ad

ad

The Last Breath Sehemu ya 1,2 na 3


Mwaa!” Loveness alimbusu Johnson kwenye paji la uso, kisha akageukia upande wa pili na kumbusu shavuni mtoto wao Melania, binti yao mwenye umri wa miaka mitatu!
Moyoni mwake alisikia uchungu mno, hakuna kitu alichokichukia kama kuagana na watu aliowapenda. Kwa hakika mume wake Johnson na binti yake Melania, ndiyo walikuwa watu pekee aliowapenda kuliko wengine wote chini ya jua la Mungu.
Kwa nguvu zake zote alijitahidi kuyazuia machozi yasimlengelenge lakini haikuwezekana, taratibu yakazipenya kope na kuanza kushuka kuelekea mashavuni, Johnson akachukua kitambaa mfukoni kwake na kuanza kumfuta huku akimtuliza asiendelee kulia mbele ya mtoto.
“Mpenzi si utakuja nyumbani kwenye Sikukuu ya Krismasi?”
“Ndiyo.”
“Kuanzia sasa mpaka Krismasi bado siku ngapi?”
“Kama mwezi mmoja hivi.”
“Sasa kwa nini unalia?”
“Sijielewi, moyoni mwangu nahisi kama nawaona kwa mara ya mwisho!” Loveness aliongea na kuzidi kububujikwa na machozi.
“Mama acha kulia!” Melania alimwambia mama yake na kumfanya ajisikie vibaya.
Katika maisha yake yote tangu azaliwe, Loveness alishasindikiza watu wengi sana stendi za basi, viwanja vya ndege, bandarini waliokuwa wakiondoka na kumwacha, ni kweli aliumia na kusikitika na ndiyo maana alizichukia sana sehemu hizo, lakini siku hiyo aliumia zaidi kuliko siku nyingine zilizotangulia, kuna sauti ilimwambia kutoka ndani kabisa kwamba asingewaona tena lakini alibishana nayo.
“Kwa kweli ungekuwa uwezo wangu, ningewazuia msisafiri!”
“Kwa nini?”
“Najisikia vibaya mno Johnson, nahisi kuna tatizo litatokea!”
“Hapana,  hizo ni hisia tu mpenzi! Acha nimrudishe Melania Dar es Salaam, Jumatatu anatakiwa darasani, si unajua likizo yenyewe ilikuwa ni ya wiki moja tu, tumekuona mpenzi, utatukuta Dar es Salaam utakapokuja na safari hii ninataka nikufanyie ‘sapraizi’ ambayo hutaisahau maishani mwako!”
“Sapraizi gani?”
“Wewe utaona ukija, siwezi kukuambia sasa hivi!” Johnson aliongea, ingawa moyoni mwake alielewa alitaka kumnunulia mke wake gari mpya aina ya Range Rover Evoque.
Zamu yao ya kuingia uwanjani ikafika,  hawakuwa na namna tena ya kuendelea kubaki nje, muda wa kuiacha Kinshansa ulikuwa umefika na pia kumwacha Loveness peke yake akiendelea na kazi katika Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambalo ofisi zake zilikuwepo katika jiji hilo,  alikofanya kazi kama Afisa Ustawi wa Jamii.
Loveness alimwangalia Johnson machoni, akahamishia tena kwa mtoto wake, akakosa nguvu za kuwaangalia, akainamisha uso wake chini, machozi yakadondoka sakafuni! Alichokifanya Johnson ni kujiondoa kwenye foleni, asingeweza kuondoka na kumwacha katika hali hiyo, akamkumbatia kwa mkono wake wa kuume kisha kumtaka afumbe macho yake ili wamwombe Mungu pamoja.
“…Mungu mwema, ubaki na mke wangu mpaka tutakapokutana naye tena, unajua ni kiasi gani nampenda na ningetaka kubaki hapa Kinshasa pamoja naye, lakini haiwezekani sababu ya majukumu yaliyoko nyumbani, hivyo basi namwacha mikononi mwako, nasi tubariki katika safari yetu mpaka tufike Dar es Salaam…” Johnson alimaliza sala yake na kumpiga busu Loveness usoni kwake.
Kilichofuata baada ya hapo ni kuingia uwanjani ambako walikaguliwa mizigo yao pamoja na wao wenyewe, kabla hawajaingia ndani kabisa Johnson akiwa amembeba Melania, aliangalia nje na kumwona Loveness amesimama palepale walipomwacha, mwanamke mmoja akionekana kumbembeleza aache kulia.
“Mama bye!” Melania aliongea kwa sauti ya juu mpaka watu wengine wakageuka.
“I love you Melania!”
“I love you to mom!”
“Take care of yourself and listen to teacher Joyce in the class, okay?” (Ujichunge na msikilize mwalimu Joyce darasani, sawa?)
“Yes mom, I will.” (Ndiyo mama, nitafanya hivyo!)
“Bye baby!” (Kwaheri mpenzi!)
“Bye husband!” (Kwaheri mume wangu!)
Johnson na mtoto wake wakazama ndani ya uwanja ambako walikuta pilikapilika za watu wakikimbia huku na kule kujaribu kuwahi ndege zao, moyoni mwake Johnson alisumbuliwa sana na alichokionyesha mke wake uwanjani, yeye mwenyewe akaanza kuingiwa na aina fulani ya hofu lakini akamwamini Mungu na kutembea moja kwa moja hadi chumba cha kusubiria ambako walikuta tayari abiria wa ndege yao wamekwishaanza kupanda.
Loveness hakuondoka uwanja wa ndege, alichokifanya ni kusogea nyuma kidogo kuliacha jengo la uwanja katika sehemu ambayo angeweza kuziona vizuri ndege zilizoruka. Dakika ishirini na tano baadaye aliiona ndege ndogo ya Shirika la Ndege la Kongo, yenye uwezo wa kubeba abiria hamsini ikiruka, hiyo ndiyo Johnson na Melania walipanda, akanyanyua mikono yake juu na kumwomba Mungu aepushe kile ambacho moyo wake ulikuwa  ukikihisia.

***
Ndege ilishaacha sehemu ya mawingu, Johnson na mwanaye Melania walikuwa wameketi vizuri kwenye viti, mkononi Melania alikuwa akichezea michezo ya kompyuta kwenye IPad. Tayari walishatangaziwa kwamba ishara za  mikanda zilishaondolewa, hivyo  waketi vizuri kwenye viti vyao na kufurahia safari.
Walikuwa wakipita kwenye futi ishirini na tano elfu juu ya usawa wa bahari, hali ya hewa ilikuwa safi kabisa, ndege imetulia kama vile walikuwa sebuleni nyumbani kwao. Wahudumu wa ndege waliwafikia na kuwauliza kile walichohitaji kutumia, Johnson akaagiza chai na kwa ajili ya mtoto wake akaagiza juisi ya sharubati pamoja na pakiti ya korosho.
Juisi zilipowekwa tu juu ya meza, ghafla mlipuko mkubwa sana ukatokea na harufu ya kama kitu kilikuwa kinaungua ikasikika! Abiria wote ndani ya ndege wakapatwa na mshtuko na kelele zikaanza kusikika, ingawa wafanyakazi ndani ya ndege hiyo walijitahidi kama hapakuwa na kitu kilichotokea kwa kuweka tabasamu usoni, abiria walishagundua kwamba tatizo kubwa lilikuwa limetokea.
Troli lililobeba chakula na vinywaji likaanza kusukumwa kuondolewa katikati mpaka sehemu yake, wahudumu wakaketi kwenye viti na kufunga mikanda, abiria wote wakatakiwa kufanya hivyo. Sekunde chache baadaye sauti ya rubani ikasikika akiwaeleza kwamba injini moja ya ndege yao ilikuwa imelipuka na kusimama kufanya kazi, hivyo walikuwa wanatumia injini moja tu, akawatuliza kwa kuwaambia wasiwe na wasiwasi kwani kwa injini moja wangeweza kufika angalau Bujumbura ambako wangetua kwa dharura.
Watu wakatulia kidogo baada ya kuelezwa maneno hayo, haikuwa hivyo kwa Melania ambaye alikuwa akilia kwa nguvu huku akitaja jina la mama yake. Kazi ya Johnson ikawa ni kumtuliza na kumwambia kila kitu kingekuwa sawa, ingawa kichwani mwake akielewa kabisa walikuwa katika hatari na kwamba kumbe Loveness alikuwa ameona kitu kilichokuwa kinakwenda kutokea.
Hali ilikuwa mbaya, ndege sasa ilikuwa ikienda kwa mwendo wa taratibu kuliko mwanzo huku harufu ya kitu kilichokuwa kinaungua ikisikika na moshi ukiingia ndani ya ndege kiasi cha watu kuanza kukohoa. Melania alikohoa sana pengine kuliko watu wengine, Johnson akachanganyikiwa kabisa.
Vifaa vya kupumulia vikashuka kutoka eneo la juu la kuhifadhia mizigo, Johnson akachukua kimoja na kumvisha mtoto wake kisha yeye mwenyewe kuvaa cha kwake, vikasaidia kidogo katika upumuaji. Ghafla ndege ikaanza kuyumba kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Dakika kama kumi hivi baadaye mlipuko mwingine wa pili ulisikika tena, moshi ukazidi ndani na ndege badala ya kwenda mbele ikaanza kushuka kwenda chini! Sauti iliyosikika kupitia kwenye kipaza sauti ilikuwa ni ya rubani akiwatangazia abiria kwamba injini zote za ndege zilikuwa zimelipuka na sasa ndege yao ilikuwa ikienda chini kwa kasi ambako ingejipiga chini.
“Kila mmoja wetu anaweza kusali kwa dini yake, pengine Mungu anaweza kutunusuru!” ilikuwa ni sauti ya rubani.
Hapo ndipo Johnson akaelewa kwamba kweli walikuwa wanakufa, akamsogeza mtoto wake karibu na kuanza kulia huku akimwomba Mungu atende muujiza wowote ambao angeweza, taswira ya Loveness akilia uwanja wa ndege iliendelea kumwijia, akajuta ni kwa nini hakumsikiliza.
“Dad are we going to die!”(Baba, tunakufa?)
“No! We can’t die, just pray!”(Hapana, hatuwezi kufa, sali tu!) Johnson alimwambia Melania ingawa alikuwa na uhakika kabisa kilichosemwa na mtoto wake kilikuwa kweli.
Ndege ilikuwa ikishuka kwa kasi mno kiasi cha kuhisi utumbo ulitaka kupitia mdomoni, Melania alikuwa akilia kwa nguvu na kuita jina la mama yake.
***
Nisingependa kumaliza hadithi hii ya leo bila kukumbusha jambo muhimu la kutoa maisha yako kwa Mungu. Maisha tuliyonayo hapa duniani ni mafupi sana, yanapita kama maua yachanuavyo na kunyauka. Wengi unaowafahamu wamekufa lakini wewe unapumua, ni vyema basi kufikiria maisha baada ya kifo.
Kila siku jiulize: “Hivi nikifa leo nitakwenda jehanam au peponi?” Kila mmoja wetu analo jibu lake, bila shaka sote tungependa kwenda peponi. Kama hivyo ndivyo, basi tiketi ya kwenda huko ni matendo mema na kujiepusha na uovu.
Tukumbuke mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele.

The Last Breath - 2

Loveness, mwanamke wa Kitanzania aliyekuwa akifanya kazi katika Shirika la Kimataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR), yupo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kinshasa akiwasindikiza mumewe kipenzi, Johnson na mtoto wao, Melania waliokuwa wanaelekea Dar es Salaam yalipo makazi yao.
Muda wote roho ya Loveness ilikuwa ikisita kwani alishaanza kuhisi kuwa kuna jambo baya litatokea kwenye safari hiyo. Anajaribu kuwazuia mumewe na mwanaye lakini wanamtoa wasiwasi. Hata mwenyewe hajui ni kwa sababu gani roho yake inasita. Baadaye anaamua kuwaruhusu kwa shingo upande.
Johnson na mwanaye wanapanda ndege na safari ya kuelekea Dar es Salaam inaanza lakini kama Loveness alivyohisi, ndege yao inapata hitilafu kubwa ikiwa angani ambapo injini zote mbili zinaacha kufanya kazi na kusababisha taharuki isiyoelezeka.
Ndege inaanza kushuka chini kwa kasi kubwa huku Johnson akiwa amemkumbatia mwanaye.
Je, nini kitafuatia? Watasalimika?
SONGA NAYO…
Ndege ilikuwa ikienda chini kwa kasi ya ajabu ikizunguka chini juu, mizigo ikianguka kutoka katika sehemu za kuhifadhia na kuwaponda abiria huku viti viking’oka vikiwa vimewabeba abiria walioshikiliwa na mikanda.
Hewa ilikuwa nzito mno, watu walishindwa kupumua, moshi ulitanda kila mahali, hakuna aliyekuwa na uwezo wa kuona hata mita moja mbele yake!
Johnson alikuwa amemkumbatia mwanaye Melania ambaye tayari alishanyamaza, kifua kikiwa kimembana.  Alichokuwa akiendelea kukifanya Johnson ni kumwomba Mungu atende miujiza, kwani hakika kilichokuwa mbele yake na mwanaye kama Mungu asingeingilia, kilikuwa ni kifo tu.
Kwa kasi ya ajabu mawazoni mwake alikumbuka kila kilichotokea tangu kuzaliwa kwake mpaka siku hiyo, wazazi wake ambao tayari walikuwa marehemu ambao kama angekufa alikuwa anawafuata, ndugu zake, rafiki zake, biashara zake, waumini wenzake kanisani, mwanaye Melania ambaye alikuwa anakufa naye, mwisho kabisa taswira ya mkewe Loveness ikasimama mbele yake akisema maneno aliyoyasema uwanja wa ndege kabla hawajapanda.
“Kwa kweli  ungekuwa uwezo wangu ningewazuia msisafiri,” maneno ya Loveness yalijirudia kichwani mwa Johnson, akajuta!
Tayari watu wote ndani ya ndege walikuwa kimya, kama vile hapakuwa na binadamu, kelele za vyuma peke yake ndizo zilisikika!  Johnson akaamini watu hufa ndani ya ndege kabla haijapiga chini au kuzama majini, akazidi kumkumbatia mwanaye huku akimwomba Mungu atende miujiza.
Haukupita muda mrefu sana baada ya hapo, naye akawa hajitambui tena!  Wala hakuelewa kilichoendelea, giza lilikuwa limeyafunika macho yake.
  ***
Baada ya kushuhudia ndege ikiwa mawinguni, jambo lililoashiria mumewe na mwanaye walikuwa wameondoka, Loveness alichora alama ya msalaba kwenye paji la uso wake na kifuani kisha kuondoka mahali alipokuwa amesimama hadi kwenye gari lake la Nissan Hard Body ambalo ubavuni lilikuwa na maandishi ya UNHCR, akaingia ndani, kuwasha na kuondoka zake kuelekea nyumbani.
Moyo wake ulikuwa mzito, mawazo yakiwa yamemjaa kichwani mwake.  Hakika tangu azaliwe, hakukumbuka siku yoyote maishani aliyowahi kujisikia kama alivyokuwa akijisikia muda huo.
Alipotupa macho yake kwenye saa ya mkononi aina ya Seiko-5 aliyoivaa aligundua ilikuwa tayari saa 6:20 mchana, kulikuwa na saa tatu kabla Johnson na mwanaye hawajaingia jijini Dar es Salaam, maana ilikuwa ni lazima wapitie Nairobi ambapo wangeunganisha na ndege nyingine ambayo ingewafikisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa J.K. Nyerere.
Kilometa kama mbili hivi kutoka uwanjani, moyo wake ulizidi kuwa mzito, akajikuta akiwa na hamu kubwa sana ya kuzungumza na Mungu.  Hivyo akawa anaendesha gari huku akiangalia kushoto na kulia kama angeona kanisa mahali popote, mita kama 800 mbele, macho yake yaliona jengo kubwa jeupe lenye msalaba kwa mbele, akajua hilo ni kanisa na hakutaka kusubiri mpaka afike nyumbani, akakatisha kulia kulifuata kanisa hilo.
Aliegesha gari na kushuka haraka kisha kukimbia hadi ndani ya kanisa lililokuwa wazi, bahati nzuri hakumwona mtu yeyote mahali popote, haraka akanyosha hadi madhabahuni na kupiga magoti mbele ya msalaba wa Bikira Maria, maana lilikuwa ni Kanisa la Kikatoliki na yeye alikuwa muumini wa dhehebu hilo.   Hivyo akasali sala ya kuomba ulinzi.
Alipomaliza mashavu yake yote yalikuwa yamelowa machozi, akanyanyuka na kuanza kujifuta.  Kisha kuanza kutembelea kuelekea nje, kabla hajatoka alikutana na Mzungu mzee aliyevaa nguo nyeupe, akaelewa moja kwa moja huyo alikuwa ni padri.
“Bonjour!” (Salama?) padri alimsalimia kwa Kifaransa.
“Bonjour!” (Salama!) akajibu.
“Pourquoi pleures-tu?”  (Kwa nini unalia?)
“Je pense quelque chose de mauvais ne peut arriver!”  (Nahisi jambo baya litatokea)
“Qu-est-ce que c’est? (Jambo gani hilo?)
Loveness akaanza kumsimulia padri huku akizidi kububujikwa na machozi, alichokifanya kiongozi huyo wa dini ni kumpeleka hadi ofisini kwake ambako aliendelea kumfariji na baadaye wakasali tena pamoja kisha kumruhusu aende nyumbani kwake akiamini hakuna baya lingetokea, Loveness aliondoka lakini maneno ya padri hayakuwa yamemuondoa kwenye hofu aliyokuwa nayo.
Nyumbani kwake eneo la matajiri mjini Kinshasa ambalo waliishi wafanyakazi wengi wa Umoja wa Mataifa, aliegesha gari na kuingia ndani akajitupa kitandani na kuendelea kufikiria juu ya mume na mtoto wake, haukupita muda mrefu sana, akiangalia runinga, usingizi ulimpitia.
Alizinduka saa mbili baadaye na kutupa macho yake kwenye saa ya ukutani,  ilikuwa tayari saa 10:40, saa nzima karibu na nusu tangu Johnson na mwanaye watue jijini Dar es Salaam, haraka akanyanyuka na kuikwapua simu yake kutoka kwenye meza ya kando mwa kitanda, akijua lazima Johnson alikuwa amepiga kumjulisha kwamba walifika salama mwisho wa safari yao.
Hapakuwa na simu iliyopigwa kutoka kwa Johnson, watu wengine tu walikuwa wamempigia ambao kwa wakati huo hawakuwa na umuhimu wowote.  Haraka akabonyeza namba ya Johnson ili aongee naye, haikuita!  Akaguna na kuendelea kupiga maana haikuwa kawaida ya Johnson kabisa kuzima simu yake hasa baada ya kufika mwisho wa safari.
Alipiga mara nyingi mno lakini bado simu iliendelea kutokuita, sauti ya mtambo ikimtaarifu kwamba simu hiyo ilikuwa imezimwa.  Mpaka giza linaingia, bado alikuwa akijaribu kupiga bila mafanikio.  Hatimaye akafikia uamuzi wa kupiga simu nyumbani kwake kwa mfanyakazi.
“Deborah!”
“Bee!”
“Mama hapa!”
“Ndiyo mama, za huko? Baba na Melania hawajambo?” mfanyakazi wa ndani aliuliza.
“Oh!  My God!” (Mungu wangu) alisema Loveness akiwa haamini kama Johnson na mwanaye eti walikuwa hawajafika nyumbani.
“Mama, unasemaje?”
“Baba hajafika?”
“Bado, Dioniz amekwenda kuwapokea uwanjani!”
“Una namba ya Dio?” aliuliza Loveness ili apewe namba ya mdogo wake na Johnson waliyekuwa wakiishi naye nyumbani kama dereva wao.
“Ndiyo!”
“Nipe!”
Alipotumiwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu, Loveness alipiga namba ya Dio, akapokea, swali la kwanza alilomwuliza ni kama alikuwa na Johnson pamoja na Melania.
“Hapana shemeji, nawasubiri hapa uwanjani, ndege yao imeandikwa delayed, ina maana imechelewa, watu wanaanza kukosa uvumilivu maana tumesubiri muda mrefu sana, wanataka kuambiwa kama kuna tatizo lililotokea!”
“Watu wa uwanja wanasemaje?”
“Wanababaika tu!”
“MUNGU WANGU! NAOMBA MAWAZO YANGU YASIWE KWELI, HII IWE NI NDOTO!” alisema Loveness na kukata simu.
Nisingependa kumaliza hadithi hii ya leo bila kukumbusha jambo muhimu la kutoa maisha yako kwa Mungu. Maisha tuliyonayo hapa duniani ni mafupi sana, yanapita kama maua yachanuavyo na kunyauka. Wengi unaowafahamu wamekufa lakini wewe unapumua, ni vyema basi kufikiria maisha baada ya kifo.
Kila siku jiulize: “Hivi nikifa leo nitakwenda jehanam au peponi?” Kila mmoja wetu analo jibu lake, bila shaka sote tungependa kwenda peponi. Kama hivyo ndivyo, basi tiketi ya kwenda huko ni matendo mema na kujiepusha na uovu.
Tukumbuke mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele.

The Last Breath - 3

ILIPOISHIA...
JOHNSON na mtoto wake mzuri Melania walikwenda Kinshasa kwa likizo ya wiki moja kabla Melania hajafungua shule, huko ndiko mama yake Melania, Loveness, anafanya kazi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), likizo yao inakwisha na wanapanda ndege ya Shirika la Ndege la Congo kurejea Dar es Salaam kupitia Nairobi.  
Moyo wa Loveness una wasiwasi mwingi, angetamani sana Johnson na mwanaye wasisafiri, anahisi kuna tatizo litatokea lakini alipomweleza mume wake, hakukubali!  Wakaruka na kuondoka wakimwacha na huzuni nyingi, wakiwa angani hali inabadilika, injini zinapasuka na ndege kuanza kuporomoka kwa kasi  kwenda chini.
Johnson akijua mwisho wa maisha yao umefika alimkumbatia mtoto wake akijilaumu ni kwa nini hakumsikiliza mke wake, baadaye wote wakapoteza fahamu na hawakujua tena kilichotokea!  Huku nyuma, Loveness akiwa na wasiwasi mwingi anapiga simu nyumbani na kuambiwa bado hawajafika, moyo wake unaingia wasiwasi mwingi akiomba mawazo aliyokuwa nayo yasiwe kweli na kila kitu kilichokuwa kikiendelea kiwe ndoto.
Je, ni nini kitafuata?
songa nayo...
ALICHOKIFANYA Loveness moyo wake ukiwa umejawa na huzuni pamoja na wasiwasi mwingi, huku hisia zikimtuma kuamini kwamba alichokuwa akikifikiria kichwani mwake ni kweli, kwamba mume na mtoto wake walikuwa wameanguka na ndege waliyokuwa wakisafiri nayo na kufa, jambo ambalo bado hakutaka kukubaliana nalo, alifikia  uamuzi wa kuwasha runinga yake ili aone kama kulikuwa na taarifa yoyote ya habari kuhusu tukio la kuanguka kwa ndege; akachagua CNN na kuketi kitako kitini, macho yake yote akiwa ameyaelekeza kwenye kioo.
Haukupita hata muda wa dakika tano maneno “DERNIERES NOUVELLES.” ambayo kwa Kiingereza ilimaanisha “BREAKING NEWS” yaani habari za hivi punde kwa Kiswahili, yalionekana, mtangazaji akiwa Samantha Jonathan, Loveness akatulia kitini akitamani ambacho kingetangazwa kiwe kitu kingine tofauti na suala la ndege kuanguka, haikuwa hivyo;
“L’information que nous venens de recevoir le rapport qu’un avio qui volait de Kinshasa a Nairobi avec une cinquantaine de passagers a bord est perdue probablement s’est ecrase…”
“Taarifa ambazo zimetufikia hivi punde zinaeleza kwamba ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Kinshasa kuelekea Nairobi, ikiwa imebeba jumla ya watu hamsini,  imepotea angani na kuna uwezekano imeanguka kwenye msitu wa Congo au kuzama kwenye Bahari ya Atlantic…”
Loveness hakuweza kuimaliza taarifa hiyo ya habari, akasikia kizunguzungu na baadaye giza nene kuyafunika macho, fahamu zikampotea!  Jirani yake ambaye pia alikuwa ni mfanyakazi wa UNHCR, ndiye aliyemgundua nusu saa baadaye kwani alikuwa na taarifa za Loveness kumsindikiza mume na mtoto wake waliokuwa wamekuja Congo likizo.
Alimkuta akiwa amelala kwenye kochi, damu zikimtoka puani, mdomoni na masikioni.  Alichokifanya ni kupiga simu haraka sana ofisini kwao ambako walituma gari la wagonjwa kwenda kumbeba na kumpeleka Kinshasa General Hospital ambako alipokelewa na kupelekwa haraka iwezekanavyo chumba cha wagonjwa mahututi akiwa hajitambui.
Kwa haraka vipimo vilifanyika na kuthibitisha kuwa mshipa wa damu ulikuwa umepasuka kichwani mwake baada ya shinikizo la damu kupanda sana, hivyo uamuzi uliofikiwa na UNHCR baada ya kutokuwepo kwa daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo mjini Kinshasa ni ndege ya shirika hilo kumbeba Loveness akiwa katika hali ya kutojitambua moja kwa moja hadi jijini Dar es Salaam ambako alipokelewa uwanja wa ndege na kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kundi la madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo walikusanywa haraka iwezekanavyo na hatua zikaanza kuchukuliwa katika kujaribu kuokoa maisha ya Loveness ambaye bado alikuwa hajitambui, huku akipagwa na degedege na kuuma meno jambo lililosababisha awekewe kipande cha ubao kilichozungushiwa kitambaa mdomoni ili asiume ulimi wake.
“She needs a Craniotomy urgently, to remove a huge blood clot under the cranium, which is compressing the left hemisphere of the brain!” (Anahitaji kupasuliwa kichwa haraka iwezekanavyo ili kuondoa bonge la damu iliyoganda chini ya kichwa ambalo linaugandamiza ubongo upande wa kushoto!) aliongea Dk. James Mabula, bingwa wa upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“What is the cause of that blood clot?” (Nini kimesababisha hiyo damu iliyoganda?)
“The blood pressure went suddenly high, and caused a rapture of a blood vessel intracranially, and therefore bleeding which resulted into a clot!” (Shinikizo la damu lilipanda ghafla na kusababisha mshipa wa damu kupasuka chini ya fuvu, hivyo damu kuvuja na kuganda!”
“So this is stroke?” (Kwa hiyo hiki ni kiharusi?) mwanafunzi mwingine wa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Muhimbili akichukua udaktari aliuliza.
“Yeah!” (Ndiyo!) Dk. Mabula alijibu.
“There is another patient in the ward, he also has stroke, but he can still talk, why is this one unconscious?” (Kuna mgonjwa mwingine wodini, pia ana kiharusi lakini bado anaweza kuongea, kwa nini huyu hana fahamu?)
“The functions of the brain are like an ‘X’, the right part of the body is controlled by the left part of the brain and vice versa. So when a stroke happens, one part of the body paralyses, if that part is the right then the part of the brain affected is the opposite! This patient is paralyzed on the right side, it means the left side is the one affected.” (Kazi za ubongo ni kama alama ya ‘X’, upande wa kulia wa mwili unaongozwa na upande wa kushoto na upande wa kushoto unaongozwa na upande wa kulia kwenye ubongo. Kwa hiyo mtu anapopatwa na kiharusi, upande mmoja wa mwili hupooza, kama upande huo ni kulia basi upande ulioathirika kwenye ubongo ni wa kushoto.  Mgonjwa huyu amepooza upande wa kulia hii ina maana upande wa kushoto ndiyo ulioathirika.)
“I still want to know why is this patient unconscious, while the other one is conscious and they are all suffering from the same disease!” (Bado nataka kujua, ni kwa nini  mgonjwa huyu haongei lakini mwenzake anaongea na wote wanaumwa ugonjwa mmoja!) mwanafunzi alizidi kumbana mwalimu wake.
“Ngoja niongee Kiswahili unielewe vizuri, mtu akiwa anatumia mkono wa kushoto kuandika, basi kwenye ubongo sehemu yake ya kuongelea huwa iko upande wa kulia na mtu akiwa anatumia mkono wa kulia kuandika, basi sehemu yake ya kuongelea kwenye ubongo au kwa Kizungu inaitwa Speech Centre, huwa iko upande wa kushoto, hapo umenielewa?”
“Ndiyo mwalimu!”
“Ukifuatilia vizuri huyu dada kwa sababu amepooza upande wa kulia na hawezi kuongea, basi utaambiwa huwa anaandika kwa mkono wa kushoto, kuna ndugu yake hapa?”
“Ndiyo!” akaitikia kijana mmoja.
“Huyu mgonjwa huwa anaandikia mkono gani?”
“Wa kushoto!”
Mgonjwa akachukuliwa haraka na kukimbizwa chumba cha upasuaji ambako kazi iliyofanyika ni moja tu kufungua fuvu lake la kichwa na kuondoa damu iliyoganda, baada ya hapo Loveness akapelekwa chumbla cha wagonjwa mahututi akiwa bado hana fahamu yoyote na matumaini ya kupona yalionekana kuwa madogo, familia yake ilikuwa ikilia kwa uchungu kwani tayari walishapoteza watu wawili, mume wake pamoja na binti  yao Melania, hakika ulikuwa ni msiba mkubwa na kila mmoja wao alikuwa amekusanya mikono yake pamoja akimwomba Mungu angalau maisha ya Loveness yaweze kuokolewa.
“Daktari atapona?” mama yake Loveness alimuuliza daktari.
“Anaweza kupona, lakini tumwombe Mungu pamoja, jambo moja ninalolifahamu hata kama atapona, hawezi kuwa na kumbukumbu kabisa ya mambo ya nyuma na itabidi aanza kujifunza upya kuongea kama wanavyofanya watoto wadogo.” Dk. Mabula alisema.
“Haijalishi sana, ilimradi tu awe hai na tuwe tunamwona siku zetu za maisha yetu,” baba yake Loveness, mzee Materu aliongea akijifuta machozi.

  ***
Kama mtu mmoja angenyanyuliwa na kukalishwa angani juu ya Afrika Mashariki na Kati kisha akasikiliza sauti zilizokuwa zikitokea kwenye eneo hilo, angehuzunishwa mno na sauti ambazo angezisikia, maelfu ya watu walikuwa wakililia ndugu zao.
Kati ya watu walioaminika kufa katika ajali hiyo;  ishirini walikuwa Watanzania, kumi walitoka Kenya, wawili Uganda, wanne Uingereza, wawili Marekani, kumi walitoka Congo na marubani wawili walitokea Afrika Kusini. Huzuni ilitanda kila mahali, palikuwa na ukimya wa ajabu, hakuna ukumbi wa muziki uliopiga muziki usiku huo, kila mtu alikuwa akiomboleza.
Mipango ya kuitafuta ndege hiyo ilianza.
CHANZO NI GPL

No comments

Powered by Blogger.