MAKUNDI 50 YAWASILISHA MAJINA YA WAJUMBE
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
WAKATI leo ndiyo siku ya mwisho Ikulu kupokea
mapendekezo ya majina kutoka kwa makundi mbalimbali, tayari makundi
yapatayo 50 yamewasilisha mapendekezo ya majina ya watu ambao wangependa
wawe wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Makundi hayo ni asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya Serikali, vyama
vya kitaaluma, madhehebu ya dini na vyama vya siasa ambayo jumla
yanafanya idadi hiyo kuwa 50 na inatarajiwa kuongezeka leo kutokana na
makundi mengine kuwasilisha majina leo.
Taarifa iliyotolewa juzi Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue ilieleza kuwa taasisi hizo zimewasilisha majina yao
kwa mujibu wa mwaliko uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete ili kukidhi
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Sheria hiyo sura ya 83 Kifungu cha 22(1) (c) cha Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba kinataka makundi kupendekeza majina na kuyawasilisha kwa Rais
ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kufanya uteuzi wa wajumbe wa Bunge la
Katiba.
Taarifa hiyo ilifafanua, kuwa makundi hayo 50 yaliyowasilisha majina
yanayopendekezwa yanatokana na barua 169 zilizopokewa na Ofisi ya Katibu
Mkuu Kiongozi na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya
Mapinduzi, Zanzibar.
Makundi ambayo yamewasilisha majina kwa mujibu wa taarifa hiyo ni
Shirika la Wasaidizi wa Jamii Kabila la Wagogo, Tanzania Association of
Social Workers (TASOWA), Jukwaa la Walimu na Wanafunzi Tanzania, Chama
cha Walimu Wanawake Tanzania, Umoja wa Wanawake Wajane wa Wilaya ya
Karagwe na Kyerwa (UWK).
Mengine ni Tanzania Peace and Development Society, Better World
Organization (BWO), Youth Focus and Development, Association of
Traditional Medicine Man, Registered Centre for Good Governance and
Development in Tanzania, Chama Cha Kijamii (CCK), CHANETA na Muungano wa
Wanajeshi Wastaafu Tanzania.
Makundi mengine ni Legal Aid Iringa Village, Tanzania Kilolo Orphans
and Social Development Organization, Legal Aid and Social Welfare
Association, Legal and Human Right Centre, Tanzania Lift Initiative NGO,
Kilolo Paralegal Unit, Women Development and Social Activities
Association, Defence of Human Right/Citizen Rights. Pia kuna makundi ya
DAWSEN Trust Fund, Baruti Development Association (BADEA), Living Hope
Ministries Trust, EFATHA Ministry, Bethel Assemblies of God Tanzania,
Muslim and Christian Brotherhood Society, Baraza Kuu la Waislamu wa
Kondoa – Tanzania na Jesus Temple Inner Transformation News.
Zingine ni Jumuiya ya Waithna Asharriyyah Tanzania, Rehmatfi
Sabilillah Trust of Tanzania, Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA),
National Reconstruction Alliance (NRA), Sauti ya Umma (SAU), Chama cha
Demokrasia Makini, African Progressive Part – APPT Maendeleo, National
League for Democracy, Tanzania Film Federation, Taasisi ya Maendeleo ya
Utamaduni, Al-Amoud General Enterprises.
Taarifa hiyo ilitaja makundi mengine kuwa ni Blue Belt and Water
Sources Control, Community
Development Training Institute – Tengeru,
Tanzania Medical Student Association, Tanzania Sea Farmers Union,
Medical Association of Tanzania, Chama cha Wastaafu wa Mbinga, Union of
Tanzania Press Clubs, Umoja wa Wanawake Tanzania, Alliance for Tanzania
Farmers Party na Tanzania Social Economic and Environment and Wellbeing.
Taarifa ya Ikulu ilisema kwa vile mwisho wa kupokea orodha ya majina
hayo ni leo, Balozi Sefue alitoa mwito kwa makundi mengine ambayo
hayajawasilisha orodha hiyo kufanya hivyo kabla muda uliowekwa kwisha.
Aidha, taarifa hiyo ilitaka makundi hayo kuwa wakati wa kuwasilisha
majina hayo ni muhimu kuzingatia vigezo vilivyowekwa na sheria na kama
vilivyofafanuliwa kwenye Tangazo la Serikali Namba 443 lililochapishwa
Desemba 13, mwaka jana.
Wakati anatoa salamu zake za Mwaka Mpya kwa Taifa juzi, Rais Kikwete
alisema mchakato wa kupata wajumbe 201 watakaoungana na wabunge na
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunda Bunge Maalumu la Katiba umeanza.
Alisema ni matarajio yake kuwa katika wiki ya tatu ya mwezi huu,
uteuzi utakamilika. Siku 21 baada ya hapo Bunge la Katiba litaanza. Hii
ni kwa nia ya kuwapa nafasi wajumbe hao kusoma Rasimu ya Katiba.
Chadema leo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema
kitawasilisha mapendekezo yao ya majina leo baada ya kupokea maombi
mengi kutoka kanda zote 10 zinazohusisha mikoa, wilaya na majimbo.
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, John
Mnyika ilieleza kuwa baada ya Ikulu kutoa tangazo la kutaka makundi
kuwasilisha majina hayo, chama hicho kilitoa mwito kwa wanachama wake
ambao wangependa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba kuwakilisha
CHADEMA, watume maombi makao makuu ya chama na katika ngazi nyingine
husika.
“Maombi yamekuja mengi kutoka kanda zote 10 za chama zinazohusisha
mikoa, wilaya na majimbo nchini. Sekretariati ya chama, jana ilianza
vikao vya kupitia majina hayo, kazi inaendelea tena leo (jana)", ilisema
taarifa hiyo.Mnyika alisema baada ya uchambuzi huo, chama kitawasilisha majina hayo kama matakwa ya sheria na tangazo la Rais yanavyohitaji.
CREDIT: HABARI LEO
Post a Comment