SI KITU BILA PENZI LAKO - 05
NYEMO CHILONGANI
Patrick na Aziz walikuwa wamelala katika hema walilokuwa wakilitumia mgodini hapo. Muda ulikuwa umekwenda sana, wadudu wadogowadogo walikuwa wakisikika wakilia kutoka maeneo tofautitofauti katika sehemu hiyo.
Walinzi waliendelea kuhakikisha usalama mahali hapo huku wakiwa na bunduki zao ili hata kama kungekuwa na mtu yeyote ambaye angekuja kufanya uhalifu kwa bunduki, basi waweze kupambana naye. Hali ya usalama mkubwa ilitawala mgodini hapo ambapo idadi kubwa ya watu waliokuwepo mahali hapo walikuwa vijana wa rika mbalimbali.
Vijana watatu waliovalia makoti makubwa meusi wakaonekana wakianza kulifuata hema ambalo Patrick na Azizi walikuwa wanatumia kama chumba chao. Mara baada ya kulifikia, wakaingia ndani na kuwafuata.
Kwa haraka sana wakawafumba midomo yao kwa kutumia mikono yao waliyoivarisha grovu. Patrick akataka kupiga kelele, akabaki akinguruma tu, akataka kumwamsha Aziz kwa kumtikisa lakini naye Azizi alikuwa amefumbwa mdomo kama alivyofumbwa yeye.
Wakatolewa kutoka katika hema lile kupelekwa katika shimo moja kubwa liliokuwa likitumika katika uchimbaji madini. Walinzi hawakusema kitu chochote kwani kila kilichokuwa kikiendelea mahali hapo, walipewa taarifa.
Watu zaidi ya saba walikuwa wamekusanyika katika shimo lile huku pembeni yao kukiwa na mzee mmoja mchafu ambaye alikuwa ameshika kisu kilichokuwa kikali. Hakukuwa na swali lolote juu ya mzee yule, kwa kumuangalia mara moja tu na kwa jinsi alivyovaa, alionekana dhahiri kuwa mganga wa kienyeji.
Patrick na Aziz wakawekwa chini na kufungwa kamba vilivyo. Walijaribu kupiga kelele lakini wala zao hazikutoka. Watu wote waliokuwa mahali pale wakaanza kumwangalia mganga katika mtazamo uliomaanisha kwamba alikuwa akisubiriwa yeye tu.
Bwana Mayasa akatoa tabasamu pana ambalo lilibeba matumaini makubwa. Kila kitu kwake kikanekana kukamilika, alitarajia kuona madini yakichibwa kwa wingi mara tu kazi ya kuwatoa sadaka Patrick na Azizi kukamilika.
Mganga akaanza kumwangalia Patrick na Azizi kwa makini kana kwamba alikuwa akiwachunguza. Aliporidhika, akachukua kisu kile na kukinyoosha juu. Akaanza kuongea maneno yasiyoeleweka na watu waliokuwa wamesimama shimoni pale.
Muda wote Patrick na Aziz walikuwa wakilia, tayari walikiona kifo kikiwa mbele yao. Patrick akashindwa kujizuia, akaanza kulia, hakuamini kama zilikuwa zimebakia sekunde chache za kuvuta pumzi ya dunia hii na kumfuata baba yake kule alipokuwa.
Mganga hakuchukua muda mrefu kuwakabidhi Patrick na Azizi kwa miungu yake. Akaagiza chungu ambacho mara kwa mara kilikuwa kikiwekewa damu kisogezwe mbele yake, kwa harakaharaka kikasogezwa. Akainama na kisha kumvuta Patrick karibu naye.
Muda wote huo Patrick alikuwa akilia, kisu kilichokuwa na makali pande zote kilionekana vizuri machoni mwake. Tayari alijiona kukaribia kifo, akaanza kusali sala yake ya mwisho katika kasi ambayo ilimshangaza hata yeye mwenyewe.
Mganga akaridhika na sala yake aliyokuwa amesali katika kipindi kichache kilichopita. Alichokifanya ni kumsogeza Patrick karibu na chungu kile na kisha kukisogeza kisu shingoni mwa Patrick ambaye alikuwa akilia huku akikukuruka huku na kule.
“Majini..miungu yetu...pokeeni damu hii kama chakula chenu cha kila siku” Mganga alisema kwa sauti ndogo lakini iliyosikika vizuri masikioni mwa Patrick.
*****
Bado Bi Anna alikuwa akiendelea na harakati zake za kuwatetea wanawake ambao kila siku wao walikuwa watu wa kufanya kazi nyingi huku waume zao wakiwa wanakunywa kahawa na kupiga soga. Kila siku idadi ya wanawake ilizidi kuongezeka katika kikundi chao mpaka kufikia wanawake elfu moja.
Bi Anna akaamua kukipeleka kikundi kile Shinyanga Mjini ambako kwa mchango mkubwa wa wanawake, ofisi ikatengenezwa na kuwa kama ofisi kuu ya chama hicho. Idadi ilizidi kuongezeka zaidi mara baada ya wanawake ambao walikuwa wakiishi mjini kujua malengo ya kikundi kile.
Jina la Bi Anna likaanza kusikika katika kila kona mkoani Shinyanga, kila mwanamke ambaye alikuwa nje ya kikundi kile alitamani kujiunga na kikundi kile. Wanawake kutoka katika mikoa mbalimbali, nao walikuwa wakijiunga katika kikundi hicho ambacho kilikuwa kikishika kasi kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Ndani ya miezi sita, kikundi hiki cha wanawake kikaamua kuchangishana michango na kutengeneza nyumba nzuri ambayo wakaamua kumpa mwenyekiti wao, Bi Anna kuitumia katika siku zote ambazo ataendelea kuwa mwenyekiti wao.
Bi Anna akaona maisha kuanza kubadilika, akaanza kujiona mtu mwenye thamani sana katika maisha yake. Hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuishi katika nyumba ambayo ilikuwa na umeme pamoja na maji. Kila wakati alikuwa akijiona kuwa mwanamke aliyepangiwa mambo mengi sana katika maisha yake.
Moyo wake haukuwa sawa, kila wakati alikuwa akiifikiria familia yake. Aliikumbuka vizuri sana siku ambayo mume wake, mzee Innocent aliuawa kwa kushambuliwa na vijana katika Kijiji cha Chibe. Bado moyo wake ulikuwa na mamivu kadiri alivyokuwa akilikumbuka tukio lile.
Hakujua kama mwanaye, Patrick alikuwa ameuwa kama alivyouawa mumewe au alikuwa hai. Kila siku alikuwa akimuomba Mungu amlinde mtoto wake kama alikuwa hai ili baadaye waweze kuonana tena.
Nyumba ile kwake ilikuwa kubwa, kila kitu kilichohitajika katika maisha ya binadamu kilipatikana katika nyumba ile. Maisha yake yalikuwa ya upweke, bado alionekana kuihitaji familia yake iwe pamoja naye.
Mara kwa mara kikundi chake kilikuwa kikifanya mikutano mbalimbali katika Mkoa wa Shinyanga. Wanawake walikuwa wakijaa kwa wingi katika mikutano hiyo iliyoonekana kumvutia kila mtu, hata wanaume nao walikuwa wakishiriki katika mikutano hiyo.
Kikundi kile kikaanza kutembea katika mikoa mbalimbali ya karibu na kuendelea kuongea maneno ambayo yalikuwa yakiwatetea wanawake waliokuwa wakifanyishwa kazi kama punda.
“Kuna mkutano wa wanawake unatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam. Na wewe kama mwenyekiti wetu tumeamua uende ukatuwakilishe,” Bi Stumai, katibu wa kikundi hicho alimwambia Bi Anna aliyenekana kushtuka.
“Unasema kweli? Taarifa hizo zimekuja lini?” aliuliza Bi Anna.
“Zilikuja juzi hapa ofisi. Nilikuwa nakusubiri urudi kutoka Mwanza ili nikueleze jambo hili,” Bi Stumai alimwambia.
Bi Anna akashusha pumzi ndefu, hakuonekana kuziamini taarifa zile. Alijiona kuwa kama alikuwa ndotoni ambapo baada ya muda angeamka kutoka katika usingizi mzito. Akaanza kumwangalia Bi Stumai huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa amemwambia.
Kila siku alikuwa na ndoto za kufika jijini Dar es Salaam. Mara kwa mara alikuwa akisikia sifa mbalimbali kuhusu Jiji la Dar es Salaam hali ambayo alitamani sana nae kuingia ndani ya jiji hilo. Taarifa ile ilionekana kumchanganya kupita kiasi.
Moyo wake uliamini kwamba kitu chochote ambacho kingefanyika ndani ya jiji la Dar es Salaam basi kilikuwa na uwezo mkubwa sana kusikika Tanzania nzima kutokana na kuwa na vyombo vingi vya habari. Alitamani ajitangaze ili Tanzania nzima kumfahamu yeye ni nani na alikuwa na malengo gani katika maisha yake. Muda wote alijisikia kuruka ruka kwa furaha, safari ya kwenda Dar es Saaam ilionekana kumchanganya kupita kiasi.
“Safari yenyewe inaanza lini?”
“Keshokutwa” Bi Stumai alimwambia.
*****
Bado Bi Anna aliifikiria safari ya kuelekea Dar es Salaam. Kila siku alikuwa akiiota safari hiyo ambayo kwake ilionekana kuwa kama tukio kubwa ambalo lilikuwa linakwenda kutokea. Vijana wengi ambao walikuwa wamefika Dar es Salaam na kurudi kule kijijini walikuwa wakielezea uzuri wa Dar es Salaam pasipo kuzungumzia mambo mengine machafu ambayo yalikuwa yamekithiri.
Kila mtu akaonekana kutaka kuhakikisha kwa macho yake kile ambacho alikuwa akiambiwa lakini tatizo lilikuwa ni kutokupata fedha za kwenda Dar es Salaam na kuliona kwa macho yao jiji hilo ambalo lilionekana kuwa na mambo mengi.
Masaa aliyaona yakikawia, kichwa chake kilikuwa kikiendelea kufikiria safari hiyo ambayo bado ilikuwa ikiendelea kukaa kichwani mwake. Bi Anna bado alionekana kuwa na hamu ya kuwa pamoja na familia yake kwani aliamini kama tu angekuwa na hata mtoto wake Patrick pamoja nae, basi nae angekuwa na nafasi kubwa ya kuelekea Dar es Salaam kusafisha macho.
Siku moja kabla ya safari, Bi Anna hakulala usiku, kichwa chake kilikuwa kikiifikiria safari hiyo ambayo kwake ilionekana kuwa kama muujiza mkubwa. Kila wakati ambao alikuwa akpata usingizi kidogo, alikuwa akishtuka na kuangalia nje kuona kama kumepambazuka.
Masaa yaliendelea kukatika huku mabegi yake yakiwa tayari kwa ajili ya safari. Alamu ya simu yake ikaanza kusikika, akaamka na kuanza kujiandaa. Wala hazikupita dakika hata tano, wanawake wanne wakaingia ndani ya nyumba hiyo na baada ya muda wakaanza kumsindikiza katika kituo cha mabasi ambapo akapanda basi na saa kumi na mbili kamili basi kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam.
Bi Magdalena alibaki akiangalia dirishani huku kumbukumbu zake zikimrudisha nyuuma kabisa katika kipindi ambacho alikuwa pamoja na familia yake. Alimkumbuka sana marehemu mumewe ambaye aliuawa baada ya kuhisiwa kuwa ni mchawi, kumbukumbu zake hazikuishia hapo, alimkumbuka na mtoto wake, Patrick huku akionekana kutokuwa na uhakika kama alikuwa hai au nae alikuwa ameuawa siku ile.
Basi liliingia katika kituo cha Ubungo Terminal saa moja usiku, Bi Anna akateremka na kuanza kupiga hatua kuwafuata wanawake wawili ambao walikuwa wamesimama huku wakionekana kumwangalia katika mtazamo wa kutaka kumuuliza kitu.
“Bila shaka wewe ndiye Bi Anna” Mwanamke mmoja alimwambia Bi Anna huku uso wake ukiwa umejaa tabasamu.
“Ni mimi” Bi Anna alijibu.
Hakukuwa na sababu ya kupoteza muda kituoni hapo, kitu walichokifanya ni kukodisha teksi na moja kwa moja kuanza safari ya kuelekea hotelini. Ndani ya dakika thelathini wakawa wamekwishafika katika hoteli ya La Vista Inn ambako moja kwa moja wakaelekea ndani ambako walikuwa wamechukua chumba kimoja.
Bi Anna alibaki akikiangalia chumba kile mara mbili mbili. Televisheni kubwa ilikuwa imewekwa ukutani, taa mbalimbali zilizokuwa na mianga tofauti zilikuwa zikiendelea kumulika katika chumba hicho. Bi Anna aliendelea kushangaa, kila kitu kwake kilionekana kama ndoto ambako baada ya muda fulani angeamka kutoka katika usingizi mzito.
Muda wote Bi Anna aliuona mguu wake kukanyaga kitu cha tofauti ambacho hakuwa na ukakika kama alikwishawahi kukikanyaga toka azaliwe. Kapeti lililokuwa na manyoya lilikuwa limetandikwa katika sakafu ya chumba kile. Kila kitu ambacho alikuwa akikiangalia kilionekana kuwa kigeni machoni mwake.
“Kesho utakuja kuchukuliwa na gari kupelekwa katika mkutano ambao utachukua siku tatu” Mwanamke mmoja alimwambia Bi Anna.
“Saa ngapi?”
“Saa tatu asubuhi”
Wanawake wale wakaondoka chumbani mule na kumwacha Bi Anna peke yake. Muda wote alikuwa akikiangalia chumba kile. Dhahiri alijiona kuwa katika ulimwengu mwingine ambao ulikuwa ulimwengu wa maajabu. Akakifuata kitanda na kukalia, akazidi kujisikia utfauti.
Kijijini Chibe alizoea kulalia kitanda cha kamba mpaka pale alipohamia Shinyanga mjini ambako kulikuwa na nyumba ambayo alipangiwa, huko ndipo ambapo alipoanza kulali kitanda ambacho kilikuwa na mvuto. Kitanda ambacho alikuwa amekikalia kwa wakati huo chumbani hapo kilionekaa kuwa tofauti na vitanda vyote ambavyo alikuwa amevilalia katika maisha yake kwani kitanda kile kilikuwa na mvuto wa juu ambao hakuwahi kuuona.
“Mmmmh! Hadi saa tatu nitakuwa nimeamka kweli! Nisije nikachelewa” Bi Anna alijisemea.
Bi Anna akajiandaa na kuelekea bafuni, mshangao wake ukaongezeka zaidi na zaidi. Akili yake ikahama kabisa na kujiona alikuwa katika ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa. Sinki kubwa la kuogea lilikuwa likionekana vizuri machoni mwake.
Akaanza kulisogelea na kulishika huku akionekana kuogopa kwa kuona kwamba angelichafua. Akafungua koki ya bomba na maji kuanza kutoka. Kia kitu ambacho alikiona katika usiku huo kilionekana kumshangaza kupita kiasi, bado alijiona kuwa mwanamke ambaye alikuwa na bahati kubwa katika maisha yake.
Asubuhi ilipofika, Bi Anna akaamka na moja kwa moja kuletewa kifungua kinywa na baada ya kumaliza, akapelekwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee kwa ajili ya mkutano wa wanawake wa kitaifa ambao ulikuwa ukifanyika mahali hapo.
Wanawake zaidi ya mia saba walikuwa wamekusanyika katika ukumbi huo huku wakiendelea kupiga stori. Walikuwa wapo tayari kwa kuanza mkutano lakini Waziri wa wanawake na watoto, Bwana Hidifonce Mayemba hakuwa amefika mahali hapo.
Zilipita dakika thelathini, gari moja la kifahari likaanza kuingia katika eneo la ukumbi ule ambapo wanawake wote wakaamriwa kutoka ukumbini na kwenda kumkaribisa waziri Mayemba. Vigeregere vilikuwa vikisikika kutoka kwa wakinamama hao katika kipindi ambacho Bwana Mayemba alikuwa akipiga hatua za taratibu kuelekea ukumbini huku akiwapungia mkono.
Mkutano ukaanza rasmi huku baadhi ya waandishi wa habari wakiwa wamekusanyika mahali hapo kwa ajili ya kupiga picha na kuandika kila kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Mara baada ya Waziri kuelekea ukumbini, mkutano ukaanza mara moja.
Kila mwanamke alikuwa akiongea kile kitu ambacho alikuwa amekiandika au kuandikiwa katika karatasi. Maneno mazito yalikuwa yakiongelewa mahali hapo, maneno ambayo yalikuwa yakimaanisha kwamba wanawake walikuwa wakitaka kupewa nafasi kubwa katika jamii.
Waziri Mayemba alikuwa akiandika mambo mengi ambayo yalikuwa yakizungumziwa mahali hapo, hakutaka kupitwa na kitu chochote kile. Wanawake tisa walikuwa wameongea na ni Bi Anna tu ndiye ambaye alikuwa amebakia kwa ajili ya kuwawakirisha wanawake wote wa kanda ya ziwa.
Bi Anna aliongelea mambo mengi ambayo yalionekana kumgusa kila mtu aliyekuwepo mahali hapo. Alionekana kuwa kama mwanamke ambaye alikuwa na elimu ya juu, kuanzia ngazi ya digrii. Maneno aliyoongea yalikuwa mazito ambayo mara kwa mara yaliwafanya watu waliokusanyika mahali hapo kutikisi vichwa vyao.
“Tunahitaji kushirikishwa katika jamii kwa kila kitu, hatutaki kubaguliwa na kuonekana kama hatuna mchango wowote ule katika jamii. Tunataka tupewe haki sawasawa na wanaume hata kama wao walichangia kwa asilimia kubwa kututafutia uhuru” Bi Anna alimalizia na kuondoka kuelekea kitini kwake. Makofi mazito na vigeregere vilikuwa vikiendelea kusikika ukumbini hapo, Bi Anna alionekana kuongea maneno makali kwa jamii.
Waziri Mayemba alibaki akishangaa, muda wote alikuwa akimwangalia Bi Anna huku akionekana kumsnagaa. Ni kweli alikuwa ameongea maneno mazito ambayo kila mtu aliyeyasikia ni lazima angemuona mwanamke huyo kuwa msomi lakini kuna kitu ambacho kilikuwa kikimfanya kumshangaa zaidi Bi Anna, uzuri wake.
Ni kweli Bwana Mayemba alikuwa amewaona wanawake wengi lakini kwa Bi Anna alionekana kuwa tofauti kabisa. Uzuri wake ulionekana kumvutia kuliko kawaida, alimwangalia katika kila hatua ambayo alikuwa akitembea mpaka kitini kwake.
Akabaki akiwa akimshangaa tu, macho yake yalikuwa yameganda usoni mwa Bi Anna ambaye hadi katika kipindi hicho, moyo wake ulikuwa umetekwa kupita kiasi. Mpaka Bwana Mayemba anakaribishwa mbele kwenda kufunga mkutano, hakuwa amesikia kabisa, bado macho yake yalikuwa yakimwangalia Bi Anna.
“Mheshimiwa....” Mwendesha mwenyekiti alimuita kwa mara ya tatu.
Bwana Mayemba akaonekana kushtushwa kutoka katika lindi la mawazo. Akasimama huku uso wake ukiwa na tabasamu pana. Wala hakutaka kuongea sana kwani bado alijiona kutaka nafasi zaidi ya kutaka kuongea na Bi Anna.
Baada ya dakika kadhaa, mkutano ukafungwa na wanawake wote kwenda nje. Waandishi wa habari wakaanza kumfuata waziri Mayemba na kuanza kumhoji maswali kadhaa. Kila kitu alicholizwa, alikijibu haraka haraka, katika kipindi hicho alikuwa akitaka kuachiwa nafasi ili amfuate Bi Anna.
“Nadhani nimemaliza” Bwana Mayemba aliwaambia waandishi wa habari na kisha kuanza kumfuata Bi Anna ambaye alikuwa amesimama pembeni.
Kadri alivyokuwa akizidi kumsogelea Bi Anna na ndivyo ambavyo mapigo yake ya moyo yalivyozidi kumdunda zaidi na zaidi. Hakuonekana kujiamini kabisa, akaanza kuusikia mwili wake ukipigwa na kijibaridi cha mbali.
“Habari za mchana” Bwana Mayemba alimsalimia Ni Anna huku akimwangalia usoni.
“Nzuri tu. Karibu Mheshimiwa” Bi Anna alimwambia Bwana Mayemba.
Bwana Mayemba hakutaka kutoa jibu la haraka haraka, akabaki akimwangalia Bi Anna kwa umakini. Uzuri wake ukaonekana kumvutia zaidi na zaidi. Akatamani kumwambia ukweli mahali hapo ili amkumbatie na kumbusu, alionekana kulitamani joto la mwanmke huyo ambaye alikuwa akionekana kuwa na kila aina ya mvuto machoni mwake.
“Samahani kama nitakuwa nakusumbua” Mzee Mayemba alimwambia Bi Anna
“Usijali Mheshimiwa”
“Hivi una nafasi jioni ya leo?”Bwana Mayemba alimuuliza Bi Anna ambaye akaonekana kuanza kusikia aibu kutokana na macho ya Bwana Mayemba kuwa usoni mwake muda wote.
“Ndio” Bi Anna alijibu kwa kifupi.
“Ningependa kupata chakula cha usiku pamoja nawe” Bwana Mayemba alimwambia Bi Anna.
“Usijali Mheshimiwa” Bi Anna alijibu.
Huo ndio ukawa mwanzo wa mawasiliano kati yao. Katika siku tatu ambazo Bi Anna alikuwa jijini Dar es Salaam muda mwingi alikuwa pamoja na Bwana Mayemba huku wakielekea katika sehemu mbalimbali kutembea.
Bi Anna alijiona kuwa na bahati hasa mara baada ya Bwana Mayemba kumwambia kuhusu kile ambacho kilikuwa kinaendelea moyoni mwake. Bi Anna hakuleta kipingamizi chochote kile, kitendo cha kutoka out kwenda kutembea tayari kilikuwa kimfanya kuvutiwa na Bwana Mayemba.
“Na vipi kuhusu mkeo?”
“Mke wangu alifariki miaka miwili iliyopita, wala hatukufananikiwa kupata mtoto hata mmoja” Bwana Mayemba alimwambia Bi Anna.
“Pole sana”
“Usijali. Nimkwishapoa. Vipi kuhusu wewe?”
Swali hilo ndilo ambalo lilimfanya Bi Anna kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea maishani mwake. Ilionekana kuwa kama hadithi fulani ambayo ilikuwa ikisisimua kupita kiasi. Bwana Mayemba alimwangalia Bi Anna mara mbili mbili, hakuamini kama mwanamke huyo alikuwa amepitia katika maisha magumu kiasi hicho.
“Hivi kweli kuna watu wana roho mbaya namna hiyo hapa Tanzania?” Mzee Mayemba aliuliza huku akionekana kushangaa.
“Wapo. Wamejaa vijijini kwetu”
Mara baada ya wiki moja kukatika ndipo Bi Anna akarudi mkoani Shinyanga. Hakutumia basi tena, safari hii alikatiwa tiketi ya shirika la ndege la Precious na kurudi Shinyanga.
Mawasiliano ndicho kilichoendelea katika maisha yao. Kila siku mapenzi ya watu hawa wawili yalikuwa yakiongezeka kiasi kwamba hata wao wenyewe walijishangaa. Mipango mingi wakaipanga maishani mwao, ni kitu kimoja tu ndicho ambacho kilikuwa kikisubiriwa, ndoa.
Je, nini kitaendelea?
Post a Comment