ad

ad

JINI LA DARAJA LA SALENDA - 12




ILIPOISHIA;
Uso wake ulionesha huzuni kitu kilichomtisha mumewe ambaye alitaka kujua kulikoni.
“Vipi mahabuba wangu?”
“Mambo yameharibika.”
“Kivipi?”

“Mpango wetu umeingia kwenye mtihani wa kwanza.”
“Mtihani upi?”
“Kizazi kimoja kimechukuliwa.”
 “Tufanye haraka kabla hakijarudishwa kwa mwenyewe tumtume  Kulani akaifanye kazi hii kabla hakujapambazuka.”

“Tumechelewa tayari kimeisharudishwa kwa mwenyewe.”
“Umejuaje?”
“Damu ya sehemu kilipotoka nilipoigusa imeganda kidoleni.”

“Ooh! Nani anataka kuchezea himaya yangu lazima nimkomeshe,” Mfalme Barami Hudirud alisema kwa hasira.
“Hebu kaniletee damu ya sehemu iliyotoka kizazi ili nimjue ni nani?”
SASA ENDELEA...

Malkia Huleiya alikwenda hadi kwenye chumba cha siri na kurudi na damu ya sehemu iliyochukuliwa kizazi cha Sharifa na kumpelekea mumewe.
“Naomba niilambe.”
Malkia Huleiya alimlambisha mumewe, mfalme alitulia kwa muda kisha alisema:
“Nimeishamjua, nitamtuma Kulani akishindwa nitakwenda mwenyewe.

Lazima nitamuonesha mimi ni nani.”
“Umemgundua ni nani?”
“Kuna mshenzi mmoja anataka kushindana na nguvu zangu, nataka mpaka kutakapopambazuka awe amebakia jina.”

“Kulaniiiiii,” aliitaka kwa sauti ya juu ambayo kama mwanadamu angeisikia basi angepasuka ngoma za masikio.
Kulani aliyekuwa mbali alikuja mbio na kupiga magoti mbele ya mfalme.
“Rabeka mtukufu mfalme.”
“Nataka uende duniani, damu hii itakuongoza mpaka kwa mtu huyu, nataka umfutilie mbali, sawa?”

“Sawa mtukufu mfalme.”
“Haya ondoka mbele yangu, usirudi mpaka umemfutilia mbali kiumbe huyo dhaifu anayetaka kucheza na nguvu zangu.”
Kulani alizama chini ya ardhi na kutoweka, baada ya muda alikuwa pembeni ya bahari eneo la Bagamoyo, aliilamba damu aliyopakwa kidoleni ambayo ilimuelekeza aende upande upi. Alitoka eneo baharini na kuelekea kwa Mganga Njiwa Manga.

Alitembea taratibu toka eneo la bahari akiwa katika umbile la kibinadamu,  hakuchelewa kufika kwenye makazi ya watu. Aliilamba tena ile damu iliyokuwepo kidoleni mwake, kwa vile kulikuwa na giza, sehemu ya Mganga Njiwa Manga ikawaka mwanga wa taa.

Mwanga ule ulimuongoza hadi karibu kabisa na nyumba ya Mganga Njiwa Manga. Nia yake kubwa ilikuwa kwenda mpaka mlangoni na kugonga ili akifungua tu wakutane uso kwa uso na ammalize pale pale kisha aondoke kabla hakujapambazuka.

Alitembea kuelekea eneo la nyumba ya mganga, ajabu alipokaribia nyumba yake alishangaa kuona moto ukiwaka  kuizunguka nyumba ile. Hali ile ilimshtua sana, aligeuka na kutimua mbio hadi baharini ambako alikunywa maji mengi na kurudi hadi kwenye eneo la nyumba ya mganga.

Alipoikaribia moto uliwaka tena, alilisogelea eneo la nyumba huku akimwaga maji aliyoyachukua baharini kwa lengo la kuuzima moto ule. Alifanikiwa lakini alipotaka kuingia kwenye himaya  ile moto uliwaka tena. Alijikuta akifanya kazi ya kwenda baharini na kurudi, kila alipouzima moto na alipotaka kuingia uliwaka tena.

Kulani alijikuta akitumia muda mwingi kwenda baharini kuchukua maji na kurudi huku moto ukizimika na kuwaka.  Mpaka kulipokuwa kunakaribia kupambazuka hakuweza kuingia katika himaya ya Mganga Njiwa Manga. Kwa upande wake aliiona kazi imekuwa ngumu au maji yalikuwa marefu na  kuamua kurudi chini ya bahari, aliogopa kutokana na kauli aliyopewa na Mfalme Barami Hudirud kuwa asirudi chini ya maji mpaka ahakikishe amemmaliza Mganga Njiwa Manga.

Kulani alijikuta kwenye wakati mgumu katika kazi ile, tofauti na zilizotangulia ambazo alizifanya kwa muda mchache. Lakini ile ilikuwa ngumu kwake, baada ya kukutana na kikwazo cha moto.
 Aliamua kurudi hadi baharini akiwa katika umbile lile la kibinaadamu, alisubiri jua litochomoze ili aweze kwenda jirani kwa mganga na kumsuburi akitoka ammalize.

Jua lilipotoka na watu kuwa wengi kujaa ufukweni kwa ajili ya  kununua samaki na wengine wakipanda ngarawa kwenda kuvua.
Kulani alijichanganya na watu bila ya kujulikana kama ni jini. Baada ya pwani kuchanganya na watu kuongezeka, alijitoa eneo la bahari na kwenda kwa mganga kwa kutembea kama mtu wa kawaida.

Kila aliyemuona hakumdhania vibaya, aliacha eneo la bahari na kuingia makazi ya watu, alipokaribia maeneo ya nyumba ya mganga aliuona moto ukiwaka tena. Alikwenda kwenye nyumba ya jirani na kuomba kupumzika, kutokana na kuonekana kama mstaarabu, alikaribishwa na kupewa kiti. Mwenyeji wake hakujishughulisha naye aliendelea na shughuli zake na kumuacha Kulani akitupia jicho njia ya kutokea kwa Mganga Njiwa Manga.
Jini Kulani ataweza kutimiza azma yake ya kumuua Mganga Njiwa Manga?
Muda ulikwenda bila mganga kuonekana, kila alipopata wazo la kwenda kwenye nyumba ile alishangaa kuuona moto ukiwaka, lakini ulipotulia nyumba ilikuwa katika hali ya kawaida. Alijikuta yupo kwenye wakati mgumu akiamini kabisa ngoma ile ni nzito kwake kuchezeka.

Kilichomchanganya zaidi ilikuwa ni kauli ya mfalme Barami Hudirud ya kuhakikisha anammaliza mganga ndipo arudi, japo muda aliopewa ulipita.
Kulani alipata pigo baada ya mwenyeji wake kutaka kuondoka, akiwa bado kichwa kinamuuma alimwambia:

“Samahani kaka.”
“Bila samahani.”
“Nataka kuondoka kwenda pwani.”
“Hakuna tatizo funga mlango wako mimi niache hapa nimekaa baada ya muda nitaondoka.”
“Hapana kaka sikujui nimekukaribisha kibinadamu, lakini siwezi kukuamini kukuachia nyumba yangu, dunia haiaminiki siku hizi.”

“Sawa.”
Kulani alikubali kuondoka pale, lakini sehemu iliyokuwa nzuri kupaona kwa mganga ilikuwa kwenye nyumba ile iliyokuwa ikitazamana na ya mganga. Aliondoka kwa kuzunguka nyumba ile na kujigeuza haraka kuwa mjusi. Aliupanda ukuta haraka na kwenda kujificha chini ya bati bila kuonekana.

Mwenye nyumba ile alishtuka na kuzunguka nyuma ili kupata uhakika kama kweli yule mgeni atakuwa ameondoka. Lakini ajabu alipozunguka nyuma ya nyumba iliyokuwa na uwazi mkubwa wa kumuona mtu kama anatembea kutoka pale, hakumuona mgeni wake. Alijiuliza kwa sauti:

“Sasa atakuwa amekwenda wapi, mtu azunguke sasa hivi asionekane, mmh! Lisiwe jini lile, Mungu aniepushie mbali.”
Kulani alimtazama na kutulia akiwa amejilaza kwenye ukuta chini ya bati. Baada ya kusema yale mwenye nyumba ile aliondoka na kumwacha Kulani palepale nyumbani bila kujua.

Baada ya kuondoka, Kulani aliendelea kumsubiri mganga palepale ukutani chini ya bati katika umbile lile lile la mjusi kama atatokea Mganga Njiwa Manga amvae na kumuulia mbali. Alisubiri kwa saa kumi mpaka jioni ilipoingia ndipo alipomuona akiwa anamsindikiza mmoja wa wateja wake.

Jini Kulani aliteremka na kurudi katika umbile la mwanadamu na kumfuatilia kwa nyuma bila ya mganga kujua. Nia yake ilikuwa kukutana naye wakati anarudi ili amvae. Taratibu alitembea kumfuata kwa nyuma mganga aliyekuwa mbele akitembea huku akizungumza na wateja wake.

Njiani Mganga Njiwa Manga alianza kuhisi kama ardhi inatetemeka na mwili kuwa mzito, kitu kile kilichomfanya ageuke na kutazama nyuma. Alishtuka kukiona kiumbe cha ajabu kwa mbali kikija taratibu. Kwa haraka alichutama chini na kushika michanga huku akilikemea jitu lile ambalo liligundua limejulikana.

Wakati Kulani akijitayarisha kumvaa Mganga Njiwa Manga baada ya kugundua amejulikana, kabla hajamfikia alirusha vumbi la mchanga lililomuingia machoni na kumpofua macho. Alipiga kelele za maumivu na kujipiga chini kwa hasira na kusababisha kishindo kizito kilichotikisa eneo kubwa la Bagamoyo.

Kishindo kile kilisababisha watu waliokuwa karibu na sehemu kilipotokea waanguke na kupoteza fahamu. Nyumba nyingine zilipata nyufa kutokana na kushindo cha Kulani kupasua ardhi na kupotea. Baada ya robo saa hali ya eneo la Bagamoyo ilirudi kuwa ya kawaida.
Baada ya kurudi hali ya utulivu Mganga Njiwa Manga alinyanyua alipokuwa ameangukia baada ya kurushwa na udongo uliotoka kwenye shimo alilozama jini Kulani baada ya kupofuka macho. Alimtuma mtu kwenda nyumbani kumletea dawa ambayo alikunywa na kujimwagia kichwani.

Baada ya kuyafanya yale alikwenda hadi kwenye shimo lililokuwa limechimbika kama kumelipuka bomu. Sehemu ile aliweka dawa kisha aliondoka na kurudi nyumbani kwake. Alipofika nyumbani mwili ulikuwa  umechoka sana, hakuweza kuendelea na kazi ya matibabu, aliwaomba wagonjwa wake apumzike baada ya kunusurika kifo toka kwa jini ambaye hakujua ametoka wapi.

Siku ile hakufanya kazi yoyote, alilala mpaka siku ya pili huku akiviona viungo vyake vikipoteza nguvu. Hata alipolala hakuweza kujigeuza mpaka siku ya pili, kwake ulikuwa upinzani mkubwa katika kazi yake. Mara nyingi upinzani uliishia nje ya ngome yake, lakini hakikuwahi kiumbe chochote cha ardhini majini au angani kilichoweza kumdhuru.

Pia katika kazi yake haikuwahi kutokea kiumbe kilichowahi kumvizia njiani kwa  ajili ya kumdhuru. Wengi walivamia sehemu aliyokuwa akifanya kazi na kukutana na vikwazo. Lakini uwezo wa kinga yake ya mwili ndiyo uliomsaidia, bila hivyo angemalizwa na jini yule.
***

Jini Kulani baada ya kuzama chini ya ardhi kwa kujipigiza kwa hasira, aliibukia pembeni ya bahari. Alitembea taratibu huku akipapasa ili kuingia majini. Baada ya kutembea kwa muda alibahatika kuyakanyaga maji. Pale pale alizama chini.
Mfalme wa bahari alishangaa kumuona Mkuu wa Watwana Kulani amesimama mbele yake akiwa haoni.

“Kuna nini tena kimekusibu mtwana wangu mtiifu?”
“Mtukufu mfalme, safari yangu imekuwa mbaya.”
“Kulani umefanya makosa, kwa nini jana hukurudi?”
“Niliogopa mtukufu mfalme kurudi bila kutimiza ulichonituma.”
“Umekitimiza?”

“Hali yangu kama unavyoniona.”
“Tatizo nini?”
“Nimepofuka mtukufu mfalme.”
“Lakini hujanijibu, umemmaliza?”
“Sikuweza, yule mtu hata wewe sikushauri uende.”
“Kwa nini?”

“Amejidhatiti, ana nguvu za ajabu sijawahi kuona, ameizindika ngome yake haiingiliki, na yeye mwenyewe alichonifanya sitasahau mpaka nakufa.”
“Hapana lazima niende, hawezi kushindana na nguvu zangu.”
“Mtukufu mfalme, bado himaya ya chini ya bahari inakuhitaji lazima atataka kutumia nguvu za ziada kukumaliza. Nashukuru sikugusana naye ningeweza kupoteza maisha.”
“Kwa hiyo tuwaache wanadamu watuchezee?”

“Hapana, ila nguvu zinazidiana, yule mwanadamu ana nguvu za ajabu sana, nilijitahidi kuuzima moto alioutega kwenye himaya yake, nilishindwa kila nilipouzima na nilipotaka kuingia uliwaka tena nikajikuta kukipambazuka bila ya kuweza kuingia kwenye himaya yake. Ndiyo sababu ya kuchelewa kurudi na kuamua kubaki ili nihakikishe nammaliza akitoka kwake.  Lakini haikuwa hivyo matokeo yake nimekuwa kipofu.”

“Mmh! Nimekuelewa, basi mpelekeni akapate tiba.”
Watwana wengine walimchukua Kulani na kwenda kumpatia tiba ya macho, baada ya kuondoka, mfalme alimgeukia mkewe aliyekuwa kimya akimuangalia Kulani kwa huruma.
“Mke wangu umeona hali ilivyo, unanishauri nini kutokana na hali aliyorudi nayo Kulani?”

“Mmh! Mume wangu hali inatisha, inaonesha wazi vita ni nzito, tukifanya mchezo tutakwisha, mpaka Kulani kusema hivyo ujue kuna kazi. Kwa nini tusiachane na mpango wa kumfuatilia huyo mwanadamu?”
“Lakini mke wangu si unajua uwezo wangu? sijawahi kushindwa na kitu,” Mfalme alijitapa.

“Naujua vizuri, hata Kulani anaujua lakini mpaka kakukueleza vile naomba umsikilize huenda kuna kitu amekiona kinaweza kukupotezea maisha kama utashindana na yule mwanadamu.”
“Lakini kumbuka jini ana nguvu kuliko mwanadamu?’
“Lakini mwanadamu ndiye kiumbe mwerevu kuliko viumbe wote wa Mungu?”
“Hilo nalijua lakini bado hawawezi kushindana na sisi.”
“Mume wangu majini sisi hatuna ushirikiano, kuna majini wengine huwakinga mwanadamu na kuwafanya kuchanganya nguvu za kijini na akili ya kibinadamu lazima tu atakushinda.”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“La muhimu tuachane na mpango huo.”

“Na suala la Balkis kuolewa na jini mwenzake?”
“Hilo nalo ni gumu, tuendelee kumshawishi aweze kubadili mawazo na kuendelea na kazi ya kukusanya vizazi vya wanadamu na kutengenezewa dawa.”
“Mimi nina hasira, jaribu kuongea naye wewe.”

“Nitafanya hivyo jioni nitazungumza naye.”
Walikubaliana mke wa mfalme azungumze na Balkis ili aweze kubadili uamuzi wake wa kung’ang’ania kuolewa na mwanadamu.
****
Baada ya kuamka siku ya pili, Mganga Njiwa Manga bado mwili wake haukuwa na nguvu, wagonjwa wengi waliofika siku ile hawakupata huduma kutokana na hali yake. Ilibidi siku ile na yeye kutumia dawa za kujifusha na kunywa ili kujirudisha katika hali ya kawaida, baada ya kukumbwa na upepo wa jini Kulani.

 Kilichomshangaza kilikuwa rangi ya jini yule,  alikuwa mweusi kama rami tofauti na majini wote aliowahi kukutana nao. Siku ya pili tangu akutane na dhahama nzito ya jini Kulani, aliendelea na kazi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaotoka mbali.

Baada ya kuingia katika chumba chake kutoa huduma, alitulia kwenye mkeka kisha aliweka ubani kwenye kitezo na kutulia kwa muda ili ajiandae kwa matibabu ya wagonjwa waliokuwa wameongezeka kutokana na kusimama kwa huduma yake.

Ilikuwa ajabu baada ya moshi wa ubani kupanda juu, ulimfuata mbele ya uso wake na akaanza kuona picha asiyoielewa. Alikiona kiumbe cha ajabu kikitoka kwenye maji na ghafla kiligeuka na kuwa mwanadamu, kisha kilitembea taratibu toka kwenye ufukwe na kuingia maeneo ya watu.

Baada ya kiumbe kile kilichojigeuza kuwa binaadamu kukaribia ngome yake, kilijigeuza umbile na kurudia lile alilotoka nalo chini ya maji. Ajabu kilipotaka kuingia kwenye himaya yake aliona moto ukiwaka kuzunguka eneo lake, ghafla kiumbe kile kilitoka mbio kurudi baharini na kuchota maji kisha kuja kuzima moto.

Kiliendelea kuzima moto mpaka kulipopambazuka, kila kilichoendelea alikiona mpaka kupambana na jini lile. Hapo ndipo alipogundua jini lile lilitoka wapi, alicheka na kuona kinga aliyokuwa nayo ndiyo iliyomsaidia bila hivyo angekufa vibaya.
Taratibu moshi ulipungua na hali ya ndani ikarudi kuwa ya kawaida, Mganga Njiwa Manga aliendelea kuweka tena ubani uliotoa moshi wa kawaida bila kuwepo na kitu kisichokuwa cha kawaida. Alimtuma msaidizi wake kuwaita wagonjwa.

Nini kiendelea baada ya mganga kuonekana kudhibiti nguvu za kijini? Je, nini hatma ya Brighton katika chumba cha giza?  TUKUTANE SIKU YAKESHO

No comments

Powered by Blogger.