Mwenyekiti CHADEMA Arusha asimamishwa kwa usaliti.
BARAZA la uongozi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Kanda ya Kaskazini limemsimamisha uongozi Mwenyekiti wake wa
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kwa tuhuma za kukisaliti chama hicho.
Uamuzi huo umefikiwa juzi katika kikao cha dharura cha baraza hilo
baada ya mwenyekiti huyo akiwa ndani ya kikao kutuma ujumbe katika
mtandao wa kijamii unaolenga kuwachonganisha viongozi na wanachama wa
chama hicho.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana juu ya uamuzi huo,
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni mbunge wa
Karatu, Mchungaji Israeli Natse, alisema wameamua kuchukua uamuzi huo
mgumu kutokana na tuhuma zinazomkabili Mwigamba na kuhitaji uchunguzi
wa kina.
Natse alisema kuwa Mwigamba ametenda kosa hilo kupitia taarifa yake
aliyotuma kupitia mtandao huo kwa jina la ‘Kwanini mabadiliko CHADEMA
ni lazima’ na kusema kuwa viongozi wa chama wamechakachua katiba ili
kuendelea kubaki madarakani.
Alitaja tuhuma hizo kuwa ni za usaliti, uzushi, uzandiki na
uchonganishi kwa viongozi, ambazo zinahitaji uchunguzi makini, na hivyo
kulazimu kumsimamisha wakati uchunguzi huo ukiendelea.
Kwa makosa hayo amekiuka Katiba ya CHADEMA sura ya 10 kuanzia kifungu
cha 8, 9 na 10 ambavyo vinamzuia kiongozi kuchafua viongozi wenzake na
wanachama kwa ujumla.
Alisema licha ya CHADEMA kuendesha uchunguzi, lakini pia uongozi wa
Kanda ya Kaskazini ulimfikisha Mwigamba polisi kwa kutumia mtandao wa
kijamii kukichafua chama hicho na viongozi wake ambapo ni kosa
kisheria.
Naye Katibu wa CHADEMA wa kanda hiyo, Amani Golugwa, alisema baada ya
kufikia uamuzi huo wanaandaa barua rasmi kumkabidhi Mwigamba,
ikimaanisha kuwa amepoteza sifa ya kuingia katika vikao vyote
alivyokuwa akiingia kupitia wadhifa wake wa uenyekiti.
“Tutakapomkabidhi barua inamaanisha kuwa anapoteza sifa ya kuingia
katika vikao vya Baraza la Kanda kama mjumbe, vikao vya Baraza Kuu
Taifa, Mkutano Mkuu Taifa na vingine vyote vya mkoa alivyokuwa
akihudhuria kwa wadhifa wake wa uenyekiti,’’ alisema.
Kuhusu kumfikisha polisi, Golugwa alisema licha ya kumshitaki kwa
tuhuma zinazomkabili, lakini ilikuwa ni kwa usalama wake kwa sababu
chama kina wanachama wengi na kila mmoja ana hisia zake binafsi juu ya
chama, hivyo ingeweza kuhatarisha usalama wake.
“Mimi kama katibu ambaye nimefanya kazi kwa karibu na Mwigamba akiwa
mwenyekiti wangu wa mkoa, suala hili limeniumiza sana kwa kuwa
sikutegemea kama angeweza kufanya alivyofanya,’’ alisema.
Alisema wakiwa katika kikao, walishangaa kuona ujumbe ukiingia katika
mtandao wa kijamii na kushtushwa, hatua iliyowalazimu kufuatilia ili
kumbaini aliyeutuma.
“Haikuwa rahisi kwake kukubali kuhusika kutuma ujumbe huo, na alitaka
kuzua vurugu kikaoni, lakini baada ya kutakiwa kukabidhisha kompyuta
mpakato ‘laptop’ na ilipokaguliwa kitaalamu na kupata uthibitisho ndipo
alipobaki ameshangaa na kukiri kutenda kosa hilo,’’ alisema.
Aidha, tuhuma nyingine zilizotajwa ni kitendo chake cha kuwatuhumu
mwenyekiti wa taifa na maofisa wengine wa chama kutumia fedha nyingi
kuzunguka na kufanya vitu visivyo na msingi.
“Baada ya kutafakari hayo yote, chama kimeona hakiwezi kuendelea
kuishi na mayai viza ama kulea mizoga kwa kuwa tunaamini amedanganywa
na watu ambao hawalitakii mema taifa hili,” alisema Golugwa.

Post a Comment