The Last Breath (Pumuzi ya Mwisho) - 4
Ndege iliyokuwa ikisafiri na abiria kutoka Congo kuelekea Nairobi inaanguka, watu wote waliokuwemo wanaaminika kuwa wafu. Ni pigo kubwa kwa mwanamke aitwaye Loveness ambaye mumewe na mwanaye pekee Melania walikuwa wasafiri ndani ya ndege hiyo.
Moyo wa Loveness ulikuwa umesita kabisa wasisafiri, lakini mume wake akalazimisha. Taarifa za ndege hii kuanguka zinamfanya Loveness apandishe shinikizo la damu na baadaye kupata kiharusi, hivyo kulazimika asafirishwe kuja Dar es Salaam kwa ndege ya kukodi ambako anafanyiwa upasuaji wa kichwa.
Juhudi za kuitafuta ndege zimeanza.
Je, itapatikana? Je, watu wote waliokuwemo ni marehemu? Nini kitatokea katika maisha ya Loveness? SONGA NAYO…
Mipango ya kuitafuta ndege hiyo ilianza, helikopta zilikuwa zikizunguka huku na kule juu ya msitu wa Congo na juu ya bahari eneo la Angola, Gabon, Congo Brazzaville ambako watu wengi walidhani huenda ndege hiyo ilizama majini! Zilikuwa ni juhudi kubwa za ushirikiano wa nchi za Congo, Angola na Gabon lengo likiwa ni kuipata ndege hiyo na pia kiboksi cha kutunza kumbukumbu ili kujua kilichosababisha ianguke, wazo la kwamba abiria waliokuwemo wangekuwa hai hakuna hata mmoja aliyelifikiria.
Vyombo vya habari vya dunia nzima vilikuwa vikitangaza juu ya kuanguka kwa ndege hiyo, CNN, BBC ndizo zilizoonyesha kila kitu juu ya juhudi za kuitafuta ndege popote ilipokuwa. Kwa muda wa wiki mbili nzima, kazi yote iliyofanyika usiku na mchana baharini na juu ya msitu wa Congo haikuzaa matunda, watu wote walishindwa kuelewa ni wapi ndege ilikokuwa.
Ikabidi nchi ya Congo iamue kuomba msaada wa wataalam wa mambo ya ajali za ndege kutoka Marekani ambao pia walifika na kufanya kazi hiyo kwa muda wa wiki nzima bila mafanikio yoyote, ndugu wakazidi kulia na kuomboleza hasa walipoambiwa zoezi la kutafuta ndege hiyo ilibidi lisitishwe na watu kutangaziwa kwamba, ndege hiyo ilizama majini mpaka kwenye kina kabisa cha bahari, hivyo hapakuwa na uwezekano wa kuokoa chochote.
Maelfu ya watu waliokusanyika kwenye miji ya Nairobi, Kinshasa, Kampala, Dar es Salaam wakiwa na tumaini kwamba ndege hiyo ingeweza kupatikana na miili ya ndugu zao kuonekana, walivunjika moyo kabisa, wakarejea nyumbani ambako baadhi walifanya ibada ya mazishi, wakachimba makaburi na kuzika nguo pamoja na picha za marehemu, hivyo ndivyo ilivyofanyika hata jijini Dar es Salaam kwenye makaburi ya Kinondoni, ambako ndugu walizika nguo na picha za Johnson na mtoto wake Melania.
Ilikuwa siku ya masikitiko mno, kwenye makaburi ya Kinondoni, vilio vilisikika kila mahali, familia zaidi ya kumi zilikuwa hapo kuzika vitu mbalimbali vya marehemu kama ishara ya kuwazika marehemu ambao walikuwa hawajapatikana.
Yote haya yakitokea, Loveness alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi hospitalini Muhimbili, hajitambui na haelewi chochote kilichokuwa kikiendelea, maelezo ya madaktari yalionyesha alikuwa akiendelea vizuri na angeweza kurejewa na fahamu zake, jambo pekee ambalo hawakuwa na uhakika nalo ni kama angeweza kuwa na akili timamu akipona.
Maelezo hayo yalimfurahisha sana mama yake ambaye muda wote alishinda nje ya chumba cha wagonjwa mahututi, akisubiri zamu ya kuingia ili akamwangalie mtoto wake kwani hakuruhusiwa kubaki kando ya kitanda. Ndugu wote walikuja na kuondoka wakimwacha hapo, mara nyingi akipiga magoti chini na kumwomba Mungu atende muujiza, wala hakuona aibu watu walipopita.
“Mama ingia!” muuguzi alifungua mlango na kumwambia.
“Asante, mwanangu anaendeleaje?”
“Vizuri mama.”
Akaingia ndani na kuvua viatu kisha kuvaa koti na viatu maalum ambavyo watu walioingia chumba cha wagonjwa mahututi walitakiwa kuvaa, haraka akatembea mpaka kwenye kitanda cha mtoto wake moyo ukimwenda mbio, siku zote alikuwa na hisia kwamba angeweza kuingia kwenye chumba hicho na kumkuta Loveness amesimama kupumua kwa jinsi hali yake ilivyokuwa mbaya, lakini alipambana na hisia hizo kwa sababu alishamwomba Mungu wake.
“Sista!”
“Bee mama!”
“Hebu njoo uone.”
“Kuna nini tena?” muuguzi aliuliza alipofika kitandani.
“Amefumbua macho na kutabasamu, nimeshangaa sana.”
“Mshukuru Mungu mama, mwanao atapona.”
Daktari aliitwa na kuja kumpima Loveness, akathibitisha kabisa kwamba mapigo yake ya moyo yalikuwa yamekaa vizuri na alikuwa akihema bila matatizo, akaagiza mashine ya kupumulia iondolewe kwa muda wa saa ishirini na nne ili aone kama angeweza kustahimili maisha bila mashine.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa, saa ishirini na nne zikapita, afya ya Loveness ikazidi kuimarika, tayari alikuwa na uwezo wa kuangalia huku na kule ndani ya chumba lakini bila kusema chochote. Alionekana kama mtu asiyetambua hata mahali alipokuwa na wapi na alikuwa akifanya nini.
“Mama kama nilivyokuambia, Loveness hatakuwa na uwezo wa kuongea na pia kumbukumbu zote za maisha yake amepoteza, kilichotokea ni kama vile kompyuta imefuta mafaili yote, hivyo ni lazima aanze kujifunza kila kitu upya, hata kuongea!”
“Hakuna tatizo daktari, ilimradi tu mwanangu awepo duniani.”
“Kama ana bahati yake, kumbukumbu kidogo zinaweza kurejea, lakini hii hutokea mara chache mno, mgonjwa mmoja kati ya wagonjwa milioni moja, hivyo hilo si jambo la kutarajia sana. Kikubwa ni kwamba mtoto wako hatimaye atapona kuruhusiwa kutoka hospitali.”
“Naamini huu ni mpango wa Mungu, hakutaka kabisa mwanangu akumbuke maumivu ya kufiwa mume na mwanaye mpendwa Melania.”
“Inawezekana!” daktari aliongea.
Wiki mbili zaidi baadaye, Loveness aliruhusiwa kutoka hospitali akiwa bado hana kumbukumbu yoyote ya maisha yake ya nyuma, zaidi ya kuelewa kilichokuwa kikiendelea tangu alipozinduka hospitalini, hata mama yake mzazi hakutambua kwamba ni mama yake.
Kilichokuwa kikifanyika nyumbani ni kumfundisha kuzungumza maneno kama vile ambavyo mtoto mdogo hufundishwa kutamka.
Siku zilivyozidi kwenda, Loveness alianzisha tabia ya kuwa analia sana kama mtu anayelilia kitu, tena kwa uchungu, hakuna aliyeelewa ni kwa nini kwani bado alikuwa hajawa na uwezo wa kujieleza. Alilia sana alipoiona picha ya mume na mtoto wake, jambo lililowafanya ndugu na jamaa waanze kuhisi fahamu zake zilikuwa zimeanza kurejea, walipozungumza na daktari juu ya hilo aliwathibitishia kwamba kidogokidogo alikuwa ameanza kukumbuka matukio. ya nyuma.
***
Hakuelewa alifikaje mahali alipokuwa fahamu zilipomrejea, lakini alikuwa juu ya mti akining’inia kwenye tawi, amekalia kiti cha ndege na mkanda ukiwa umembana sawasawa. Akavuta kumbukumbu zake na kukumbuka namna ndege ilivyokuwa ikishuka kwa kasi kubwa kuelekea chini, baba yake akiwa amemkumbatia na akiomba kwa Mungu awanusuru, baadaye hakuelewa kilichoendelea mpaka alipojikuta juu ya mti huo.
Chini yake kulikuwa na mabaki ya kitu alichokifananisha na ndege, kikiwa kimekunjika na kubakiza sehemu ya nyuma ikiwa imeangalia juu angani! Kulikuwa na harufu kali iliyozikera pua zake, miili ya watu waliolala chini wengine wakiwa wamekatika viungo ilionekana chini yake. Akaelewa ndege waliyokuwa wakisafiri nayo ilianguka mahali hapo na kubaki kipande kidogo.
“Baba! Baba!” aliita bila kuitikiwa.
Kulikuwa na milio mingi ya ndege kila upande, akaelewa ilikuwa ni asubuhi ingawa mwanga wa jua ulikuwa umezuiliwa na miti mirefu ya misitu. Hakuelewa mahali hapo ni wapi, lakini ulikuwa ni msitu mzito na mnene ambao hakujua mwanzo wala mwisho wake. Hofu kubwa ikamwingia moyoni, alipomfikiria mama yake, Melania akazidi kulia.
“Baba! Baba!” akaendelea kuita bila kuitikiwa.
Sababu ya kujitingisha, alishangaa kuona anaporomoka kutoka mtini na kwenda kutua ardhini kwenye mwili wa mtu aliyekuwa amelala, mtu huyo akatoa mlio kuonyesha alikuwa ameumizwa na kiti cha ndege kilichomgandamiza. Melania akafungua mkanda kama alivyofundishwa na wazazi wake na kusimama, mwili wake ulikuwa imara, ukiwa bila mchubuko hata mmoja.
“Mh!” aliguna macho yake yalipotua juu ya mtu aliyemgandamiza na kiti, alikuwa ni baba yake, katika hali ya kutojitambua.
Nisingependa kumaliza hadithi hii ya leo bila kukumbusha jambo muhimu la kutoa maisha yako kwa Mungu. Maisha tuliyonayo hapa duniani ni mafupi sana, yanapita kama maua yachanuavyo na kunyauka. Wengi unaowafahamu wamekufa lakini wewe unapumua, ni vyema basi kufikiria maisha baada ya kifo.
Kila siku jiulize: “Hivi nikifa leo nitakwenda jehanam au peponi?” Kila mmoja wetu analo jibu lake, bila shaka sote tungependa kwenda peponi. Kama hivyo ndivyo, basi tiketi ya kwenda huko ni matendo mema na kujiepusha na uovu.
Tukumbuke mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele.
Je, nini kitaendelea?

Post a Comment