SI KITU BILA PENZI LAKO-07
NYEMO CHILONGANI
0718069269
Mikakati ya harusi kati ya Bi Anna na Bwana Mayemba iliendelea kufanyika. Waandishi wa habari hawakuwa mbali, kila siku ilikuwa ni lazima waizungumzie harusi hiyo ambayo ilitarajiwa kufanyika siku chache zijazo.
Miezi sita waliyokuwa wamekaa katika uhusiano iliwatosha kuchunguzana na hata kuzoeana. Kupeana zawadi ndiyo ilikuwa sehemu ya maisha yao, mara kwa mara Bi Anna aliondoka Shinyanga na kuelekea Dar kwa ajili ya kuonana na mwanaume huyo ambaye siku chache zijazo angekuwa mume wake wa ndoa.
Michango ikaanza kuchangishwa, kila mtu alitoa kwa moyo kwani walikuwa na hamu ya kuwaona wapendao hao wakiingia katika maisha mapya ya ndoa. Mavazi ya bwana harusi na bibi harusi yalikuwa yameandaliwa vizuri kwa kukodishwa kutoka JM Fashion iliyokuwa Kinondoni.
Magazeti mengi yaliandika habari ya harusi hiyo, watu wa mitandao mingi ya kijamii waliitangaza harusi hiyo ya mheshimiwa, Waziri wa Wanawake na Watoto, Bwana Mayemba. Jina la Bi Anna likazidi kupata umaarufu, sasa alikuwa akijlikana Tanzania nzima kwa sababu tu alikuwa akienda kuolewa na mtu ambaye alikuwa akijulikana nchini Tanzania.
Bendi ya matarumbeta ikaagizwa kutoka nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuja kutumbuiza katika harusi hiyo. Kadi zaidi ya elfu tatu zikatengeneza kwa ajili ya kupewa kila mtu ambaye angetoa mchango wake. Magazeti yote nchini Tazania yalikuwa yakiandika habari za harusi hiyo ambayo ilikuwa ikitarajiwa kufanyika mwezi mmoja utakaofuata.
Mchungaji kutoka Ghana akaitwa kwa ajili ya kuja kufungisha harusi hiyo ambayo ilizidi kusambaa kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele. Kila mtu masikio yake aliyaweka karibu na vyombo vya habari kwa kutaka kujua siku ambayo harusi hiyo ingefugwa.
Hamu ikazidi kuongezeka mioyoni mwa watu hasa mara baada ya kutangazwa siku ambayo ilitakiwa kufanyika harusi hiyo. Viongozi mbalimbali wakaziandaa zawadi zao tayari kwa kuwapa maharusi katika siku ya harusi ambayo ilikuwa imebakia siku ishirini na moja kabla ya kufungwa katika kanisa la Praise and Worship.
Siku ziliendelea kukatika huku watu wakizidi kuisubiri siku hiyo ambayo ilitangazwa kama siku ambayo ingeweka historia kwa kufanyika harusi kubwa na ya gharama kuliko harusi zote ambazo zilitokea kufanyika nchini Tanzania.
Siku ziliendelea kukatika kama kawaida. Bwana Mayemba alionekana kuwa na shauku zaidi. Ofisini hakutulia, mara kwa mara aliwapigia marafiki zake mbalimbali na kuwataarifu juu ya harusi yake ingawa alijua fika watu hao walikuwa wakifahamu kila kitu.
“Uliniambia, na nimejipanga hasa aisee! Siku hiyo ni kucheza masebene kwenda mbele,” alisema rafiki yake kwenye simu.
Bwana Mayemba akavuta kiti chake na kutulia, akayapeleka macho yake katika saa kubwa iliyokuwa ukutani ambayo ilionyesha kwamba tayari ilikuwa saa tatu usiku. Huku akiandika majina ya watu waliotakiwa kupewa kadi hasa wale ambao walikuwa serikalini, mara simu ya mezani ikaanza kusikika ikiita.
Bwana Mayemba akakasirika. Akatamani kuacha kuipokea simu ile lakini kutokana na kelele iliyokuwa ikipiga, akaamua kuifuata na kuipokea. Akaupeleka mkonga wa simu sikioni na kuita.
“Naongea na nani?” Bwana Mayemba aliuliza mara baada ya kuitikia simu ile.
“Hutakiwi kunifahamu kwa sasa, ninajua kuwa umenisahau. Ila sitoweza kukusahau milele,” sauti ya msichana ilisikika.
Mayemba akashtuka, sauti ile ilimchanganya. Akajaribu kuvuta kumbukumbu juu ya mahali ambapo aliwahi kuisikia sauti ile, kila alipojaribu kukumbuka, hakukumbuka chochote kile.
“Wewe ni nani?” Bwana Mayemba aliuliza huku akionekana kuwa na hasira.
“Unanifahamu Mayemba. Ila kuna kitu nataka kukuambia,” sauti ya mwanamke yule iliendelea kusikika.
“Kuna kitu unataka kuniambia! Kitu gani?” aliuliza Mayemba. Tayari kijasho chembamba kikaanza kumtoka, wasiwasi ukampata, akajaribu kuvuta kumbukumbu ya maisha yaliyopita, hakupata jibu lolote lile.
“Ni lazima nitaipinga harusi yako. Harusi haitofungika,” alisema mwanamke yule.
“Utapinga harusi isifanyike? Wewe ni nani na kwa nini unataka kufanya hivyo?” Mzee Mayemba aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa zaidi ya kipindi kilichopita.
“Utanifahamu siku hiyo,” sauti ya mwanamke yule ilisikika na simu kukatwa.
“Halooo...Halooo...” aliita Mayemba lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyejibu.
Akaurudisha mkonga wa simu mahali pake. Akarudi kitini na kutulia. Uso wake ulionekana ni jinsi gani alikuwa na mawazo. Akili yake haikuwa sawa kabisa, alichanganyikiwa kupita kawaida.
Kazi aliyokuwa akiiifanya ya kuandika kadi mbalimbali hakuifanya tena, akaiacha na kutulia kochini. Kadiri dakika zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo wasiwasi ulivyozidi zaidi. Sauti ya msichana yule ilijirudia mara kadhaa kichwani mwake lakini wala hakupata jibu.
Furaha yote aliyokuwa nayo katika kipindi kilichopita ikayayuka. Kwa uchovu mkubwa, akainuka na kuelekea chumbani kwake ambako akajilaza kitandani na kutulia.
Mawazo hayakumuisha kichwani mwake, kila wakati sauti ile ilikuwa ikisikika masikioni mwake. Alibaki akiwa amechanganyikiwa, bado hakuweza kupata jibu lolote juu ya sauti ile ya mwanamke yule. Usingizi wala haukupatikana, akabaki akiangalia darini tu.
Kuanzia siku hiyo, furaha yote aliyokuwa nayo ilikuwa imepotea, hakuonekana kuwa na furaha ingawa mara kwa mara alijilazimisha kuwa na furaha. Mbele yake aliiona aibu ikimnyemelea, kitendo cha harusi yake kutaka kupingwa kanisani kilimfanya kuwa na mawazo kupita kawaida.
Siku ziliendelea kukatika na hatimaye siku iliyosubiriwa kwa hamu kuwadia. Magari zaidi ya mia moja yalipaki katika Kanisa la Praise And Worship, kanisa kubwa kuliko makanisa yote Afrika Mashariki.
Idadi ya waumini pamoja na watu wengine ambao walikuwa wamehudhuria harusi hiyo hapo kanisani ilikuwa zaidi ya watu elfu mbili. Kila kona kulikuwa na kamera za waandishi wa habari na za watu binafsi ambao walitaka kupiga picha harusi hiyo.
Kwaya moja baada ya nyingine zilikuwa zikiimba kanisani kama kuwasubiri maharusi waliokuwa njiani kuelekea kanisani hapo. Kila mtu aliyekuwa kanisani hapo alikuwa na furaha isipokuwa mwanamke mmoja tu ambaye macho yake yalikuwa mekundu hali iliyoonyesha kwamba alikuwa amelia kwa kipindi kirefu.
Dakika ziliendelea kwenda huku vigeregere vikipigwa kanisani hapo. Zilipita dakika thelathini, gari la bwana harusi likasimama katika eneo la kanisa hilo. Mayemba akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea kanisani huku akiongozana na mpambe wake.
Zilipita dakika tano, gari la bibi harusi, Bi Anna likaanza kuingia mahali hapo hali iliyowafanya wakinamama kuanza kupiga vigeregere. Bwana Mayemba akamfuata Bi Anna na kisha kuanza kuelekea nae mbele ya kanisa.
Muda wote Mzee Mayemba alionekana kutokuwa na furaha, macho yae yaliangalia kila kona kanisani mule kumtafuta mwanamke ambaye alikuwa amempigia simu usiku wa siku ile.
Mara baada ya maharusi kufika mbele ya kanisa, mchungaji Samuel Mwashambwa akaanza kuhubiri, alihubiri kwa dakika tano, alipomaliza akaziomba pete ambazo zililetwa moja kwa moja mpaka pale alipokuwa.
“Nitakwenda kufungisha ndoa hii, ndoa ambayo kila mtu alikuwa na hamu ya kuiona,” mchungaji alisema na kuendelea.
“Kwa mamlaka ambayo nimepewa, nitakwenda kuifungisha ndoa hii mchana wa leo,” mchungaji aliwaambia.
Kanisa zima lilikuwa kimya likimsikiliza mchungaji ambaye alikuwa akiendelea kuongea. Alichukua dakika mbili, akaanza kuliangalia tena kanisa lile na kutulia.
“Kabla ya kuifungisha ndoa hii, kuna mtu mwenye kipingamizi chochote cha kuzuia ndoa hii isifugwe?” mchungaji aliuliza.
Kanisa zima lilikuwa kimya, watu wakaanza kuangalia huku na kule kuona kama kulikuwa na mtu yeyote ambaye alisimama. Mchungaji akarudia kwa mara ya pili, Bwana Mayemba akaanza kuwaangalia washirika waliokuwa kanisani mule.
Japokuwa kanisani hapo palikuwa na watu wengi lakini macho ya Mayemba yakatua usoni mwa mwanamke mmoja aliyekuwa amekaa katikati ya umati ule. Alimfahamu mwanamke huyo, historia ya maisha yake ilikuwa ndefu, akawa na hofu kwa kuhisi kwamba mwanamke huyo angeweza kusimama na kuipinga ndoa hiyo, mwili wote ukamnyong’onyea.
Mwanamke yule alikuwa akilia huku akimwangalia Bwana Mayemba kwa hasira, alionekana kama kutaka kusimama na kuongea kitu ambacho alikuwa nacho moyoni. Bwana Mayemba akatamani kumzuia mwanamke yule asisimame.
“Kuna mtu ana kipingamizi cha ndoa hii kutokufungwa?” mchungaji alilirudia swali lake.
“Nakuomba Maria usisimame. Niko tayari kumlea mtoto. Nakuomba Maria usisimame,” Bwana Mayemba alisema kimoyomoyo huku akionekana kuwa na wasiwasi juu ya Maria kusimama na kuipinga harusi hiyo.
*****
Serikali ilichanganyikiwa kutokana na idadi ya watoto iliyokuwa ikipotea mara kwa mara nchini Tanzania. Ulinzi uliwekwa katika maisha ya watoto wengi lakini bado watoto hao walikuwa wakiendelea kupotea.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Bwana Nehemia Kiki alionekana kuchanganyikiwa kuliko kawaida. Kesi mbalimbali alizozipata kutoka kwa wakinamama mbalimbali kuhusiana na watoto waliokuwa wakipotea zilimchanganya.
Akaamua kujitoa na kupambana kwa nguvu zote. Maoni mbalimbali ya wakinamama yakaanza kukusanywa mitaani. Kazi ilionekana kuwa kubwa lakini alionekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana. Maoni mengi kutoka kwa wakinamama yakawa yamekwishakusanywa na kupelekwa ofisini mwake.
Alianza kuyasoma maoni yale huku akionekana kuwa makini kupita kawaida. Alipitia karatasi mbalimbali huku akionekana kuanza kuhisi kitu fulani kichwani mwake. Karatasi za maoni zilikuwa nyingi lakini alizipitia kwa haraka haraka usiku kucha na ndipo alipozimaliza.
“Inawezekana hupelekwa katika migodini na baharini,” Kamanda Nehemia alijisemea na kuzihifadhi zile karatasi.
Kwa harakaharaka akaanza kusambaza taarifa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini. Upelelezi ukatakiwa kufanyika kwa haraka sana katika migodi yote nchini pamoja na sehemu ambazo walikuwa wakitumia katika uvuvi wa samaki.
Polisi walijipanga vilivyo, ingawa taarifa ilitolewa usiku wa saa tatu lakini kila kitu kilitakiwa kufanyika kwa haraka sana. Kila polisi alimuogopa Kamanda Nehemia kutokana na ukali wake aliokuwa nao kazini na hiyo ndiyo ilikuwa sababu iliyowafanya Polisi wote kutekeleza kile alichotaka kifanyikike.
Mkuu wa polisi mkoani Shinyanga, Bwana Haji Omari mara baada ya kupewa taarifa ile, akaanza kulifanyia kazi jambo lile usiku uleule. Kwa haraka akainuka kutoka kitandani na moja kwa moja kutoka nje ambako akachukua gari lake na kuanza kuelekea katika jengo la kituo kikuu cha polisi cha mkoa wa Shinyanga.
Huko akatoa taarifa juu ya kila kitu alichoambiwa kwenye simu. Polisi zaidi ya kumi wakaingia katika magari mawili na kisha safari kuanza kuelekea Mwadui kuanza. Dakika zilizidi kusogea zaidi na zaidi huku manyunyu ya mvua yakianza kudondoka ardhini.
Polisi wote waliokuwa ndani ya magari yale walishika bunduki zao vilivyo. Bado manyunyu yaliendelea kudondoka na baada ya muda, mvua kubwa ikaanza kunyesha. Matope yakaanza kuonekana barabarani hasa katika barabara hiyo ya vumbi ambayo ilikuwa ikielekea katika Mji wa Mwadui.
Magari yalikuwa katika kasi kubwa, walitaka kuingia mgodini hapo kwa kushtukiza ili kusiwe na mtu yeyote ambaye angetambua kama usiku huo walikuwa wakielekea katika mgodi huo. Polisi waliliona gari lao haliendi kabisa, kiasi ambacho walitamani liote mabawa na kupaa.
Kwa mbali wakaanza kuziona taa za gari lililokuwa likija kwa kasi. Gari lile likazidi kusogea na hatimaye kupishana nalo. Hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa na wasiwasi na gari lile, bado walikuwa wakiendelea na safari yao ya kuelekea Mwadui.
“Simamisha gari,” ilikuwa ni sauti ya Kamanda Haji ambaye alikuwa amemwambia dereva.
Gari likasimamishwa, Kamanda Haji akataka gari lile ligeuzwe na kuanza kulifuatilia gari lile walilopishana nalo huku gari lile jingine la polisi likiendelea na safari ya kuelekea Mwadui. Tayari kamanda huyo akatilia shaka, alitaka kulifuatilia kuona ni kitu gani kilikuwa kinaendelea katika gari lile.
“Zima taa za gari. Tunataka tulifuatilie kigiza giza,” Kamanda Haji alimwambia dereva ambaye alifanya kama alivyoambiwa.
Waliendelea kulifuatilia gari lile lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi ambao uliwashangaza hata hao wenyewe. Wasiwasi ukazidi kuwaingia mioyoni mwao, tayari waliona kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kinaendelea kuhusiana na lile gari.
“Bunduki mnazo vizuri?” Kamanda Haji aliwauliza Polisi watatu alikuwa nao katika gari lile aina ya Difenda.
Gari lile likakata porini hali hiyo ikawapa uhakika asilimia mia moja kwamba gari lile lilikuwa la watu wabaya waliokuwa wakikorofishana na polisi mara kwa mara. Mara baada ya kufika katika sehemu ile, nao wakakata kona kuelekea kule gari lile lilipokuwa likielekea.
Bado mvua kubwa ilikuwa ikiendelea kunyesha huku baridi kali likiwapiga wale polisi watatu ambao walikuwa nyuma. Walitembea kwa mwendo fulani, wakalikuta gari lile likiwa limepakiwa pembeni. Kwa staili ya kikomando, wakateremka na kuanza kuelekea kule ambako walikuwa na uhakika wenye gari lile walipokuwa.
Kwa kutumia mwanga wa gari lile la wauaji, wakafanikiwa kuwaona watoto wawili wakiwa chini. Mikono yao ilikuwa imefungwa kamba huku midomoni wakiwa wamewekewa gundi ya nailoni iliyowafanya kutokuongea vizuri.
Mmoja wa wale vijana akachukua bunduki yake na kuanza kuiangalia kama alikuwa akiichunguza. Kamanda Haji na polisi wenzake wakagundua kwamba mahali hapo kulikuwa na hatari kitu ambacho kiliwafanya kuandaa vizuri bunduki zao.
“Tuanze na nani hapa? Huyu mpemba au Mswahili?” kijana mmoja alisikika akimuuliza mwenzake.
“Anza na Mpemba”
Godwin akaishika bunduki yake vilivyo na kumuelekezea Azizi pale chini alipokuwa. Azizi alikuwa akilia huku akitaka kuachiliwa na kuondoka mahali pale alipokuwa pamoja na Patrick. Huku Godwin akiwa amejiandaa kumfyatulia risasi Aziz, risasi mfululizo zikaanza kusikika, Godwin na Ally wakaanguka chini huku damu zikiwatoka.
Patrick alikuwa akilia kwa uchungu, tayari alijua kwamba rafiki yake, Azizi alikuwa ameuawa na sasa ilikuwa ni zamu yake. Polisi wanne wakatokea mahali hapo kutoka vichakani na kuwafuata Patrick na Aziz ambao walikuwa wakilia.
“Mungu wangu! Angalia, yaani ni watoto wadogo kweli, sijui kwa nini walitaka kuwaua,” Polisi mmoja aliwaambia wenzake.
“Hawa ndiyo watatuambia ukweli kwa nini watoto wanapotea na kupelekwa migodini. Cha msingi wafungueni kambana tuondoke nao,” Kamanda Haji alisema huku bado mvua ikiendelea kunyesha.
Mara baada ya kufunguliwa kamba ambazo zilikuwa zimewafunga pamoja na gundi ambazo zilikuwa zimefunika midomo yao, moja kwa moja wakachukuliwa na kupelekwa garini huku nguo zao zikiwa na matope.
Kamanda Haji alionekana kufurahia, tayari alikuwa na uhakika wa kujua juu ya kitu kilichowasumbua Watanzania. Aliamini kuwa Patrick na Azizi ni lazima wangewaambia ukweli juu ya kile ambacho kilikuwa kikitokea migodini.
“Endesha kwa kasi, nina hamu ya kuwahoji watoto hawa,” Kamanda Haji alimwambia dereva ambaye aliongeza kasi.
Gari liliendeshwa kwa kasi lakini kutokana na matope mazito ambayo yalitanda katika barabara ile ya vumbi kutokana na mvua ile kubwa, wakashangaa kuona gari lao likikwama katika matope. Dereva alijitahidi zaidi na zaidi lakini wala gari halikutoka mahali pale.
“Tufanye nini?” Kamanda Haji aliuliza.
“Inabidi mteremke na mlisukume,” dereva aliwaambia.
“Kwa hiyo wasukumaji tuwe mbele au nyuma?”
“Nendeni nyuma,” dereva aliwaambia.
Polisi wale watatu pamoja na kamanda Haji wakaelekea nyuma ya gari lile na kuanza kulisukuma huku dereva akijaribu kukanyaga moto. Kazi ilionekana kuwa bure hali iliyomfanya dereva awaambie waelekee mbele na kulisukuma kurudi nyuma. Wote wakaenda mbele ya gari lile na kuanza kulisukuma.
Patrick pamoja na Azizi walikuwa wakitetemeka kwa barini, mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha. Patrick akaanza kuangalia katika kila upande kama mtu ambaye alikuwa akiangalia noma, alipoona hali iko fresh, akamsogelea Azizi.
“Tuondoke. Tukimbie!” Patrick alimwambia Azizi ambaye alionekana kushtuka.
“Tukimbie? Tukimbie nini sasa na wakati hawa ni Polisi,” Azizi alimuuliza Patrick.
“Bado hatuko salama Azizi, ni lazima tuishi maisha ya kuhangaikahangaika tu. Hawa hawatotusaidia kabisa,” Patrick alimwambia Azizi.
“Bado unanichanganya Patrick! Hawatotusaidia?”
“Ndiyo. Wao wanataka kutuhoji tu. Hebu jifikirie wakishamaliza kutuhoji watatupa sehemu ya kuishi au watatuacha tuondoke?” Patrick aliuliza.
“Watatuacha tundoke.”
“Basi haina maana. Tuondoke Azizi.” Patrick alimwambia Azizi huku akimshika mkono.
Hakukuwa na muda wa kuchelewa, kutokana na Polisi wale kuwa mbele ya gari lile, hawakuweza kuwaona Patrick na Azizi ambao walikuwa nyuma ya gari lile aina ya Difenda. Patrick na Azizi wakaanza kukimbia kuelekea Porini. Hawakujua walikuwa wakielekea wapi ila wao kitu walichokijua ni kuondoka, hawakutaka kuishi na mtu yeyote yule, walitaka kuhangaika kivyao.
Mara baada ya kusukuma gari lile na kuona imeshindikana, wakaamua kurudi tena nyuma ya gari kwa ajili ya kusukuma. Wote wakapigwa na mshangao, Patrick na Aziz hawakuwa garini pale hali iliyowachanganya.
“Mungu wangu! Wamekimbia! Ingieni vichakani, watakuwa hawajafika mbali, zifuateni alama za miguu yao. Tunawahitaji watoto hawa. Yaani wao ndiyo wa kutueleza kila kitu,” Kamanda Haji aliwaambia Polisi huku akionekana kuchanganyikiwa. Polisi wote wakaingia vichakani kwa ajili ya kuwatafuta Patrick na Azizi kwa kufuatilia alama za miguu yao.
Je, nini kitaendelea?
Je, polisi hao wataweza kuwapata watoto hao?
Je, ndoa ya Bwana Mayemba na Anna itapingwa na mwanamke Maria?
Post a Comment