ad

ad

SAFARI YANGU YA KWANZA KUZIMU-16 (MWISHO)


NYEMO CHILONGANI

Nilimuona msichana akiwa amesimama barabarani, ilikuwa usiku sana, kama saa nane hivi. Alikuwa msichana mrembo, alivalia kiheshima sana, alivutia mno, nywele zake ndefu zilifika mgongoni, alipendeza mno, kadiri nilivyokuwa nikimwangalia, hata mimi nilimpenda sana.
Uso wake ulijawa na tabasamu kila wakati, hakuwa mswahili, alikuwa msichana mwenye mchanganyiko wa rangi ambaye ningeweza kumuita Chotara. Sikujua msichana huyu alikuwa nani, alikuwa akifanya nini mahali pale, ila kila nilipomwangalia, hakika nikajisemea kwamba hakukuwa na mwanamke mrembo kama alivyokuwa.
Mwanzo nilifikiri alikuwa akijiuza barabarani pale, lakini haikuwa hivyo, sidhani kama kungekuwa na mwanamke aliyekuwa akijiuza huku akiwa amevalia gauni refu, lililofika unyayoni kama alivyovaa msichana yule.
Magari yalipita, kila aliyepita na gari lake, alipokaribia mahali aliposimama msichana yule, alipunguza kasi ya gari lake na kisha kumtupia macho. Msichana yule aliendelea kusimama mpaka nilipomuona jamaa mmoja akienda upande ule aliokuwa msichana yule, kwanza akampita huku akimwangalia, alipofika kama hatua nne mbele, akaona haiwezekani, akaanza kupiga hatua kumfuata.
Kumbuka haya yote nilikuwa nikiyaona kwenye ile televisheni kubwa ya kichawi, baada ya kumuona msichana huyu kule kuzimu huku akiitwa kwa jina la Maimuna, hapo ndipo nilipoanza kuonyeshewa maisha yake, yaani kwetu sisi hujulikana kama Jini Maimuna, yaani jini ambaye hutumia sana mvuto wake kukamata wanaume.
Kabla ya kuzungumza chochote kile, mwanaume yule akaupamba uso wake kwa tabasamu pana, alijitahidi kuonyesha uchangamfu usoni mwake lakini msichana yule akabaki akimshangaa, mshangao uliomfanya aonekane mzuri zaidi.
“Mambo vipi mrembo!” alisalimia jamaa yule.
“Salama.”
“Mbona upo hapa usikuusiku, huogopi vibaka na wabakaji?’ aliuliza jamaa yule.
“Niogope nini sasa?”
“Au mfanyabiashara tufanye biashara ya chapchap?”
“Wewe kaka, umeniona mimi malaya?”
“Hapana. Ila nimeuliza tu, ila kama haupo kama ninavyofikiria, naomba unisamehe,” alisema jamaa yule.
Msichana yule hakuongea chochote, alibaki kimya huku akipiga hatua kwenda nyuma zaidi. Kumuacha msichana yule ilihitaji roho ngumu mno, jamaa yule hakutaka kukubali, mvuto wa msichana yule ulimpagawisha sana, hivyo akaona iwe isiwe ilikuwa ni lazima kumchukua usiku huo.
Jamaa alijielezeaelezea wee, mwisho wa siku msichana yule akakubaliana naye, ila kwa sharti moja tu kwamba hakuwa tayari kwenda nyumbani kwa mwanaume huyo au gesti, kama alitaka, basi usiku huohuo, sehemu yoyote isipokuwa zile sehemu alizozitaja, na baada ya hapo, wasijuane, jamaa akakubaliana naye.
Wakasogea pembeni kidogo, kutokana na usiku kuwa mkubwa, hakukuwa na watu kabisa, ni magari tu ndiyo yaliyokuwa yakipita. Walisogea nyumba mpaka walipofika sehemu iliyokuwa na mitimiti, hapo ndipo walipoamua kumalizia haja zao.
Kuwa na Chotara, mrembo, anayevutia, kulimpagawisha sana jamaa yule, akachojoa nguo zake harakaharka mithili ya mtu aliyetaka kwenda sehemu fulani, baada ya hapo, akalipandisha gauni la msichana yule, akaishusha nguo ya ndani na kisha kumlaza chini na kwenda juu yake.
Ni sauti za mahaba tu ndizo zilizokuwa zikisikika, wala hazikupita hata dakika mbili, ghafla nikamuona jamaa yule akianza kukakamaa mwili wake, akaanza kutokwa na mapovu mdomoni yaliyochanganyikana na damu, baada ya hapo, akatulia palepale kifuani.
Msichana yule akasimama, macho yake yalikuwa mekundu mno, meno yake yakabadilika na kuwa kama ya ngiri, akamwangalia kijana yule, mwili wake ukakauka, baada ya kuona kwamba amekufa, akanyoosha mikono juu kisha kupotea.
*****
“Dada! Una kampani yoyote?”
“Kampani ya nini?”
“Utakaporudi nyumbani!”
“Hapana! Kwani nini?”
“Wewe unaishi wapi?”
“Naishi Ilala!”
“Waooo! Mimi naishi Magomeni Mikumi. Naweza japo kukupa lifti manake nipo alone tu, nina usafiri mzuri tu.”
Sawa! Ila mpaka muziki uishe!”
“Haina noma.”
Yalikuwa ni mazungumzo ya watu wawili, alikuwa kijana mmoja aliyeonekana mstaarabu sana lakini uso wake ungekufanya kugundua kwamba alikuwa mlevi, alikuwa akizungumza na msichana mmoja mrembo sana katika klabu ya Usiku ya Maisha.
Kulikuwa na disko, watu walijazana mno, kila aliyecheza, alijitahidi kuonyesha umahiri mkubwa, msichana huyo ambaye alikaa peke yake, alikuwa kimya. Wanaume wengi walikuwa wakimmezea mate msichana yule mrembo, kila mtu alikuwa na shauku ya kutaka kuzungumza naye lakini hakukuwa na aliyemsogelea zaidi ya kijana huyo tu.
“Mimi naondoka!”
“Poa! Twende tu!
Wakachukuana na kisha kuelekea garini. Mwanaume yule alijiona kupata lakini ukweli ni kwamba alipatikana yeye. Alionekana kuwa mchangamfu mno, kuopoa msichana mzuri kama yule klabu, kulimfurahisha na kujiona mtu mwenye bahati sana.
Gari likawashwa na kisha kuanza safari ya kuelekea huko Ilala. Njiani, walizungumza mengi. Kijana yule alionekana kuwa na presha kubwa, alijiona kama angemkosa msichana yule au ule ndiyo ungekuwa mwisho wa kuonana naye, hivyo akaanza kutupia ndoano yake.
Kweli ikanasa, walipofika karibu na Mkwajuni, Kinondoni, jamaa akaegesha gari pembeni, akahamia kiti cha nyuma na kisha kumvuta msichana yule kulekule. Hakukuwa kilichoendelea zaidi ya kuanza kushikana hapa na pale na mwisho wa siku wote kujikuta wakiwa watupu, kilichofauata ni kuanza kufanya ngono.
Kama ilivhyokuwa kwa jamaa yule wa jana ndivyo ilivyotokea hata kwa huyu, akiwa kifuani mwa msichana yule, akaanza kukakamaa mwili wake, mapovu yaliyochanganyikana na damu yakaanza kumtoka mdomoni mwake, kilichofuata, akafariki dunia na kisha yule Jini Maimuna kupotea mulemule garini.
*****
Tetesi zikaanza kusikika ndani ya jiji la Dar es Salaam kwamba kulikuwa na mwanamke aliyekuwa akiua watu nyakati za usiku, alikuwa msichana mrembo kwa kumwangalia lakini urembo wake ule ndiyo uliowamaliza wanaume wengi.
Watu wengi walipuuzia na hivyo kuendelea kupukutika mitaani. Wengi waliogopa lakini hakukuwa na mtu aliyethubutu kuacha kumchukua msichana mrembo kama alivyokuwa Maimuna ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kupeleka damu kule kuzimu.
Ndani ya miezi miwili, tayari wanaume kumi na nne walikuwa wameuawa na miili yao kukutwa ikiwa imekakamaa.
Miongoni mwa majini yote yaliyokuwa na roho mbaya, Maimuna alikuwa na roho ya kikatili, hakuwa na huruma hata kidogo kitu kilichompelekea kukusanya kiasi kikubwa cha damu na kukipeleka kuzimu.
Ndugu yangu! Unaposikia kuhusu majini, usitegemee kila jini atakuja huku akiwa kwenye utisho mkubwa, kwa hapa Tanzania, hasa mitaani kuna majini wengi mno wanaokatiza huku wakiwa katika maumbo ya kibinadamu, ni vigumu kuwajua.
Niliendelea kubaki kuzimu kwa muda zaidi, mpaka hapo nilionyeshwa watu watatu au wanne ambao walikuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha kazi ya Mungu aiendi sawa huku duniani na kwa kiasi kikubwa walikuwa wamefanikiwa kwani kama alivyotaka shetani ndivyo kile kilichokuwa kikiendelea kilivyofanyika.
“Tunataka kuondoka,” aliniambia Yusnath.
“Kwenda wapi?”
“Kwako!”
“Wapi?”
“Duniani!”
“Kwani tushamaliza?”
“Ndiyo! Sikutaka kukuonyeshea mengi kwa huyu Maimuna kwani bado anaendelea na kazi kubwa huko duniani, cha msingi, kuwa makini na wasichana warembo wa usiku wa manane,” aliniambia Yusnath.
“Sawa. Ila hukuniambia lengo la kunileta huku usiku huu.”
“Nilitaka kukuonyeshea haya, upate kuwaambia na wenzako wawe makini.”
“Mmmh!”
“Nini?”
“Wewe ni jini au binadamu?”
“Unanionaje?”
“Sijui nijibu nini, ila unaonekana kuwasaidia wanadamu, unanishangaza,” nilimwambia Yusnath ambaye alicheka sana, naweza kusema kwamba kicheko chake kilikuwa cha ajabu mno, kilinishtua sana, hapohapo akapotea, na mimi kujikuta nikiwa nimelala kitandani, yaani usiku uleule aliokuwa amenichukua, nikajiuliza sasa mbona siku haikubadilika na wakati nilitumia siku nyingi? Sikupata jibu.
Asubuhi nilipoamka, nikayabadilisha maisha yangu, kwanza sikutaka kumuamini mtu yeyote, leo hii ninapowasikia wachungaji wakijisifia sana kwamba wanatenda miujiza, huwa ninawachukia kwa kuamini miujiza anafanya Mungu peke yake na si binadamu.
Ninaposikia kwamba maalbino wanauawa, najua wanasiasa wenye roho mbaya wapo kazini wakifanya mambo yao ya kikatili.
Ndugu yangu! Katika ulimwengu huu kuna mambo mengi sana hutokea, mengine yanaweza kuonekana kwa macho ya kibinadamu ila mengine ni vigumu sana. Tunachotakiwa ni kuishi katika misingi ya Mungu, wale wa kwenda kanisani, waende, na wale wa kwenda msikitini pia waende japokuwa hatutakiwi kuwaamini hata viongozi wetu kwani wengi wao huchukua nguvu kutoka kuzimu.
Hiyo ilikuwa safari yangu ya kwanza na ya mwisho kwenda kuzimu, ni miaka ishirini imepita, sikuwahi kuchukuliwa tena na kupelekwa huko mpaka leo hii ambapo nimemkabidhi Mungu maisha yangu na kuwa mchungaji katika Kanisa la Praise And Worship.
Yusnath hakunitokea tena, na sikutaka kusikia kitu chochote kile kutoka kwake. Nilichokuwa najaribu kukwambia ni kwamba shetani yupo kazini, unapojikwaa tu, anatokea kwa ajili ya kukuchukua na kukutumikisha maisha yako yote.
Sisi kama watoto wa Mungu! Yatupasa tumwangalie Baba yetu ambaye ni Mungu na kuachana na uovu wote wa dunia hii.

MWISHO.

No comments

Powered by Blogger.