ad

ad

WAKALA WA SHETANI - 07


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Okay, nafikiri ukipata chakula utapona kabisa.”
“Nitashukuru, mwanangu yupo wapi?”
“Yupo, utaweza kumnyonyesha?” walimuuliza.
“Ndiyo.”
“Okay, kamleteni mwanaye.”
Baada ya kusema vile msaidizi alitoka kumufuata mtoto na kubakia daktari mzungu ambaye aliendeleza kumdodosa mgonjwa.
“Eti mama umetokea sehemu gani?”
“Kabla sijakujibu naomba unieleze hapa ni wapi na nimefikaje?”
SASA ENDELEA...

“Ooh vizuri mama, hapa ni kituo cha watumishi wa kiroho, tupo kwa ajili ya kutoa misaada kwa watu wa maeneo ya karibu kielimu na kiafya. Taarifa zako tumezipata kutoka kwa wasamalia wema waliokuwa wakipita porini na kukuta ukiwa umepoteza fahamu, ilibidi tuwatume vijana wetu ambao walikuchukua na kukuleta hapa.
“Baada ya kukufanyia uchunguzi haukuwa na tatizo kubwa zaidi ya njaa na uchovu wa kuonekana umetembea kwa muda mrefu bila kupumzika na pia ulikuwa hajapata chakula cha kutosha kitu kilichofanya mwili upoteze nguvu na kukufanya upoteze fahamu.
“Nina imani imenielewa vizuri una swali lingine?” daktari alimuuliza kwa sauti ya faraja.
“Ooh, asanteni sana Mungu aendelee kuwabariki.”
“Amen, m’hu, nawe nini kimekusibu mpaka kuwa katika hali hii?”
Ngw’ana Bupilipili kabla ya kujibu alivuta kumbukumbu jinsi alivyonyanyasika kwa ajili ya kujifungua mtoto albino na kifo cha mumewe huku akishangaa jinsi mwanaye alivyopewa huduma nzuri bila kubaguliwa kwa jinsia au rangi yake.
Bila kutegemea machozi yalianza kumtoka mdomo ulikuwa mzito kutoa matamshi. Daktari alishtushwa na hali ile na kumfanya aamini lazima yule mama atakuwa na tatizo zito. Kabla hajanyanyua mdomo wake kutamka kitu. Mara mlango ulifunguliwa aliingia yule msaidizi akiwa amempakatia mtoto.
Ngw’ana Bupilipili alitaka kunyanyuka kitandani baada ya kumuona mwanaye akiwa hai. Baada ya kupewa mwanaye alijikuta akimtazama mara mbili mbili huku akimgeuza kwa kumuangalia kama yupo sawa.
Baada ya kupata uhakika yupo sawa alimnyonyesha, mtoto kulidaka ziwa la mama yake na kunyonya kwa fujo kutokana na njaa kali.
Daktari na msaidizi wake alijikuta wakitabasamu kwa pamoja huku wakifurahia mtoto alivyofurahia ziwa la mama yake. Daktari hakutaka kumsumbua sana alimwacha amnyonyeshe mtoto na kumuachia maagizo msaidizi wake.
“Pamera, baada ya kumaliza kunyonyesha mgonjwa apewe chakula apate maji ya kuoga kisha apumzike, jioni nitakuwa na mazungumzo naye anaonekana ana kitu kizito moyoni mwake.”
“Sawa dokta.”
Daktari alitoka na kumuacha msaidizi wake ameketi kwenye kiti kusubiri amalize kunyonyesha mtoto na kumpa huduma alizopangiwa.
*****
Ngw’ana Bupilipili aliishi pale kwenye kituo cha kiroho na mtoto wake ambaye alikutana na watoto wengine wenye ulemavu wa ngozi. Hali ile ilimpa faraja kubwa na kuamini kijijini kwao imani za ushirikina ndizo zilizotawala na kuwafanya kila kukicha wamkosee Muumba.
Pamoja na kukaa pale kwa amani moyo wake ulikuwa ukiumia kila ulivyofikilia kifo cha mumewe na mali walizoziacha kijijini. Alijikuta akiapa lazima alipe kisasi cha kifo cha mumewe na mtoto wao wa kwanza albino aliyeuawa kwa imani za kishirikina.
Kila kukicha alikuwa akibuni njia ya kulipa kisasi kwa wanakijiji waliosababisha yote yale. Siku moja akiwa katika kufanya usafi kwenye stoo aliona paketi dogo iliyokuwa imeanguka chini na kumwaga unga mweupe chini.
Aliiokota na kutafuta sehemu ya kukiweka, wakati huo Sister Lucy alikuwa akiingia stoo na kushtuka kumuona Ngw’ana Bupilipili amekishika paketi ile tena bila gloves mkononi.
Alionekana kushtuka sana kumkuta amekishika paketi kile.
“Mama Kusekwa kwa nini unashika dawa hiyo bila gloves?”
“Nimeikuta hapa chini ndio nilikuwa natafuta sehemu ya kuiweka.”
“Hii sumu, ukiiweka mdomoni umekufa dada yangu.”
“Sumu!?”
“Eeh.”
“Mungu wangu, Kama sumu inafanya nini humu ndani?”
“Si sumu kwa maana imetengenezwa kuua watu, ni dawa ya kuuwa wadudu katika mitalo mashimo ya maji hata wadudu warukao na watambaao.”
“Sasa inakuwaje unasema sumu kumbe dawa ya kuulia wadudu?”
“Mama Kusekwa, hii ni dawa lakini ukiitia mdomoni inageuka sumu na kukudhuru.”
“Mmh, sawa.”
“Tena dawa hii kama utakumbuka mwaka mmoja kuna mtu aliweka kwenye tenki la maji na kuiua familia nzima.”
“Mmh! Sasa inakuwaje mtu aweke kwenye tanki la maji wafe watu wengi, kwani ina nguvu gani isiyopungua katika maji mengi?”
“Hii ni sumu kali sana ndio maana nikashangaa kukuona umeishika kwa mkono. Unatakiwa kunawa vizuri na sabuni mikono yote na kuhakikisha unakuwa msafi kabla ya kumshika mtoto wako.”
“Nashukuru Sister Lucy, hapa sina moja. Basi ningetoka hapa ningepewa embe mimi ningekula tu bila kujua kama nina sumu mkononi.”
“Basi kuanzia leo unatakiwa kuvaa gloves kabla ya kupanga vitu vya humu ndani.”
“Nitafanya hivyo, hivi kama ukiitia dawa hii kwenye lambo la kijijini si unaweza kuua watu wengi?”
“Tena usiombe kufanya kitu kama hicho, na dawa hizi hupatikana sehemu kama hizi madukani hazipo ni kali sana inaua mara moja.”
Baada ya maelezo yale Ngw’ana Bupilipili alikwenda kunawa kwa sabuni na kisha aliendelea na kazi yake.
******
Jioni ya siku ile akiwa amejilaza kitandani kwake, wakati huo mwanaye akiwa anaendelea kufaidi ziwa tamu la mama yake. Alijikuta akikumbuka maneno aliyokuwa akizungumza na Sister Lucy kuhusu ukali wa ile dawa ya kuulia wadudu kuwa ni sumu kali kama mwanadamu atainywa.
Aliamini kupitia sumu ile itakuwa njia nyepesi ya kulipa kisasi, alijua akienda kuiweka katika chanzo cha maji ambayo hutumiwa na wana kijiji lazima ataua watu wengi.
Alijikuta akiwachukia watu wote wa kijiji cha Nyasha kwa kuamini kila aliyetoka katika dawa ya wauaji nao walitakiwa kuipata hukumu ile kwa kuamini kama wao walifurahia vifo vya watoto wenye ulemavu wa ngozi basi nao watoto hao nao watafurahi kusikia mauti yao.
Alijikuta akiapa lazima alipe kisasi tena kikubwa na kuacha historia ya vifo vya watu wengi. Alipanga siku ya pili ikiingia kufanya usafi achukue paketi nne ya sumu ambazo zote ataviweka katika vyanzo vya maji ya kijiji cha Nyasha.
******
Siku ya pili akiwa anafanya usafi stoo alichukua paketi nne za dawa ya kuulia wadudu na kuificha kwenye kanga. Baada ya usafi alitoka nayo na kwenda kuificha chumbani kwake.
Baada ya kuipata ile dawa alipanga siku moja ataondoka kwenye kambi ile saa kumi za usiku kwenda kijiji cha Nyasha.
Baada ya kujipanga na kuipanga siku ya kwenda kulipa kisasi. Alimtaarufu shoga yake wa karibu kuhusu safari yake, Lakini alimdanganya kuwa anafuata vitu vyake.
Baada ya kukubaliana siku ya pili majira ya saa kumi za usiku Ngw’ana Bupilipili aliamka na kwenda kumwamsha shoga yake ambaye alikuwa amelala.
“Vipi, safari imeiva?”
“Eeh, shoga, niangalizie mwanangu,” alimpa mtoto wake aliyekuwa bado na usingizi.
Shoga yake alimchukua na kumwingiza chumbani kwake na kumlaza kitandani kisha alitoka ili amuage.
“Basi shoga safari njema.”
“Nashukuru shoga, Mungu akijalia tutaonana.”
Ngw’ana Bupilipili kabla ya kuondoka aliingia chumbani kwa shoga yake na kumnyanyua mtoto wake kitandani na kumkumbatia kwa uchungu huku machozi yakimtoka. Hali ile ilimshtua shoga yake na kuhoji kulikoni.
“Vipi mbona unalia?”
“Basi acha tu, nimekumbuka vitu vingi hasa baada ya kukumbuka kifo cha mume wangu na leo narudi huko huko.”
“Kama ni hivyo kwa nini unakwenda tena?”
“Hapana kuna vitu vyangu vingi na vya muhimu sana lazima niende.”
“Sasa utaingiaje pale kijijini?”
“Hapana siendi nyumbani nitaishia shambani kwetu.”
“Unajuaje kama shamba bado lipo mikononi kwenu?”
“Yote nitayajua hukohuko.”
“Basi bwana akutangulie safari yako yote.”
“Amen.”
Alimrudisha mtoto kitandani baada ya kumbusu, alimgeukia shoga yake na kumkumbatia kabla ya kugeuka na kuondoka kuwahi safari yake ambayo aliamini mpaka saa mbili asubuhi atakuwa kijiji cha Nyasha.
Hakutokea mlango wa mbele aliruka ukuta kuogopa kuulizwa na mlinzi anakwenda wapi. Baada ya kufanikiwa kutoka salama nje ya kambi alianza safari kuelekea kijiji cha Nyasha moyoni akiwa na dhamira nzito ya kuwa tayari kupambana na lolote litakalo tokea mbele yake.
Aliamini hata kama atafariki mwanaye bado ataishi katika malezi mazuri japo hakuomba iwe hivyo. Ngw’ana Bupilipili aliiacha kambi na kuingia porini kuitafuta njia ya kuelekea kijiji cha Nyasha. Bado hali ilikuwa ya giza huku milio ya wanyama wakali ikiendelea kutawala pori lote.
Alitembea huku akimuomba Mungu avuke salama. Alikwenda kwa mwendo wa kasi huku akikwepana na wanyama wakali mpaka majira ya saa moja na nusu alikuwa amefika kwenye chanzo cha maji ya kijiji cha Nyasha.
Aliangalia hali ya usalama kwa mbali aliwaona watu wakielekea upande ule alipokuwa. Alijificha, watu walipita huku wakizungumza na moja ya mazungumzo yalikuwa kuigawa mali ya Mathayo mume wake ng’ombe mashamba na nyumba. Alimsikia mmoja akisema:
”Haiwezekani baba Sabina na mkewe wachukue sehemu kubwa kwa kisingizio eti walikuwa wanamdai Mathayo.”
“Ile mali ilitakiwa ikabidhiwe kwa kijiji hata ng’ombe na mashamba yale ya kijiji kuliko mtu mmoja kuchukua sehemu kubwa.”
“Hivi mfano jamaa atokee kutakuwa na usalama kweli?”
“Hapo sasa.”
“Na lile eneo la nyumba ya Mathayo mbona baba Sabina analing’ang’ania kwa kusema ni yeye aliyempa.”
“Yule jamaa muongo sana, Mathayo mimi namjua vizuri, lile eneo aliwahi kujenga kipindi kirefu hata kabla hajaoa leo hii anasema eti yeye ndiye aliyemkaribisha.”
“Ndiyo hivyo wenye nguvu ukisema unatafuta utengwe na kijiji.”
Wale watu walipita huku wakizungumza kama walikuwa wakimpa taarifa Ngw’ana Bupilipili bila wao kujua. Baada ya kupita alijikuta akipata picha halisi ya kijijini kwao jinsi mali yao watu walivyoigawana.
Moyoni alijisemea kila aliyeila jasho litamtoka kama sumu ya kwenye maji haitawatosha basi atapambana nao kwa mkono wake.

ITAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.