ad

ad

HADITHI: Msafara wa Mamba - 04

 
 
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’

ILIPOISHIA:
Mama alitulia kama anawaza kitu kisha aliendelea kunipa simulizi ambazo kwa upande wangu zilikuwa sawa na kuupasua moyo wangu bila ganzi. Sijui maumivu yake yako vipi ukiyapimia, nilishindwa kulia kutokana na kumuonea huruma mama yangu kwa simulizi yake ambayo hakupenda niijue.
SASA ENDELEA…
Mashavu ya mama yalibeba michirizi ya machozi na macho yake yalikuwa yamevimba na kuwa mekundu kwa kulia kilio cha kwikwi kilichoambatana na simulizi.
"Mwanangu sikupenda hata siku moja uijue historia hii najua lazima itaujeruhi moyo wako na kukufanya upoteze mwelekeo wa maisha yako. Sitajisikia furaha pale nitakaposikia amevunjika moyo wako aliouonyesha katika masomo...
Mwanangu Herena japo sipendi kuongea habari hizi mbele yako, mama yako nilibweteka na uzuri wangu na kujiona nina rasilimali ya kuweza kunisaidia katika maisha yangu. Mwanangu uzuri umeniponza mama yako."
Kufikia hapo mama alianza kulia na kushindwa kuelewa uzuri umemponza kivipi. Nilitulia tuli huku roho ikiniuma na machozi yalishindwa kujizuia yalitoka bila kupenda, nilimuonea huruma mama yangu. Baada ya kufuta machozi na kamasi nyembamba aliendelea kunisimulia.
"Mwanangu uzuri nilionao mama yako nilifuatwa na wanaume kama malkia wa nyuki. Mama yako nilishindwa kuchagua nimkubali yupi kila mmoja alimzidi mwenzie dau. Kwa kweli kila aliyekuja nilimpokea niliweka masirahi mbele.
“Muda mfupi mama yako niliweza kuishi maisha nusu ya peponi, huku nikikutunza kama mboni ya jicho langu. Ajabu nyingine mwanangu nilijikuta nimekumbwa na ugonjwa wa ngono wa kutoridhika na mwanaume mmoja.
“Mwanangu unashangaa kuachana na Anko wako wa benki, mbona hata mshipa wa fahamu haunigongi. Nimeachana waziri mkubwa serikalini nini nilichokikosa na ndiye aliyenijengea nyumba hii na kuninunulia vitu vyote na benki aliniwekea pesa lukuki.
"Tena.." mama alisita kidogo kuendelea kuzungumza na kujifikiria jambo na kuamua kuendelea kunisimulia
"Mwanangu japo maneno mengine hupaswi kuyasikia lakini hakuna jinsi kwa vile sipendi kosa nililolifanya unalirudia. Yaani mwanangu vitu vingine mbona aibu yaani sijui nimerogwa ugonjwa gani wa kupenda ngono kupindukia...
Anko wako wa Serikalini alinifumania na muuza mchicha.. mmh we acha yaani muuza mchicha mwenyewe pesa nilikuwa nampa mimi," Mmmh yaani sijui niseme nini nilimuangalia mama yangu na maneno yake kwa kumshusha na kumpandisha bila kupata jibu. Nilijua hakuna ugonjwa bali ni kujiendekeza na matokeo yake kuwa wazoea.
"Basi mwanangu kama nilivyo kwambia mama yako nilikuwa kama malkia wa nyuki nilipo achana na Muheshimiwa yule nilipata muarabu mmoja ambaye sikukaa naye sana kutokana na tabia zake chafu ambazo hizo hupaswi kuzijua ila elewa tulishindwana tabia.
“ Kwa kweli sikuyumba hata siku moja na maisha yaliendelea kuwa mazuri. Nina imani hata siku moja hukuteteleka katika maisha yako, hata uliponiuliza kuhusu baba yako na kukukanya uliziba mdomo wako.
“ Lakini ajabu tabia yako iliyobadilika ghafla tena yenye msimamo ilinichanganya sana. Pamoja na kukutisha hukuonekana kutetereka na msimamo wako ulikuwa pale pale kuhusu kuwafukuza wanaume zangu. Niliweza kusalimu amri na nyumba yangu kwa kweli imerudisha heshima.
“Niliamua kufanya mambo yangu nje ya hapa, lakini kwa bahati mbaya nimeandamwa na maradhi. Kwa kweli nilishindwa kutulia nyumbani kutokana mradi wangu wa mwili nisingeweza kutulia nyumbani. Kutokana na sehemu kubwa ya mahitaji yangu kupatikana kwa njia ya kuutoa mwili wangu.
“ Sina budi kukushukuru kwa kuweza kunizuia kutoka nje ili kuokoa hali yangu. Kwa kweli nilikuwa siamini hata siku moja kama akili za mtoto zinaweza kumsaidia mtu mzima. Kweli usidharau usicho kijua, ila leo umekuja na mapya ya kutaka kujua kumjua baba yako sina budi kukueleza ukweli.
“Naomba unisamehe mwanangu, hiyo ndiyo kweli ila nakuomba mwanangu habari hizi zisikukatishe tamaa".
Mama alinipigia magoti, kwa kweli roho iliniuma na kumuonea huruma mama yangu. Nilimshika mabegani na kumnyanyua, tulikumbatiana kila mmoja alilia na kumlowesha mwenzake machozi.
Mama alikuwa wa kwanza kunyamaza na kuninyamazisha mimi, nilinyamaza na kumuomba mama japo maji yameisha mwagika abadilike tabia. Mama alikubali kubadilika ili kuilinda afya yake na kumuomba aende kwa Anko wa benki kumuomba msamaha.
Lakini mama alikataa alisema katu hawezi kurudiana na mtu aliyeachana naye. Sikuwa na uwezo wa kumlazimisha, nilimuomba mama tuanzishe mradi ili tuepukane na maisha tegemezi hata kama mjomba atakapositisha huduma zake.
Tuliyaanza maisha mapya ambayo japo hatukuwa juu kiuwezo, lakini mama alibadilika kwa kiasi kikubwa. Kwa kweli hata mimi moyo ulitulia japo sikumjua baba yangu na jinsi mimba yangu ilivyopatikana, sikutaka habari zile zinikatishe tamaa. Niliamua kusoma kwa bidii ili kujikwamua na hali iliyokuwa ikija mbele yetu.
Anko wa benki aliendelea kunihudumia kama mtoto wake, na hali ya mama iliendelea kuimalika siku hadi siku. Ajabu mama alinenepa na kunawili, wakati huo mama alikuwa amefungua palepale nyumbani duka la kuuza vocha na kupigisha simu pamoja na kuuza mawigi na vitu vya kike.
Kidogo ilisaidia kupata pesa ndogo ndogo za matumizi, pesa zote nilizoingiziwa na Anko wa benki niliongezea kwenye duka na kuongezea vipodozi. Lilionekana duka lililoshiba na kuweza kutupatia kipato chenye kutuwezesha kuweka angalau pesa kidogo kwa wiki. Kweli mzowea punda farasi hamuwezi, mama baada ya kupendeza akaanza kubadilika na kurudia tabia yake ya awali ya ukahaba. Kila nilivyo mkanya alikuja juu na kusema yeye anajua zaidi yangu kwa vile ameona jua kabla yangu.
Mama alibadilika kwa kiasi kikubwa na kurudi nyumbani amelewa, tabia zile zilinichanganya kwa kiasi kikubwa na kusababisha hata kuyumba kimasomo. Mama hakutaka kabisa kunisikiliza na mara nyingi alikuwa mkali kwa kutotaka kunisikiliza.
Siku moja nilikwenda ofisini kwa Anko wa benki, kwa kweli hakunipokea kama ilivyo kawaida. Nilishangaa na kumuuliza kulikoni, aliyonieleza yaliniacha mdomo wazi kwa kusema:
Kuwa amekutana na mama yangu kwenye pati akiwa na mkewe yaani mke wa Anko. Mama alikuwa na mwanaume wake, alipomuona alianza kumtukana na kusema pesa zake ndizo zinazo nitia mimi kiburi cha kukosa heshima. Kwa hiyo alimuomba aache mara moja kumihudumia.
Mjomba alisema alipata aibu mbele ya mkewe na kusababisha ugomvi mkubwa na mkewe. Kwa hiyo ameamua kusitisha huduma kwangu mara moja.
Kauli ile ililivuruga tumbo langu na kunifanya nisikie tumbo la kuhara. Nilimbembeleza mjomba, lakini hakuwa tayari kunisaidia na kuniuliza swali:
"Herena."
"Abee Anko," niliitikia huku nikilia.
"Mimi mzazi wako?"
"Hapana."
"Nina imani una baba yako, lakini nimeamua kubeba jukumu la kukulea kutokana na tabia zako na juhudi zako kimasomo. Na nilikuwa sikujui bila mama yako na mama yako ndiye aliyenipiga marufuku sasa mimi nifanyeje?"
"Hapana Anko naomba unisaidie nitakimbilia wapi?" nilipiga magoti mbele yake.
"Herena itakuwa vigumu kama aliweza kunieleza vile mbele ya mke wangu nikirudia si atanifuata nyumbani au hata kusema nimekubaka na kunishushia heshima yangu..Mfuate baba yako."
"Anko, sina baba."
"Mimba mama yako amejibebesha?"
"Nilipatikana kwa njia ya kukutana na wanaume tofauti na kushindwa kumjua baba yangu," ilibidi nijivue nguo mbele ya Anko labda ningepata msamaha, lakini haikusaidia kitu.
"Ooh, pole sana ndio hivyo sina jinsi siyo mimi ni mama yako nina imani huenda amekuandalia maisha mazuri ndio maana amekuambia amewahi kuona jua hivyo muachie. Hata ulipofikia hujui pesa alipata vipi, tena sasa hivi analipa. Amerudi kwenye hali yake ya zamani. Utapata baba mpya au yatari ameisha mpata."
Maneno ya Anko niliona sasa yanaelekea kunisimanga, sikutaka kuongeza neno niligeuka na kuondoka. Sikuwa na haja ya kulia japo moyo uliniuma, nilijikaza mtoto wa kike na kurudi hadi nyumbani.
Nilipoingia ndani nilimkuta mama na mwanaume wa kizungu walikuwa wakinywa pombe kali, aliponiona alinyanyuka ili anikumbatie.
"Wawooo..my Babiiii."
Aliponisogelea ili anikumbatie nilimsukuma na kuanguka chini, sikutaka kumuangalia nilikimbilia chumbani kwangu huku nikilia.

Nini kitaendelea? Endelea kufuatilia.


Powered by Blogger.