ad

ad

Yanga yailiza Rhino, Simba yakaa kileleni

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, jana walivuna ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku tatu tu tangu watoke sare ya mabao 3-3 na mtani wao Simba.

Wakati Yanga wakivuna ushindi huo hivyo kupoza machungu ya sare ya Jumapili, ambapo licha ya wakali hao wa Jangwani kuwa mbele kwa mabao matatu, hadi mapumziko, Simba ilifanikiwa kusawazisha yote katika kipindi cha pili.

Kwa ushindi huo, Yanga wamefikisha pointi 19 huku mtani wao Simba ambaye jana alitoka sare ya bila kufungana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, akifikisha pointi 20, hivyo kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Katika Uwanja wa Taifa, Yanga walipata bao la kwanza dakika ya 15, likifungwa na nyota wake wa kimataifa, Hamis Kiiza, aliyefunga mabao mawili dhidi ya Simba, akimalizia pasi ya Simon Msuva.

Bao hilo lilionekana kuongeza kasi ya mchezo kwa kila moja kufanya mashambulizi na kama nyota wa Yanga wangekuwa makini wangeweza kupata mabao zaidi lakini hadi mapumziko walikuwa mbele kwa bao hilo moja.

Kipindi cha pili, Rhino walikianza kwa kasi huku mabeki wa Yanga wakiwa imara kuonkoa hatari zote katika lango lao ambalo lilikuwa likilindwa na kipa Deogratius Munish ‘Dida’ huku Rhino wakifanya mabadiliko kadha kwa kumtoa Iman Ndely na kumwingiza Msafiri Hamisi.

Dakika ya 73, Yanga walipata bao la pili likifungwa na Frank Domayo aliyemalizia kazi nzuri ya kiufundi iliyokuwa imefanywa na Ngasa aliyewahadaa mabeki wa Rhino kabla ya kutoa pasi ya uhakika ambayo ilitendewa haki.

Bao hilo lilizidi kupata nguvu Yanga ambao walizidi kupanga mashambulizi na Kiiza kurejea tena katika nyavu za Rhino na kufunga bao la pili kwake na la tatu kwa timu yake, akimalizia kazi nzuri iliyokuwa imefanywa na Ngasa.

Hadi filimbi ya mwisho, Yanga wakatoka uwanjani na ushindi huo mnono wakifikisha pointi 19, nyuma ya Simba, Azam na Mbeya City zenye pointi 20 kila moja.

Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, David Luhende, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Rajab Zahir, Simon Msuva, Frank Domayo, Hamis Kiiza, Mrisho Ngasa na Haruna Niyonzima.

Rhino Rangers: Mohamed Othman, Ally Mwanyiro, Julius Masoga, Ladislaus Mbogo, Stanslaus Mwakitosi, Shija Mongo, Iman Ndely, Victor Hangaya, Saad Kipanga na Nurdin Bakar.

Kutoka Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, Mwandishi Wetu, Kenneth Ngelesi, anaripoti kuwa Tanzania Prisons jana walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Kagera Sugar.

Kagera Sugar walitangulia kupata bao dakika ya 58, likifungwa na Themi Felix kabla ya Ernest Mwalupaji wa Kagera Sugar kujifunga katika harakati za kuokoa.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea kutimua vumbi kesho katika viwanja mbalimbali.
Powered by Blogger.