Sumaye amshangaa JK
SIKU mbili baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa kauli ya kuhofia
chama chake kuondoka madarakani iwapo rushwa itashindwa kutokomezwa,
Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amemtaka kiongozi huyo kuchukua
hatua.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili jana, Sumaye alisema kuwa wala
rushwa wanajulikana, lakini wameshindwa kuchukuliwa hatua.
Sumaye alisema kuwa anashukuru Rais Kikwete kubaini tatizo hilo na
kumshauri kwenda mbali zaidi, ikiwa ni pamoja na kulifanyia kazi na
kuwachukulia hatua watu hao.
“Kama rais naye amegundua hilo, basi ni vizuri zaidi, ayafanyie kazi
hayo. Msimamo wangu unajulikana, nimeshalalamika sana kuhusu rushwa,
najua rushwa inakwamisha maendeleo, tuchukie rushwa, tutafute nafuu ya
maisha kwa Watanzania wote, sio nafuu ya mtu mmoja mmoja,” alisema.
Alipoulizwa na gazeti hili kama anawajua wala rushwa na hatua ambazo
anamshauri rais achukue, Sumaye alisema kuwa watu hao wanajulikana na
wameshawahi kuandikwa, hivyo hana haja ya kuwataja.
“Wanajulikana, kama na ninyi mmeshawaandika basi wanajulikana, sina haja ya kuwataja,” alisema.
Waziri Mkuu huyo mstaafu, mwaka jana alilalamikia rushwa baada ya
kuenguliwa katika kuwania ujumbe wa NEC katika Wilaya ya Hanang ambako
Mary Nagu aliibuka kidedea.
Siku za hivi karibuni, Sumaye alikaririwa akisema wanaokerwa na
karipio lake kuhusu rushwa, wanapaswa kuachana na vitendo hivyo viovu.
Sumaye, alitoa karipio hilo kwa viongozi wa dini, hususani ndani ya
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), akionya kuhusu kasi ya
wanasiasa kutumika katika harambee zake.
Alikaririwa akisema miongoni mwa wanasiasa hao, wanatumia mwanya huo
kama njia ya kuungwa mkono watakapotangaza kuwania urais katika
uchaguzi mkuu ujao.
Ingawa hakuwataja wanasiasa hao kwa majina, kauli yake ilitafsiriwa
kumgusa aliyekuwa mrithi wake, Edward Lowassa, ambaye baadaye
alijiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond.
Lowassa, mbunge wa Monduli, ameshiriki harambee mbalimbali nchini,
hali inayoelezwa na baadhi ya wachunguzi wa mambo ya siasa kuwa na
lengo la kujisafishia njia kuelekea katika kinyang’anyiro cha urais wa
2015.
Lakini Lowassa amekanusha kushiriki harambee hizo kwa nia ya kutafuta
urais, badala yake akasisitiza kwamba ana karama ya ushawishi
inayomfanya afanikishe shughuli hizo kwa kupata fedha nyingi.
Naye aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Wiliam Ngeleja, alisema
anamuunga mkono Rais Kikwete kwa kuwa rushwa imeumiza taifa, imepoteza
rasilimali nyingi, na ufisadi mkubwa umepitia hatua iliyosababisha
maendeleo kurudi nyuma.
“Suala la rushwa linaaibisha taifa letu, tusilitazame kama suala la
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, tulitazame kama suala la
Watanzania wote, tuchukie rushwa, rushwa itazamwe kwa mapana yake, na
kila Mtanzania ajue madhara ya rushwa, hapa ndiyo tutasaidia taifa,”
alisema.
Alisema kuwa kama rushwa itaendelea kushamiri, haki za wananchi
zitaminywa, huduma za muhimu hazitapatikana kwa njia ya haki, hivyo
wananchi wataendelea kuteseka na kukosa huduma hali ambayo inasababisha
watu kuichukia CCM na serikali yake.
Ngeleja alisema kuwa anamuunga mkono Rais Kikwete kwa kauli yake, na
kuwataka Watanzania wazidishe mapambano dhidi ya rushwa, na wenye
ushahidi kwa watuhumiwa wa rushwa wajitokeze ili kuisaidia Takukuru
ifanye kazi yake ipasavyo.
Aidha, mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel
Lwaitama alisema Rais Kikwete anaonekana sasa kuwa na nia nzuri na
taifa, hivyo alimuomba Mungu amsamehe makosa ya zamani, kwa kuwa
msimamo wake wa sasa unaitesa CCM.
“Kauli ya Kikwete ya sasa imenifanya nifikirie uamuzi wa kuendelea
kulipia kadi yangu ya CCM, kwani niliacha tangu 2005, baada ya kuona
chama kinaendeshwa kwa rushwa.
Mimi ninampongeza kwanza kwa kukiri yale
ambayo yalitufanya tuache kulipia kadi, sasa tunamhimiza afikirie
zawadi ya MO Ibrahim, asimamie upatikanaji wa katiba mpya kwa njia ya
haki na kusikiliza maoni ya wapinzani, atusaidie kusimamia uchaguzi wa
mwaka 2015 bila rushwa, hayo yataandika historia nzuri ya jina lake na
atakumbukwa kwa msimamo huu,” alisema.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA

Post a Comment