ad

ad

WAKALA WA SHETANI - 08


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Wale watu walipita huku wakizungumza kama walikuwa wakimpa taarifa Ngw’ana Bupilipili bila wao kujua. Baada ya kupita alijikuta akipata picha halisi ya kijijini kwao jinsi mali yao watu walivyoigawana.
Moyoni alijisemea kila aliyeila jasho litamtoka kama sumu ya kwenye maji haitawatosha basi atapambana nao kwa mkono wake.
SASA ENDELEA...
Baada ya kupita wanakijiji wale ambao alikuwa akiwajua, aliangalia kama kuna wengine, lakini hakuona mtu ile ilimpa nafasi ya kufanya mambo yake. Alisogea hadi kwenye chanzo cha maji, alivaa gloves na kuifungua dawa yake ya kuulia wadudu na kuweka paketi mbili kisha aliteremka hadi kwenye lambo la kunyweshea mifugo ambako nako aliweka paketi moja kisha alikwenda mpaka kwenye kisima ambacho kilikuwa kikitumiwa na kina mama kuchota maji ya kupikia na kunywa.
Sehemu ile alichelewa kidogo kutokana na kuwa na wanawake wengi waliokuwa wakichota maji. Ilibidi awe mvumilivu kusubiri wamalizike, kina mama walipungua baada ya jua kuwa kali na kwenda kupika kujiandaa kwa ajili ya jioni.
Ngw’ana Bupilipili aliitumia nafasi ile kuweka paketi iliyobakia kwenye kisima kwa kuamini mpaka jioni maji yatakuwa mengi na hivyo dawa itakuwa imejichanganya kwenye maji mengi. Baada ya kuiweka aliikoroga kwa kijiti ili wasiishtukie.
Baada ya kumaliza zoezi lake lililokwenda kama alivyolipanga aliondoka eneo lile na kurudi zake kambini kwa kujificha. Kutokana na kutumia muda mwingi kusubiri kuweka dawa kwenye kisima cha wanawake. Alijikuta akirudi kambini majira ya mchana.
Alijikuta akiingia kambini majira ya saa kumi na moja jioni akiwa amechoka sana na njaa kali ilikuwa imemshika. Alipofika alikwenda kuoga kisha alikwenda jikoni kutafuta chakula kisha alimfuata mwanaye ambaye alikwenda naye chumbani kwake.
Alipofika chumbani alimlaza mtoto kitandani na yeye kupiga magoti kuomba msamaha kwa Mungu kwa kile alichokifanya. Huku moyo ukimuuma kwa jinsi watu walivyokosa huruma na imani kwa kuigawa mali yao bila kuitolea jasho.
Alimuomba Mungu amhukumu kila mmoja aliyehusika na kifo cha mumewe mtoto wao na wote waliochukua mali zao za jasho lao kwa nguvu.
Kwa vile alikuwa amechoka alioga na kupanda kitandani kulala kusubiri matokeo ya mpango wake hatari wa kulipa kisasi cha mumewe mwanaye wa kwanza na mali zao.
Baada ya maombi yale alimpa ziwa mtoto wake na yeye kujilaza usingizi mzito kutokana na uchovu wa safari.
********
Katika kijiji cha Nyasha ilikuwa siku ambayo iliwachanganya watu wengi baada ya kila nyumba kulalamikia tatizo la tumbo. Hospitali zilijaa wagonjwa ambapo wengi walipoteza maisha. Ilibidi taarifa zifike haraka mkoani na kutumwa timu ya wataalamu kuja kufanya uchunguzi.
Ilionesha watu wa kijiji kile wamekunywa sumu iliyokuwa kwenye maji, mifugo yote ilikufa na kufanya kijiji kiwe katika janga zito la maafa ya watu na mifugo. Ilibidi wagonjwa wote wahamishiwe mjini lakini wengi walifia njia.
Katika kila kaya zipo zilipoteza familia nzima na nyingine ilipoteza zaidi ya watu watatu.
Mara moja watu wa kijiji cha Nyasha walipigwa marufuku kunywa maji yote na kufanywa uchunguzi mzito na kubainika kuwa vyanzo vyote vya maji vilikuwa na sumu.
Ilibidi iletwe dawa na kuondoa sumu katika sehemu zote zenye vyanzo vya maji lakini wakati huo kijiji cha Nyasha nilikuwa na msiba mzito wa kupoteza nusu ya wanakijiji.
Taarifa za msiba mzito uliowakuta wanakijiji wa Nyasha zilimfikia Ngw’ana Bupilipili ambaye alijawa na furaha kuamini mpango wake umefanikiwa. Pamoja na kufanikiwa kuua watu wengi bado dhamira yake ilikuwa haijatimia. Alipanga kijiji kile kukifanya kiwe cha historia kwa kuwamaliza wanakijiji wote na kubakiza magofu.
******
Baada ya kufanikiwa na zoezi la awali la kukiteketeza kijiji cha Nyasa, Ngw’ana Bupilipili aliendelea na mchezo wake ule kila hali ilipotulia alikwenda kuweka sumu kwenye maji. Hali ile ilikiweka kijiji cha Nyasa kwenye mashaka na kuamua kufanya uchunguzi wa kina juu ya nani anayefanya mchezo ule.
Makachero toka serikalini walianza uchunguzi wa siri bila mtu yeyote kujua. Walilinda kwa masaa 24 vyanzo vyote vya maji kwa kubadilishana kufuatilia mtu aliyekuwa akisababisha mauaji ya wanakijiji cha Nyasha.
Ngw’ana Bupilipili kama kawaida yake baada ya mambo kutulia alirudi tena kwenye kijiji cha Nyasa kuendeleza hukumu yake ya kuhakikisha anakisafisha kijiji chote.
Kurudi kijiji pale ilikuwa mara ya nne, kama kawaida alimuaga shoga yake na kumuachia mwanaye Kusekwa aliyekuwa ametimiza miaka miwili.
Alitembea katika mbuga kama ilivyo kawaida yake, kwa vile alikuwa ameisha kuwa mzoefu. Hakuwa na hofu tena ya kitembea mbugani peke yake. Kutokana na uzoefu alikuwa akitoka usiku zaidi ili alfajiri imkute ameisha maliza kazi yake.
Baada ya mwendo wa masaa matatu bila kupuumzika alijikuta akiingia kijiji cha Nyasa pakiwa bado kiza hakukuwa na mtu yoyote. Alijisifu kuondoka mapema kwa kuamini atamaliza kazi zake bila mtu yeyote kumuona.
Baada ya kuangalia usalama wa eneo lile na kuona hakuna tatizo. Aliifungua ile dawa na kuitia kwenye chanzo cha maji kisha aliifunga kuelekea kwenye kisima cha kina mama. Wakati akifanya vile walinzi wa eneo lile walikuwa bado hawajamuona.
Wakati anataka kuondoka eneo lile askari mmoja alishangaa kumuona mwanamke akitokea kwenye chanzo cha maji.
“Hey, wee mama unafanya nini alfajiri hii?”
“Nakwenda shamba,” Ngw’ana Bupilipili japo alikuwa katika mshtuko mkubwa lakini alijitahidi kujibu kwa kujiamini.
“Shamba, mbona majibu yako yana utata, unakwenda shamba gani ikiwa mashamba hayapo eneo hili?”
“Achana naye bwana, si unajua tumemaliza lindo salama,” alisema mlinzi mwingine.
“Haya potea hapa.”
Ngw’na Bupilipili alimshukuru Mungu kumpitisha na watu wale, ndipo alipofumbuka macho kuwa sehemu ile ina ulinzi. Aliteremka kuelekea bondeni kwa kuhofia kugeuza lazima wangemtilia wasiwasi.
Aliamua kutafuta njia nyingine ya kumuokoa kwa kuondoka eneo lile ambalo aliamini limezungukwa na ulinzi mzito. Alitembea kwa taadhari akipita pembeni pembeni kutafuta njia ya kutokea nje ya kijiji cha Nyasha.
Askari mmoja alimuona Ngw’ana Bupilipili akitembea kwa mashaka na kuamua kumfuatilia taratibu. Baada ya mwendo mfupi alikutana na sehemu kubwa iliyokuwa imetengeneza kama bwawa.
Alipoiangalia sehemu ile ilimuonesha kabisa watu huchota maji. Akili yake ilimtuma sehemu ile vilevile inatakiwa kuwekwa sumu. Kwa taadhari kubwa alitoa paketi ya dawa ya kuulia wadudu na kuanza kuinyunyizia kwenye maji yale.
Askari aliyekuwa akimfuatilia alimshangaa na kujiuliza yule mwanamke ananyuziza nini kwenye yale maji.
Hakutaka kumshtua alimsogelea taratibu mpaka alipokuwa na kusimama nyuma yake bila Ngw’ana Bupilipili kumuona. Baada ya kuimiminia ile dawa iliyobaki aliirudisha kwenye paketi yake kisha aliifunga kwenye kalatasi ya lailoni na kuiweka katika mfuko wa kaputula aliyokuwa amevaa.
Wakati anavua gloves ndipo yule asakari alipomshtua.
“Unafanya nini?”
Ngw’ana Bupilipili alishtuka na kuanza kutimua mbio, lakini hakufika mbali alikamatwa. Askari baada ya kumpekuwa alimkuta na paketi mbili na nusu za dawa ya kuulia wadudu. Alimuuliza zile dawa zina kazi gani Ngw’ana Bupilipili hakuwa na jibu lolote zaidi ya kusema kwa hasira.
“Niueni kama mlivyo muua mume wangu.”
“Tukuue kwa sababu gani, huyo mumeo tunamjua?”
“Usimjue kwa nini wakati mmemuua na mali zetu mmegawana baada ya kumuua mwanangu wa kwanza pia mimi kunikosa kuniua na mwanangu.”
“Lakini unajua unazungumza na nani?” askari alimuuliza baada ya kuona hamuelewi anayoelezwa.
“Na wauaji.”
“Basi mama kwa taarifa yako sisi si watu unaowasema, ni wana usalama toka serikalini tuliokuja kufuatilia nani mhusika mkuu wa mauaji ya wana kijiji cha Nyasha.”
“Mmh! Leo ndiyo mmeona uchungu, mlikuwa wapi mpaka siku zote wakati watoto maalbino wasio na hatia wameuawa kwa kisingizio cha ushirikina, mume wangu ameuawa na hao wana kijiji mbona hakuna aliyekuja kumtetea.
“Mtoto wangu umekoswa kuuawa na wanakijiji mbona hamkuja kumsaidia leo hii wanakufa wao ndio mnajitia kiherehere.”
“Ina maana wewe ni mwenyeji wa kijiji hiki?”
”Nilikuwa.”
“Sasa upo wapi?”
“Haiwahusu, naishi kama mnyama porini kuokoa maisha yangu.”
“Hii dawa ulikuwa unaiweka kwenye maji ili?”
“Niwamalize na bahati yao umenikamata, ningebakiza historia katika kijiji hiki na mkinifunga mnifunge maisha au mninyonge lakini kama nitatoka hata niwe natambaa nitahakikisha naendeleza kisasi,” Ngw’ana Bupilipili alisema kwa hasira.
“Kisasi cha nini?”
”Siongei na jiwe, nimewaeleza nimepoteza mwanangu nimepoteza mume wangu nimepoteza mali zangu mashamba ng’ombe nyumba vyote vimechukuliwa na wana kijiji mlikuwa wapi?”
“Kwa sababu gani?”
“Kuzaa mtoto albino.”
“Sasa kuzaa mtoto albino inaingiliana vipi na mauaji ya mumeo na mwanao?”
“Wanasema ni mkosi hivyo kila mtoto aliyezaliwa albino aliuawa.”
“Kwa nini taarifa hizi hamkuzileta mapema?”
“Hizi za mauaji nani kawaletea?”
“Wakuu wenu.”
“Sasa ndiyo ujiulize kwa nini mauaji ya watoto albino hamkuletwa, mletewe kwenye mauaji haya?”
“Huoni kama kosa lako linaweza kusababisha kunyongwa?”
“Nilijiandaa mapema toka nilipopata dhamira ya kulipa kisasi, nilikuwa tayari kwa lolote, kifo kitu gani nimempoteza mwanangu na mume wangu nitakuwa mimi,” Ngw’ana Bupilipili alisema kwa hasira huku akilia.
ITAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.