ad

ad

MLIBERIA WA YANGA KUFANYA MAAJABU KESHO TAIFA

 

Mshambuliaji Kpah Sherman, raia wa Liberia.

MSHAMBULIAJI Kpah Sherman, raia wa Liberia, amekamilisha mchakato wa vipimo vya afya na kisha moja kwa moja akaanza mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Boko Veterani nje kidogo ya Dar, jana jioni.

Sherman ambaye inaelezwa kuwa atapewa mkataba wa miaka miwili mara baada ya mazungumzo ya usajili wake kukamilika, alifanya mazoezi maalum chini ya Kocha Msaidizi wa Yanga, Leonaldo Neiva ambapo alikuwa tofauti na wenzake waliokuwa wakisimamiwa na kocha mkuu Marcio Maximo.

Katika mazoezi hayo ya jana, Mliberia huyo ambaye ametua nchini juzi Jumatano, bila kujali uchovu wa safari, alianza kwa kuzunguka uwanja raundi 10, akaruka koni mara 10, akapiga mpira kontroo kwa dakika kadhaa, akazunguka tena uwanja mara mbili, hivyo kuwa amezunguka uwanja mara 12.

Wakati anawasili uwanjani hapo mchezaji huyo aliteka hisia za umati wa mashabiki waliofika uwanjani hapo, ambapo wengi wao walisema uwezo wa pumzi anaouonyesha mchezaji huyo ni kama maajabu kwani angekuwa mchezaji mwingine angehitaji kupumzika hasa kwa kuwa alitoka safari ndefu ya kutoka nchini Cyprus anapocheza soka la kulipwa na kutua Dar, juzi.

“Afya ameshapimwa, alipelekwa uwanjani kwa ajili ya kujiweka fiti ili kesho ndiyo aanze mazoezi rasmi na wenzake, kila kitu kikienda fresh tutavunja mkataba wake na klabu anayoichezea ambapo amebakiza mkataba wa miezi minne,” alisema kiongozi mmoja wa Yanga.

Mliberia huyo ambaye amekabidhiwa jezi namba 25 iliyokuwa ikivaliwa na Emmanuel Okwi ambaye yupo Simba, alizungukwa na umati mkubwa mara baada ya mazoezi hayo, ambapo mashabiki wengi walihitaji kujua kama ameshapewa mkataba.

“Kesho (leo) nitakuja kufanya mazoezi kamili, leo (jana) nilikuwa napasha misuli tu, kuhusu mkataba wakala wangu ndiyo wa kulizungumzia hilo,” alisema Sherman.Wakati mchezaji huyo akitua mazoezini, Kocha wa Yanga, Marcio Maximo ameonekana kuwa bize na kutafuta kikosi ambacho kitaanza kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba, kesho Jumamosi.

Inavyoonekana Maximo huenda akaipata hivi timu yake: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Emerson, Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima na Andrey Coutinho.

Aidha, wakati likiingia mtamboni Championi Ijumaa lilipata taarifa kuwa Yanga imepanga kumpa mkataba wa miaka miwili Mliberia huyo na mchezaji atakayeondolewa kuziba nafasi yake ni Kiiza.

No comments

Powered by Blogger.