Mfanyabiashara adai kuibiwa mil. 700/-
MFANYABIASHARA wa madini ya tanzanite, Pendaeli Mollel,
ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuingilia kati ili aweze kupata
fedha zake zaidi ya sh milioni 700 alizodai zimepotea baada ya kuziweka
kwenye akaunti zake katika Benki ya Exim tawi la Arusha.
Mollel aliwasilisha malalamiko hayo kwenye Idara ya Usimamizi wa
Mabenki ya BoT, kupitia mwanasheria wake, Omar Iddi Omar, wa Kampuni ya
Law Bridge ya jijini hapa, Julai 26 mwaka huu, akitaka imsaidie namna ya
kupata fedha hizo.
Omar alidai kuwa katika kipindi cha miezi minne, mteja wake aligundua
upotevu wa fedha katika akaunti zake tatu ambazo ni 5789633006,
5792261005 na 5789633334.
Alisema moja ya akaunti hizo ilikuwa ya dola za Marekani na nyingine ya fedha za Tanzania.
“Kama unavyoona, mteja wetu ameshuhudia upotevu huo katika akaunti
hizo unaofikia dola za Kimarekani 361,722 pamoja na sh 225,000,000.
“Kiasi hicho ni kikubwa, na kwa ujumla kinamletea usumbufu, mfadhaiko
na hali ngumu kwa biashara zake na familia yake ikizingatiwa yeye ni
mfanyabiashara ndogo na ambaye anategemea fedha hizo katika mzunguko wa
biashara yake,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Wakili Omar alisema kuwa hadi sasa mustakabali wa mteja wake uko
shakani baada ya benki hiyo kukataa ombi lao la kutaka kulipatia
ufumbuzi tatizo hilo kutokana na kukaa kimya bila kujibu barua yao
waliyowapelekea Juni 6, mwaka huu.
“Tumeona ni vema kuomba uingiliaji kati wa idara yako adhimu tukiamini
wewe ndiye msimamizi wa mabenki yote hapa nchini kisheria na mwenye
mamlaka ya kuhakikisha mabenki yanatimiza wajibu wao wa kutoa huduma
sahihi na zenye ubora kwa wateja,” iliongeza barua hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima, Mollel alisema kuwa aliamua kupeleka
malalamiko yake BoT akiamini kuwa taasisi hiyo ya fedha itachukua
hatua stahiki ingawa hadi sasa ni miezi miwili imepita bado hajapata
majibu ya kuridhisha.
Alisema kuwa fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti zake kwa njia
tofauti ikiwemo kwa kuhamisha hundi pamoja na utoaji katika mashine za
fedha (ATM).
“Nashangaa taarifa za benki zinaoyesha kuwa nimetoa au kufanya malipo
kwa hundi na mashine za ATM wakati benki hiyo haikuwahi kunipa hundi
yoyote au kadi ya ATM na mara zote naweka na kutoa fedha kwa kujaza
fomu maalumu ya kutolea fedha.
“Nimeshitushwa kuona kuwa nimefanya malipo kwa njia ya hundi ya dola
50,000 kwa mfanyabiashara mmoja wa Arusha (jina linahifadhiwa) ambaye
hata simfahamu wala hatukuwahi kufanya biashara ya aina yoyote, lakini
pia sikuwahi kupewa kitabu cha hundi,” alisema Mollel.
Akizungumzia madai ya mfanyabiashara huyo, Mkurugenzi wa Idara ya
Usimamizi wa Mabenki wa BoT, Kened Nyoni alikiri kupokea barua hiyo ya
Mollel akilalamikia benki ya Exim na kupotea kwa fedha zake.
Wakili wa Exim Bank, Albert Msando alikiri kupokea barua za malalamiko
ya Mollel na kwamba alizijibu huku akisema kuwa baada ya kupitia
vielelezo vya karatasi ya kuweka fedha hizo benki (bank-in slip) pamoja
na taarifa za benki (bank statement) walizoambatanisha, alibaini kuwa
zina upungufu mkubwa.
Alisema kuwa mapungufu hayo hayawezi kujadilika nje ya mahakama kwa
kile alichoeleza kuwa baadhi ya makaratasi hayo ya kuweka fedha yalikuwa
hayajaandikwa namba ya akaunti, huku mengine yakiwa hayajasainiwa,
hivyo akasema kuwa ni vema suala hilo likapatiwa ufumbuzi mahakamani.
Suala hili limeibuka huku kukiwa na shauri jingine la jinai kwenye
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha la kula njama na kuiba zaidi ya sh
bilioni 7 linalowakabili wafanyakazi 14 wa benki hiyo akiwemo meneja wa
tawi la Arusha, Bimal Gondalia.
Katika shauri hilo la jinai namba 309 la mwaka huu, washitakiwa hao
ambao ni wafanyakazi wa Benki ya Exim tawi la Arusha, walisomewa shitaka
la kula njama na kuiba zaidi ya sh bilioni 7 sanjari na kuiibia benki
hiyo, fedha za Marekani dola 400,000 katika kipindi cha miaka mitatu.
HABARI NA TANZANIA DAIMA
Post a Comment