SI KITU BILA PENZI LAKO -06
NYEMO CHILONGANI
0718069269
Victoria alikuwa akikimbia kuelekea mbele zaidi. Machozi bado yalikuwa yakimtoka, moyoni aliumia kupita kiasi. Vibao ambavyo alipigwa na baba yake vilionekana kumkasirisha kupita kiasi. Hakutaka kurudi tena kijijini kwao, aliona ni bora kuendelea na safari, kutafuta maisha mapya.
Kila wakati taswira ya Patrick ilikuwa ikionekana kichwani mwake, wakati mwingine alikuwa akitabasamu huku akijiona kuwa mtu wa bahati kupendwa na mtu kama Patrick. Alimpenda Patrick kuliko mvulana yeyote katika maisha yake, aliyatoa maisha yake kwa ajili yake na ndio maana hata aikuwa radhi kuutoa usichana wake kwa mvulana huyo.
Pori lilikuwa na giza kubwa lakini macho ya Swema yalionakana kuwa na nguvu ya kuona kila kitu ardhini. Aliruka vishimo na magogo kadhaa. Woga wote ambao alikuwa nao ulikuwa umemtoweka, hakuogopa giza tena kwa wakati huo.
Mara kwa mara Victoria alikuwa akipumzika chini ya miti na kisha kuendelea na safari kama kawaida. Hakujua alikuwa akielekea upande gani, kitu ambacho alikuwa akikijali ni kuukimbia mkono wa baba yake, mzee Carlos ambaye alionekana kukasirika kuliko kawaida.
Victoria alikimbia zaidi na zaidi huku masaa yakiendelea kukatika, kwa mbali macho yake yakaanza kuona mwanga wa taa kadhaa. Victoria akaachia tabasamu kwani tayari alikwishaona kuwa mahali pale ndipo ambapo angepata msaada wa kulala na kisha kesho kuendea na safari ambayo hakuwa akiifahamu.
Akajikuta akipata nguvu ya ziada na kuzidi kukimbia zaidi na zaidi kuelekea kule ambako kulionekana kuwa na nyumba chache. Kadri alivyozidi kukimbia na ndivyo ambavyo matumaini yalivyozidi kuongezeka moyoni mwake.
Akafika katika uwanja mkubwa ambao kwa mbele kulikuwa na nyumba kadhaa. Victoria akaanza kupiga hatua kuzifuata nyumba zile huku macho yake yakiangalia huku na kule. Hakukuwa na mtu yeyote nje zaidi ya ng’ombe ambo walikuwa wamefungiwa zizini.
Victoria akaanza kupiga hatua huku akiangalia katika kila upande. Mara ng’ombe wakaanza kupiga kelele. Victoria akaonekana kushtuka, akasimama na kuanza kuangalia kila upande huku akionekana kuanza kushikwa na wasiwasi.
Wanaume kama nane wakatokea kutoka katika vichaka walipokuwa wamejificha na kuanza kumsogelea Victoria kwa kasi. Hakukuwa na mtu aliyemuuliza kitu chochote kile zaidi ya kumvamia na kuanza kumshambulia kwa kumchapa fimbi mfululizo na kumpiga kwa marungu waliyokuwa wameyashika.
Victoria akadondoka chini na kuanza kulia. Hakukuwa na mtu aliyeonekana kujali, bado walikuwa wakiendelea kumshambulia kwa nguvu huku wakionekana kuwa na hasira. Victoria alikuwa akitokwa na damu katika sehemu kubwa ya mwili wake, mbele yake akaanza kuona giza ambapo baada ya muda, hakuonekana kujua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea.
“Tumewakomesha sasa. Huyu ni wa kwanza, kuna wengi watakuja, kazi yetu itakuwa ni hii hii, kuwaua tu” Kijana mmoja aliwaambia wenzake huku wakipongezana kwa furaha kwa kitendo kile cha kumpiga Victoria mpaka kutokujitambua.
“Mhhhhhh...!” Kijana mmoja alisikika akiguna hali iliyomfanya kila mtu kumwangalia.
*****
Kila mtu alikuwa akimwangalia mganga ambaye alikuwa amemaliza sala yake ya kuikabidhi damu ya Patrick mikononi mwa miungu yake. Akayarudisha macho yake kwa Patrick na kukishika vizuri kisu chake kilichokuwa na makali pande zote mbili.
Akakipeleka shingoni mwa Patrick huku akijiandaa kumchinja kama kawaida yake. Muda wote huo Patrick alikuwa akisali sala yake ya mwisho huku machozi yakiendelea kumtoka, hakuamini kama siku hiyo ndio ilikuwa siku yake ya mwisho kuvuta pumzi ya dunia hii.
Kila mmoja aliyekuwa mahali hapo alishtushwa na mlio wa simu ambayo ilikuwa ikiita. Mganga akaacha kile ambacho alikikususdia kukifanya na macho yake kumwangalia kila mtu huku akitaka kujua ni nani ambaye alikuwa ameiacha simu yake ikiwa imewashwa.
Kila mmoja akamwangalia Bwana Mayasa ambaye alikuwa akijipapasa na kuitafuta simu yake. Hakukuwa na mtu aliyesema kitu chochote kile, kwani bosi ndiye ambaye alikuwa amefanya kosa kwa kuiacha simu yake ikiwa imewashwa.
Bwana Mayasa akaonyesha ishara ya kuomba msamaha na kuipokea simu ile na kuipeeka sikioni. Kila mmoja alikuwa kimya akimwangalia Bwana Mayasa ambaye muda wote wa maongezi alionekana kama mtu ambaye alishtushwa na kitu fulani.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo mkuu. Yaani hapa ninapoongea, wako njiani wanakuja huko” Sauti ya kijana fulani ilisikika simuni.
Bwana Mayasa akaonekana kuchanganyikiwa upita kiasi, akakata simu ile na kuanza kumwangalia kila mtu mahali pale. Mganga akataka kuendelea kwa kukirudisha kisu chake shingoni mwa Patrick kwa ajili ya kumchinja kama ambavyo ilikubaliwa.
“Ngoja kwanza” Bwana Mayasa alimwambia mganga ambaye alionekana kushtuka.
Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akiamini kama Bwana Mayasa angeweza kumsimamisha mganga ambaye alitaka kfanya kile alichotaa kukifanya. Hawakuelewa sababu iliyompelekea kumsimamisha mganga kwani jambo hilo halikuweza kutokea toka miaka kumi iliyopita katika kipindi kazi hiyo ilipoanza.
“Wanakuja” Bwana Mayasa alimwambia mganga.
“Wanakuja? Wakina nani?” Mganga aliuliza huku akiwa ameacha kufanya kile alichotaka kukifanya.
“Mapolisi. Wanakuja kufanya uchunguzi mashimoni. Usifanye hivyo, acha kwanza kwani hali inaweza kuwa ya hatari kwetu” Bwana Mayasa alimwambia mganga.
“Kwa hiyo hawa watoto tuwafanye nini bosi?” Godwin alimuuliza Bwana Mayasa.
“Waacheni waondoke”
“Hauoni kama siri hii inaweza kujulikana?”
Bwana Mayasa akaonekana kushtushwa kutoka katika hai fulani. Tayari aliona kama angewaacha Patrick na Aziz basi ni lazima watoto hao wangekwenda kutangaza kile ambacho kilikuwa kikitokea mashimoni. Kukaonekana kutokuwa na sababu ya kuwaacha watoto hao hai, ilikuwa ni lazima wawaue ili kuilinda siri hiyo.
“Basi wapotezeni. Ila msifanyie hapa mgodini, nendeni nao porini, tena mbali kabisa na hapa ili miili yao iende ikaliwe na wanyama wa mwituni kupoteza ushahidi” Bwana Mayasa aliwaambia.
Hakukuwa na cha kupoteza, kila kitu kikaanza kufanyika haraka haraka. Patrick na Aziz wakabebwa juu juu na kupelekwa nje ya shimo lile. Patrick akajiona kuwa na bahati kubwa, hakuamini kama kweli walikuwa wamenusurika kutoka katika mdomo wa kifo.
Wakapakizwa garini na moja kwa moja Godwin na Ally kuingia garini na safari ya kuelekea porini kuwaua Patrick na Azizi kuanza.
Patrick na Aziz walibaki kimya garini, bado walikuwa wakiona kuwa katika hali ya hatari. Manyunyu yakaanza kudondoka na hatimae mvua kubwa kuanza kunyesha. Patrick akaonekana kukosa tumaini, tayari alijiona kuelekea kuuawa pamoja na rafiki yake, Aziz.
Godwin na Ally muda wote walikuwa wakifurahia tu, bunduki zilikuwa zikiandaliwa vizuri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wasingechukua hata dakika moja katka kukamilisha kile ambacho walikuwa wanakwenda kukifanya.
Gari likakatwa kona na kuingia porini. Mvua ambayo ilikuwa imenyesha ilisababisjha matope ardhini lakini kutokana na gari lao kuwa na nguvu, liliweza kupita bila tatizo lolote lile.
Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka katika sehemu ambayo ilionekana kuwa wazi kidogo, wakasimamamisha gari lao na kisha kuteremka.
“Vipi hapa! Kunafaa?” Godwin alimuuliza Ally.
“Pako mzuka. Kama vipi tuwateremshe tuwaue fasta fasta tukaendelee na kazi zetu” Ally alimwambia Godwin.
Patrick na Azizi wakateremshwa kutoka garini na kuwekwa chini. Kila mmoja alikuwa akilia mara baada ya kumuona Godwin akiikoki bunduki yake kwa mbwembwe. Tayri walijiona kutokuwa na nafasi ya kunusurika kutoka katika mikono ya watu hao ambao walionekana kuwa hatari katika maisha yao.
“Nani aanze kufa? Huyu Mpemba au huyu mswahili?” Godwin alimuuliza Ally ambaye alikuwa ameegemea gari akivuta sigara.
“Anza na mpemba” Ally alijibu.
Godwin akamnyooshea Aziz buduki tayari kwa kumfyatulia risasi. Muda wote Azizi alikuwa akilia, tayari alijiona kuwa muda huo ndio ambao alikuwa akienda kufa na kuungana na wazazi wake ambao walikufa kipindi kirefu kilichopita.
“Paaa...paaa...paaa..paaa...” Milio ya risasi ikasikika mahali hapo.
Patrick alikuwa akilia, hakuamini kama huo ndio ulikuwa mwisho wa kumuona Azizi maishani mwake. Sasa aliiona zamu yake ikifuata.
Je, nini kitafuatia?
Je, Patrick atapigwa risasi?
Post a Comment