Makinda: Wabunge waliotemwa wamepigika ..Adai wanakwenda ofisini kwake kuombaomba.
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amesema kuwa kutokana na hali ngumu
ya kiuchumi inayowakabili wabunge wanapomaliza vipindi vyao, ofisi yake
imelazimika kutoa mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kumudu maisha.
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda.
Makinda alitoa kauli hiyo jana wakati akibadilishana mawazo na Spika
wa Bunge la Uswisi, Maya Graf ambaye yupo nchini kwa mapumziko mafupi na
familia yake.
Alisema kuwa kwa kipindi alichokaa katika kiti cha uspika, amebaini matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wabunge waliostaafu.
Makinda alisema kuwa wabunge wengi wamekuwa wakiathirika kiuchumi
pindi wanapotoka katika nafasi hiyo, hivyo mafunzo yatawawezesha kuwa na
shughuli za kufanya, na kwamba yatatolewa kwa wabunge wote.
Alisema kuwa ni muhimu wabunge wakaichukulia siasa kuwa sio kazi ya
kudumu ili wanaposhindwa kuchaguliwa, wafanye shughuli nyingine za
kuwaingizia kipato.
“Hata ukiangalia magomvi yanayotokea wakati wa uchaguzi, wengi
wasiokubali matokeo ni wale ambao hawana shughuli za kufanya,” alisema.
Spika Makinda alisema kuwa kwa wabunge ambao wana shughuli za kufanya,
kwao ubunge unakuwa sio tatizo kwa kuwa wana uwezo wa kuendesha maisha
yao.
Alisema tangu ashike nafasi hiyo, wabunge wengi walioshindwa uchaguzi
wamekuwa wakifika ofisini kwake na kuomba msaada wa kifedha wakati ofisi
hiyo haina fungu la wastaafu hao.
“Kuna siku nilikuwa ofisini walikuja wabunge wastaafu zaidi ya watano
wakiomba msaada, ikanilazimu nitoe akiba yangu nikawasaidia baadhi,
lakini wale ambao hawakupata chochote walinung’unika sana,” alisema.
Makinda alisema kuwa kabla ya mwaka 1995, Bunge liliweka utaratibu wa
pensheni kwa wabunge wastaafu, lakini uliondolewa na anachopata sasa
mbunge ni posho ya kumaliza vipindi vyake vya ubunge.
Alisema kuwa na hiyo inatokana na mishahara midogo wanayopata wabunge ukilinganisha na mabunge mengine.
“Hata ukiangalia fedha unayopata, unatakiwa kuigawa na nyingine
kupeleka jimboni, nyingine wengine wanatumia wakati wa uchaguzi jambo
linalofanya mbunge akikosa kuchaguliwa akose la kufanya,” alisema.
Naye Graf, alisema kuwa wabunge wa nchi yao hawana shida pale
wanaposhindwa kuchaguliwa kwa kuwa wana uwezo wa kupata kazi nyingine,
na ajira sio tatizo.
CHANZO TANZANIA DAIMA

Post a Comment