KUSALITIWA, KUACHWA NI KUBAYA,WAJIBIKA KAMA MWANAMKE.
Tunakutana tena kupitia ukurasa huu ambao ni namba moja kwa
kuandika makala nzuri zinazogusa maisha yako ya kimapenzi. Ukiwa
unaufuatilia kila wiki, mapenzi hayawezi kukutesa kama yanavyowatesa
wengine.
Utajua mbinu bora za kumpata mwenza sahihi lakini pia jinsi ya kuishi
naye kwa raha mustarehe na kamwe asifikirie kukusaliti wala kukuacha.
Mpenzi msomaji wangu, leo nataka kuzungumza na wanawake walio kwenye
ndoa lakini pia si vibaya na wale wanaotarajia kuingia kwenye maisha
hayo wakasoma.
Ndugu zangu, vilio vya baadhi ya wanawake kuibiwa waume zao na
kuachwa vimekuwa vikiongezeka kila kukicha lakini nimebaini kitu kimoja.
Wengi wanakutwa na janga hili kwa kushindwa kutimiza wajibu wao kama
wanawake, wanalilia kuolewa na wakibahatika kuingia kwenye maisha hayo
wanajisahau na kubweteka.
Kimsingi mwanamke anayemjali mpenzi wake ndiye anayetimiza wajibu
wake, lakini wengi hujikuta wakitoswa na wapenzi wao kutokana na ufahamu
mdogo ama dharau ya mambo madogomadogo.
Ni busara kutambua kuwa uhusiano hauna mambo ‘simpo’. Kila kitu kina
umuhimu mkubwa kulingana na nafasi yake sambamba na utekelezaji wako.
Mwanaume hata siku moja harogwi kwa limbwata la sangoma, mahaba
yaliyoshiba peke yake yanatosha kumfanya awe hapindui kwako. ‘Ukimhendo’
kwa kiwango kitakachomridhisha, hatowaza kukuacha. Unawezaje? Jibu ni
rahisi, muoneshe unampenda na thibitisha kwa vitendo.
Daima hili liwe akilini mwako, mwanamke kupitia mapenzi yake ana
uwezo mkubwa mno, lakini lazima awe anajua kutimiza wajibu wake kwenye
uhusiano.
Kama mpenzi wako anakuacha, ujue kuwa umeshindwa kuchukua nafasi yako
kama mwanamke na kuna mambo unayomkosea. Unyenyekevu kwa wanawake wa
kisasa kimekuwa ni kitu adimu, kiasi ambacho kinahatarisha uhusiano wa
watu wengi.
Wanaume wanawapenda wanawake ambao hujionesha waziwazi kuwa wenyewe
ni wasaidizi wao wakuu katika masuala mbalimbali hivyo anza leo kutimiza
wajibu wako.
Hii ni moja ya mbinu za kumdatisha mwenzi wako na ninachotaka ukijue
ni kwamba, wengi wamefanikiwa na ndiyo hao ambao leo hii wanazifurahia
ndoa zao na kujihisi wako peponi.
Lakini kitu kingine ambacho nahisi unatakiwa kukijua ni kwamba, mke
wa mtu au mwanamke yeyote aliye kwenye uhusiano anatakiwa kuwa mjanja.
Hii ni kwa sababu wanaume wengi wanapenda kuwa na watu wa dizaini hii.
Sababu ya wanaume kuwapenda wanawake wajanja ni kukwepa aibu wanazoweza kuzipata pindi watakapokuwa kwenye uhusiano na washamba.
Wanaume wengi huogopa kujiingiza katika mapenzi na watu wasiokuwa na
uelewa mpana wa mambo ambao kutokana na tongotongo za ufahamu, hujikuta
wakiwa mafundi wa kuiga mambo ya hatari.
Washamba mara nyingi huwa ni malimbukeni, hujifunza mambo yasiyokuwa
na faida kwa imani kwamba naye ataonekana mtu kati ya watu. Wanawake wa
aina hii ni rahisi kuwaingiza wenzi wao katika hasara kubwa. Hawakawii
kuiba, ni rahisi kuharibu vitu, wao ni wabadhilifu na wanaopenda makuu!
Wanawake malimbukeni huharibika katika vikao vya ususi, kutokana na sifa
kubwa ya umbeya kwenye sehemu hizo. Wanaume wasiokuwa na subira
hujikuta wakiwapiga teke wenzi wao mara tu wanapoanza kuhisi nyendo
zisizoeleweka.
Tumekuwa tukishuhudia wanawake malimbukeni wakiiga tabia za ulevi wa
pombe au mihadarati kutoka kwa marafiki zao. Wengine hubadilika na
kufikia hatua ya kuwa mafuska waliokubuhu huku wakiwapanga mabwana kila
kona.
Mwanamke mjanja hawezi kuiga hovyo hovyo, siku zote anajua kitu cha
kuanzia na kinachofuata. Hawadanganyiki kwa penzi la pesa, wanaelewa
malipo yake ni makubwa. Ndiyo maana wanaume wanawapenda!
Nawe kama unataka kupendwa zaidi kuwa mjanja, lakini zaidi ya yote
chukua nafasi yako kama mwanamke kisha timiza wajibu wako. Majibu yake
utayaona.
Credit: GLP

Post a Comment