Babi, Humud, Dida watemwa Azam FC.
PAMOJA na Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall kuwahi kutamka kuwa
hakuna mchezaji atakayeachwa kwenye kikosi chake, uongozi umeachana na
nyota wawili baada ya mikataba yao kwisha na kuwapandisha watatu wa
kikosi cha pili.
Baada ya kwisha kwa Ligi Kuu ya Bara Mei 18, Stewart alidokeza kuwa
hana mpango wa kumtema mchezaji wala kuongeza kutokana na timu yake
kusheheni nyota wengi wenye uwezo mkubwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo yenye
maskani yake Chamazi, nje kidogo ya Dar es Salaam, Nassor Idrisa
aliwataja waliotemwa ni pamoja na kipa Deogratius Munish ‘Dida.’
Alisema baada ya Dida kumaliza mkataba wake wa mwaka mmoja, wameamua kuachana naye na tayari yaelezwa amejiunga na Yanga.
Nassor alisema nyota wengine waliotemwa, ni Abdi Kassim ‘Babi,’
Abdulahim Humud aliyetimkia nje ya nchi, Zahor Pazi aliyejiunga
na Simba na Uhuru Selemani aliyekwenda Coastal Union ya Tanga.
Idrisa alisema nyota waliopandishwa kutoka kikosi cha pili kwa ajili
ya kuziba nafasi hizo, ni Aish Manula, Hamadi Kadebi na Yustus
Achimpate.
“Dida na Babi na wengine tumeachana baada ya kwisha kwa mikataba yao
kwa vile tunao vijana wa kuziba nafasi. Tunasikia Dida amejiunga na
Yanga… tunamtakia mafanikio,” alisema Idrisa.
Kuhusu kambi, alisema wamepanga kwenda nje ya nchi kujiandaa kwa Ligi
Kuu itakayoanza Agosti, hawajui ni lini hasa kutokana na nyota wao
kadhaa kuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Stars chini ya kocha wake Kim Poulsen, itaingia kambini Julai 3,
kujiandaa na mechi dhidi ya Uganda katika vita ya kuwania tiketi ya
kucheza fainali za Afrika kwa nyota wa Ligi za Ndani (CHAN).
Hata hivyo, alisema wachezaji wameanza kujifua kwa Ligi Kuu kwani
baada ya kumaliza nafasi ya pili mara mbili mfululizo, kilichobaki sasa
ni kutwa ubingwa.
Alisema hawatasajili wachezaji zaidi ya hao kuelekea Ligi Kuu,
isipokuwa kwenye dirisha dogo na kuongeza kuwamfikirii kipa Juma Kaseja
aliyeachwa na Simba.

Post a Comment