Wanne wauawa na polisi kwa kuvamia benki Mbagala
Polisi wakiimarisha ulinzi kwenye benki hiyo iliyovamia na wanaosadikiwa kuwa majambazi Mbagala, Dar.
WATU wanaosadikiwa
kuwa majambazi na ambao idadi yao inasadikiwa kuwa sita wakiwa na
mabomu na bunduki za kisasa jana walivamia Benki ya Access
tawi la Mbagala jijini Dar es Salaam ambako walipora viroba vya
fedha, kuua mlinzi na baadaye wanne kati wakauawa na polisi.
Watu walioshuhudia tukio hilo
walisema baada ya watu hao kufika katika benki hiyo kwa
bodaboda nne majira ya saa nane mchana, walimuua mlinzi wa
benki hiyo, kisha kubomoa kwa risasi mlango wa vioo na kuingia
ndani na kuzua taharuki kubwa ndani ya benki hiyo.
Mmoja wa majambazi hao baada ya kuuawa.
Mashuhuda hao walisema, katika
tukio hilo lililodumu kwa karibu saa moja, mmoja wa majambazi
hao aliyekuwa amevaa kininja, alikuwa barabarani akiamuru magari
kupita haraka huku akifyatua risasi hovyo.
Ilielezwa kuwa jambazi huyo
aliyeonekana kuwa na uzoefu wa matumizi ya bunduki alikuwa
akifyatua risasi kwa kutumia mkono mmoja na ndiye aliyewajeruhi
baadhi ya wapita njia.
Majambazi wawili kati ya wanne waliouawa wakiwa katika gari la polisi.
Wakati uporaji ukiendelea na
jambazi huyo akiimarisha ulinzi barabarani baadaye hakukuwa na
magari wala pikipiki zilizokuwa zikipita.
Mfanyabiashara wa duka la vifaa
vya ujenzi jirani na benki hiyo, Ramadhani Tairo, alisema baada
ya jambazi huyo kuliona gari la polisi likielekea eneo la
tukio, alifyatua risasi na kulipiga kabla halijafika. Gari hilo
lilipoteza mwelekeo na kutumbukia mtaroni.
Tairo alisema mbali na jambazi
huyo kulipiga risasi gari la polisi pia alilirushia bomu la
mkono, lakini liliangukia barabarani bila kulipuka. Polisi
walifanikiwa kulifyatua bomu hilo baadaye likiwa halijasababisha
madhara kwa wananchi waliofika kushuhudia tukio hilo.
Mkazi mwingine wa eneo hilo,
Rebecca Maliva, alisema majambazi walioingia ndani ya benki
hiyo walionekana wakitoka na viroba vitatu vya fedha ambavyo
walivipakata kwenye pikipiki na kuondoka kwa kasi kuelekea
Mkuranga kupitia barabara ya Kilwa.
Rebecca alisema polisi zaidi
walifika kwenye eneo hilo wengine wakiwa kwenye pikipiki na
kuanza kuwafukuza majambazi hao ambapo walipofika eneo la shule
ya St. Mary’s, walitupa kiroba kimoja cha fedha ambacho
wananchi waliokuwa jirani waligombania na kuchukua fedha
zilizokuwemo na kisha kila mmoja kukimbia na bulungutu la
noti.
Baada ya nusu saa wakati umati
ukiwa bado upo kwenye benki hiyo, magari ya polisi yalipita
katika eneo hilo yakitokea eneo la Mkuranga yakiwa yamebeba
miili ya majambazi waliouawa.
Magari hayo yalikuwa yakisindikizwa na vijana wa bodaboda waliokuwa wakishangilia kazi iliyofanywa na polisi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam, Simon Sirro, alizungumzia kwa ufupi tukio hilo
akasema majambazi wanne wameuawa na kukamata silaha tatu, lakini
hakutaka kuingia kwa ndani zaidi akisema atatoa taarifa baadaye.
(HABARI NA ‘MWANANCHI’)

Post a Comment