“Ongezeko
la bei za mafuta ya petroli na dizeli katika Mkoa wa Tanga linatokana
na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na kuongezeka kwa
gharama za usafirishaji,” amesema Mchany.
Kaimu
mkurugenzi mkuu huyo amesema sehemu ya shehena kubwa ya mafuta
yaliyopokewa katika Bandari ya Dar es Salaam ni yenye bei ya soko la
dunia za Novemba, 2017 wakati iliyopokewa katika Bandari ya Tanga ni ya
bei ya soko la dunia ya Desemba 2017.
Amesema
bei za mafuta katika soko la dunia kwa Novemba 2017 ziko juu kwa zaidi
ya asilimia sita ikilinganishwa na bei za Oktoba 2017, wakati bei za
Desemba zina mabadiliko tofauti.
Amesema bei ya petroli imepungua kwa asilimia 0.2 na ya dizeli na mafuta ya taa imeongezeka kwa asilimia 2.7 na asilimia 1.9.
“Kampuni
za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya
ushindani ili mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo kama
ilivyokokotolewa na kanuni iliyopitishwa na Ewura,” amesema Mchany.
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI KIKOMO ZA MAFUTA AINA YA PETROLI KUANZIA JUMA TANO, TAREHE 7 FEBRUARI 2018 => BONYEZA HAPA KUISOMA YOTE
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI KIKOMO ZA MAFUTA AINA YA PETROLI KUANZIA JUMA TANO, TAREHE 7 FEBRUARI 2018 => BONYEZA HAPA KUISOMA YOTE
Post a Comment