ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 22

 
ILIPOISHIA...
“Zoezi linafanyika lini?”
“Hakuna kusubiri, ni kesho tu baba mdogo.”
“Sawa.”
SASA ENDELEA...
CHRIS hakutaka kupoteza muda, kilichokuwa akilini mwake ni mke tu. Hakutaka mwanamke mwingine zaidi ya Laura. Baba yake mdogo, Shamakala alikubaliana na wazo lake.
Hakuwa na sababu ya kupoteza muda. Alimfuata mama yake, alipokuwa amekaa kisha akaketi kwenye kigoda jirani yake.
“Mkombi...” (Mama) Shamakala aliita kwa Kinyiramba.
“Shamakala unasemaje?”
“Kuna jambo zuri nataka kukuambia.”
“Zuri? Hebu nikae vizuri sasa. Haya niambie ni nini?”
“Ni kuhusu Chris... anataka kuoa.”
“Jambo zuri sana hilo. Ameshapata huyo mwali mwenyewe sasa?”
“Ndiyo, tena ni mtu wa hukuhuku kwetu.”
“Wa wapi?”
“Anatokea Kijiji cha Mpambala.”
“Safi sana, sasa mmefikia wapi?”
“Anataka kesho amlete hapa nyumbani aje kututembelea, kama tena taratibu zetu, tukikaa naye hapa japo kwa siku mbili tutaweza kumchunguza japo kidogo unavyojua na sisi ili tujiridhishe kuwa anafaa kuingia kwenye familia yetu.”
“Ni wazo zuri, utaongozana naye sasa au?”
“Ndiyo... mimi ndiyo mwenyeji wake pale, lazima niende naye.”
“Mimi naunga mkono mwanangu, sina matatizo na hilo.”
“Sawa mama, nilisema nikujulishe tu maana ungeshangaa kuona mtu amekuja nyumbani bila taarifa yako, tukaona si busara.”
“Mmefanya vizuri.”
Shamakala alifurahishwa sana na majibu ya mama yake. Alimfuata Chris na kumweleza kila kitu kilivyokuwa, akafurahi sana.
Usiku ulikuwa mrefu sana, alitamani  asubuhi ifike haraka ili Laura afike nyumbani kwao. Alitaka kuona namna ambavyo bibi yake angemchukulia.
***
Chris alikuwa wa kwanza kuamka asubuhi hiyo. Alidamka saa moja kasoro, muda ambao kwa kipindi hicho ambacho hakikuwa cha kilimo, ilikuwa mapema sana.
Kwa kawaida wakati wa kilimo wanakijiji hadaamka mapema na kwenda mashambani. Si katika kipindi hicho cha kiangazi. Alifanya shughuli ndogondogo za nyumbani hadi saa mbili ndipo baba yake mdogo alipoamka.
Chris alifurahi sana alipomuona baba yake mdogo akitoka nje. Baada ya salamu, wakaanza kupanga namna ya kufanya.
“Hapa hakuna cha kujadili sana, twende tu juu kule juu tukachukue pikipiki tuondoke,” akasema Chris.
“Sawa... lakini tupate kifungua kinywa kwanza.”
“Hapana, tutakunywa supu Ibaga.”
“Sawa.”
Hawakuwa na muda wa kupoteza, walikwenda barabarani walipochukua pikipiki moja ambayo walipanda kwa mtindo wa mshikaki, safari ya kwenda Ibaga ikaanza.
Kwa pikipiki ulikuwa ni mwendo wa dakika kumi tu, walikuwa wameshafika Ibaga. Chris ndiye aliyemlipa dereva, kisha wakatembea na kuelekea kwenye mgahawa mmoja maarufu eneo hilo.
“Sasa dingi, we’ nisubiri hapa, ngoja nikamchukue.”
“hivi ni wapi kwani?”
“Tumefikia Sayuni Lodge.”
“Sawa.”
Shamakala na Chris walikuwa na umri unaokaribiana sana, Shamakala alikuwa mtoto wa mwisho katika uzao wa baba yake na Chris. Sababu hiyo iliwafanya wazoeane kwa kiasi kikubwa.
Hata mazungumzo yao yalikuwa ya ujana zaidi kutokana na umri wao kukaribiana. Hata hivyo, hilo halikuvunja heshima waliyokuwa nayo. Bado Chris aliendelea kumheshimu Shamakala kama baba yake.
Chris alifika Sayuni na kwenda kugonga katika chumba alichomuacha Laura jana yake. Aligonga mara moja tu, Laura alifungua. Chris alishangaa sana.
Alikutana na Laura mpya kabisa. Laura alikuwa amevaa mavazi ambayo kwa kumwangalia tu unajua kuwa, alikuwa msichana aliyeishi kijijini. Alifafana nao kwa kila kitu.
“Daah! Kweli umefunika mpenzi wangu. Hapo umepatia kabisa.”
“Nashukuru mpenzi, nini kinaendelea?”
“Kama uko tayari, tuondoke. Hakuna kitu cha kusubiri zaidi.”
Ndivyo ilivyokuwa, walitoka na kwenda mgahawani alipokuwa Shamakala. Utambulisho mfupi ukafanyika kisha wote wakaagiza supu ya mbuzi. Walitumia dakika kumi tu kumaliza kula, kisha wote kwa pamoja wakainuka na kwenda kukodisha pikipiki iliyowafikisha kijijini Mkalama.
Safari hii walifikishwa hadi nyumbani kwao kabisa. Walishuka kwenye pikipiki kisha wakapiga hatua za taratibu huku nyuso zao zikiwa zimepambwa na tabasamu pana. Bahati nzuri bibi alikuwa nje ameketi kibarazani.
Bibi alipowaona, alionekana kuukunja uso wake. Hata Chris alipojaribu kutabasamu, bado bibi aliendelea kukunja uso wake.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia
Powered by Blogger.