ad

ad

Meneja wa Global Afunguka, Asema Maoni ya Shigongo Hayahusiani na Shoo ya Dar Live



MWISHONI mwa wiki iliyopita ulizuka mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya Mkurugenzi wa Global Publishers Limited, Eric Shigongo, kuandika ushauri kwa msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul maarufu Diamond Platnumz na mameneja wake, Hamsi Taletale au Babu Tale na Sallam Sharaff na kuuweka kwenye Mitandao ya Kijamii ya Facebook na Instagram.

Bahati mbaya sana, ushauri huo kwa Diamond pamoja na viongozi wake ulipokelewa kwa mitazamo tofauti, jambo ambalo ni la kawaida kwani watu wote hamuwezi kufanana kifikra.
Lakini nalazimika kuandika taarifa hii na kutoa ufafanuzi baada ya kuona Babu Tale akihusisha Shigongo kuandika maoni yake na masuala ya kibiashara, hususan shoo za muziki.

Nakumbuka ilikuwa Machi 27, mwaka huu, nikiwa ofi sini, nilitoka nje ya lango kuu la ofi si kumtafuta mmoja wa madereva wetu, ndipo nilipoona gari ndogo aina Toyota Vitz (au linalofanana na hilo) limepaki kwenye moja ya maegesho yetu yaliyopo nje ya ofi si yetu, Bamaga-Mwenge, Dar.
Wakati najiuliza ndani ya hilo gari kuna nani, Babu Tale alifungua mlango na kushuka na kunipa ishara kuwa ni yeye yupo pale. Nilimfuata kwenye gari lake na tukasalimiana kwani tunafahamiana. Kwa kuwa sikuwa na ahadi naye na si kawaida yake kuja ofi sini kwetu kama hana suala muhimu, ilibidi nimuulize shida yake.

Akaniambia alikuwa na ahadi na bosi (Shigongo) lakini alikuwa amechelewa, kwani walikubaliana wakutane saa tano asubuhi, lakini kutokana na foleni, yeye alifi ka saa sita mchana. Wakati tunaendelea kuongea, akanigusia madhumuni ya kuonana na Shigongo kuwa, anataka kufanya shoo ya Pasaka kwenye Ukumbi wa Dar Live.

Alisema shoo hiyo ameiandaa kwa jina la Raj Night Party ya msanii Harmonize pamoja na wasanii wengine watakaomsindikiza. Kwa bahati nzuri, wakati tunaongea hilo, akatokea Meneja wa Dar Live, mzee wetu, Juma Mbizo ambaye nikamwambia shida ya Babu Tale na kumtaka wafanye mazungumzo ya awali kisha anitaarifu.

Niliwaacha Babu Tale na mzee Mbizo waendelee na mazungumzo hayo ya awali kisha anipe taarifa na kumjulisha mkurugenzi wetu kuhusu kufi ka kwa Tale.
Wakati huo, mkurugenzi alikuwa na mkutano na wageni wengine na kimsingi yeye hajishughulishi moja kwa moja na shoo za Dar Live, kwani ana miaka mingi hata kufi ka hajafi ka pale ukumbini. Baada ya muda kidogo, mzee Mbizo alikuja kuniomba tumsikilize Babu Tale kwa pamoja kwani wazo lake ni jema, ingawa kama ukumbi, tayari kulikuwa na mpango wa kufanya shoo na wasanii wengine.

Tulikutana na kuweka kikao ofisini kwangu tukiwa watu wanne. Mimi, mzee Mbizo, Babu Tale na Harmonize. Katika mazungumzo yetu, tulizungumza wazo la shoo kwa jumla na sote tukakubaliana kuwa, ni wazo zuri na bila shaka shoo itafanikiwa.
Aidha, tulijadili majukumu ya kila upande ili kufanikisha shoo hiyo ambapo Babu Tale alisema yeye atashughulikia suala la wasanii na matangazo upande wa redio.
Upande wa Dar Live, utashughulika na masuala ya ukumbi, jukwaa na muziki wake, ulinzi, umeme, maji na ‘logistics’ zote za ukumbini pamoja na matangazo kupitia media zetu (magazeti, social media na Global TV).

Baada ya hapo likaja suala la mapato, kutokana na majukumu ya kila mmoja, tulikubaliana tufanye ‘shares’ ambapo katika kikao hicho tulivutana nani achukue zaidi ya mwenzie na mwisho tukakubaliana tupeane muda wa kutafakari na kupiga hesabu sawasawa ili siku inayofuata tujulishane uamuzi wa mwisho.

Siku inayofuata, Dar Live, kupitia idara yake ya mahesabu ilikaa chini na mhasibu mkuu na kupiga hesabu ili kuona iwapo tutagawana mapato kiasi gani kitakuwa sawa, ambacho hakitaitia hasara kampuni na kitaweza kumudu gharama zote, bila kusahau masuala ya kodi ya serikali. Baada ya kufanyika kwa mahesabu na kurejea kumbukumbu za shoo za Pasaka ya mwaka jana na zingine, ilipendekezwa kuwa, mgawanyo usiwe chini ya asilimia 50.
Katika mazungumzo yetu ya awali, Babu Tale alipendekeza alipwe asilimia 70 na Dar Live ichukue asilimia 30. Baada ya kupewa tathimini hiyo na watu wa mahesabu, iliwasilishwa kwa uongozi ambao ulipendekeza tuangalie njia nyingine ya kushirikiana ili shoo hiyo ifanyike Dar Live lakini ikashindikana.

Nilimjulisha Babu Tale uamuzi wa Dar Live kuhusu mgawanyo wa mapato, kuwa tuko tayari kufanya shoo kwa pamoja kwa kugawana sawa (50/50). Babu Tale hakuafi ki mgawanyo huo kwani aliona hauna maslahi kwake kwa sababu asingeweza kupata faida.  Nilimueleza kuwa, hata sisi tumeona chini ya asilimia 50 hatuwezi kupata faida.
Nikamtania pia kwa kumwambia kuwa, tumekutana wote TUNAPENDA PESA. KILICHOANDIKWA NA SHIGONGO HAKIHUSIANI NA KUTOKUBALIANA KWETU Siku aliyofika ofisini, ilikuwa ni Jumatatu ya Machi 27, 2017.
Mazungumzo tuliyafanya mimi, Babu Tale, Harmonize na mzee Mbizo, Shigongo hakuwepo na alishalikabidhi suala hili kwetu (ushahidi wa picha unajionesha).
Siku hiyo tulizungumza na Babu Tale na kuachana kwa makubaliano kuwa tutajulishana siku inayofuata ambayo ilikuwa Jumanne Machi 28. Hadi tarehe 28, Shigongo anaweka maoni yake mtandaoni kwa mara ya kwanza alikuwa hajajua tumezungumza nini na Babu Tale na wala alikuwa hajui kama tumekubaliana au la.

Wazo la kuandika maoni yale kwa Diamond alikuwa nalo hata kabla Babu Tale hajaja ofisini kwetu. Siku anaweka posti yake ya kwanza, Jumanne Machi 28, 2017, mazungumzo yetu na Babu Tale yalikuwa bado yanaendelea na wala hakuweka kwa nia ya kumchafua Babu Tale kutokana na ukweli kwamba, kukubaliana au kutokubaliana kufanya shoo ilikuwa ni jambo jingine. Hata kama tungekubaliana, bila shaka Shigongo angeendelea kuandika alichopanga kuandika kwa wasomaji wake.

Nimelazimika kutoa ufafanuzi huu ili ieleweke kuwa, kutokubaliana kwetu kufanya shoo Dar Live hakuhusiani kwa namna yoyote na maoni aliyoyaandika Shigongo kuhusu Diamond. Kutofautiana kimtazamo juu ya yale yaliyoandikwa Facebook na Instagram kusihusishwe na kutofautiana kwetu kibiashara.

Hata kama tungekubaliana na kufanya shoo hiyo, mwenyewe alishapanga kuyaandika hayo aliyoyaandika kama ushauri kwa akina Tale na Diamond na ni maoni yenye faidia kwa vijana wote wenye mafanikio kama ya Diamond na akina Babu Tale.
ASANTENI KWA KUNISOMA, ABDALLAH MRISHO, MENEJA MKUU GLOBAL PUBLISHERS.

No comments

Powered by Blogger.