Lowassa ataja vipaumbe vyake 13 ndani ya siku 100
Mgombea
urais aliyesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia
Chadema, Edward Lowassa, ametaja vipaumbele vyake 13 ambavyo
atavitekeleza ndani ya siku 100 akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania
Oktoba 25, mwaka huu.

Lowassa alitaja vipaumbele hivyo wakati akizungumza katika mikutano mbalimbali ya kampeni jijini Dar es Salaam jana.
Alivitaja vipaumbele atakavyovitekeleza ndani ya siku 100 kuwa ni,
upatikanaji wa dawa na vifaa vya uzazi kwa kina mama, umeme wa uhakika
nchi nzima, kupunguza foleni jijini Dar es Salaam, kuondoa kero kwa
wafanyabiashara wadogo wadogo na bodaboda na kutengeneza mkakati wa
kumaliza tatizo la maji nchini ikiwamo Dar es Salaam.
Vingine ni kutengeneza mfumo bora na rafiki wa wafanyabiashara
wakubwa na wadogo, kufuta ada na michango kwa wanafunzi, kupunguza kodi
ya mshahara kwa wafanyakazi, kufuta kodi zote za mazao ya wakulima,
mkakati kabambe wa kukuza michezo na sanaa, kuunda tume ya kutatua
migogoro ya wafugaji na wakulima, kuanzisha kituo kila wilaya kwa ajili
ya kutoa huduma za serikali na kuboresha maslahi ya polisi, wanajeshi na
walimu.
Aidha, Lowassa alisema akichaguliwa kuingia Ikulu, kuanzia Januari,
mwakani hakuna Mtanzania atakayelipa ada ya shule wala mchango wa aina
yoyote.
Alisema zipo fedha nyingi na za kutosha kwa ajili ya kuwasomesha
Watanzania bure na kwamba akiingia Ikulu pia atafuta utaratibu wa
serikali kununua magari ya kifahari ili fedha hizo zitumike kuboresha
elimu nchini.
Kuhusu kuondoa umaskini, Lowassa alisema anauchukia, hivyo
atahakikisha anauondoa na kuwataka vijana kuhakikisha wanampigia kura
ili kumuingiza ikulu Oktoba 25, mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment