Yafahamu malalamiko ya watoto dhidi ya wazazi - 1.
TUMEZOEA mara nyingi kuona wazazi wakilalamika kuhusu watoto
wao. Malalamiko ya wazazi yanahusu mambo mengi kuhusu tabia za watoto
wao. Inaweza kuwa ni maisha ya nyumbani, vyakula, marafiki au masuala
ya shuleni.
Ni mara chache sana wazazi wamekuwa wakikaa na kufikiria
jinsi watoto wao wanavyowafikiria wao.
Wazazi wengi tunaona kwa kuwa jukumu la kulea na kumpatia mahitaji
mtoto ni la kwetu, basi yeye (mtoto) ni mtu wa kusikiliza tu na kufuata
maelekezo na maagizo anayopewa.
Kutokana na kuendekeza hali hiyo, imetokea mara nyingi sana watoto,
hasa walio katika umri wa vijana wakawa na malalamiko mengi kuhusu
wazazi wao.
Mbaya zaidi ni kuwa vijana hawa, mara nyingi wanakuwa hawana fursa ya
kuelezea malalamiko na manung’uniko yao kuhusu wazazi kwa sababu
hawapewi fursa hiyo.
Kama unataka kazi yako ya malezi iwe rahisi, jenga tabia ya kuwapa
fursa watoto nao kueleza mawazo yao. Na si usikilize tu, bali hakikisha
pia kuwa mawazo yanayopaswa kufanyiwa kazi unayafanyia kazi.
Tunachosisitiza hapa ni kuwa mtoto naye anapaswa kupewa fursa ya kueleza mawazo yake katika suala la malezi.
Ili kuifanya kazi yako ya malezi kuwa rahisi, jitahidi kumsikiliza
pia mtoto. Na unapomsikiliza uwe unachunguza anataka kueleza nini
ambalo anadhani kuwa unalifanya visivyo. Kwa namna hiyo, utafahamu
malalamiko yake dhidi yako.
Lakini ili kuwasaidia wazazi, wataalamu wa masuala ya malezi
wamefanya utafiti na kubaini mambo makuu kumi ambayo watoto wengi
wanayalalamikia kuhusu wazazi wao.
Tutayachambua mambo haya hapa kwa jumla ili kuwapa wazazi picha ya nini hasa watoto wengi wanafikiria kuhusu wao.
Mosi, watoto wengi hawafurahishwi na tabia ya mzazi kuwasiliana na
walimu wake moja kwa moja bila kwanza kumfahamisha yeye kuwa anafanya
hivyo.
Na ni kweli wazazi wengi wana tabia hii. Lakini kama mzazi ambaye
unapenda mtoto wako awe na maendeleo shuleni, haifai kufanya mambo kwa
kumficha hasa kama jambo lenyewe linamhusu moja kwa moja.
Hakuna madhara yoyote ya kumweleza mtoto kuwa utawasiliana na walimu wake kuhusiana na jambo fulani.
Hali hiyo itokee tu pale ambapo mtoto hapaswi kulifahamu jambo lenyewe linalohusika.
Pili, watoto wengi hawapendi wazazi kuanza kutangaza kwa watu wengine
mambo ambayo wao waliwaambia kwa sharti kuwa asimwambie mtu mwingine.
Mtoto anapenda mambo anayoyasema sirini kwa mzazi wake yabaki sirini.
Kutoa siri zake kunamfanya mtoto amwone mzazi kuwa si mwaminifu. Na
kukosa uaminifu kwa mtoto kunaweza kumfanya asiwe muwazi anapozungumza
na wewe.
Akishajua kuwa ni mtu ambaye hatunzi ahadi zake mtoto hatakuwa huru kukueleza kila kitu kinachomhusu.
Unatakiwa kuwa msiri wa mtoto wako ili awe anakimbilia kwako na
kueleza kila jambo ambalo linamtatiza. Akishabaini kuwa wewe hautunzi
siri basi akiwa na tatizo ambalo anadhani kuwa anapaswa kulizungumza na
msiri wake, hatakuja kwako, atatafuta mtu mwingine wa kuwa msiri wake.
Je, wewe kama mzazi utafurahi iwapo mtoto wako atakuwa anazungumza mambo yake nyeti kwa watu wengine na kukuficha wewe?
Tatu, watoto wengi hawapendi mambo yao, hasa yale wanayoamini kuwa ni nyeti, yazungumzwe bila ya wao wenyewe kuwepo.
Kuzungumzia mambo yake wakati yeye mwenyewe hayupo anaweza kuona kuwa ni umbeya.
Ni vema kila suala linalomhusu mtoto linapozungumzwa basi na yeye
mwenyewe awepo. Kama hayupo, basi apewe taarifa kabla kuwa suala lake
litazungumzwa na ni nani na nani watahusika katika mazungumzo hayo.
Na pia, kama itashindikana kumpatia taarifa kabla suala
halijazungumzwa, ni vema kuwa mara fursa itakapopatikana mtoto
afahamishwe kuwa kulikuwa na mazungumzo kumhusu yeye na yalihusu jambo
gani mahsusi.
Kufanya hivyo kutatoa fursa na yeye kutoa mawazo yake kuhusiana na suala hilo.
Nne, si kila mara mtoto anapenda kukusikia ukimsifia, hasa unapoongea
na watu wengine. Kuna watu kwa kawaida wanapenda sifa. Lakini kuna
wengine ambao hawapendi sifa, hasa zile za kupakana mafuta kwa mgongo
wa chupa.
Kumbuka lakini hata kama mtoto hapendi kusifiwa, ni lazima mzazi umsifie pale anapostahili kusifiwa.
Lakini usiwe unamsifia eti tu kwa sababu mpo pamoja na marafiki au
watu wengine. Mtoto asifiwe kwa jambo alilolifanya ambalo linastahili
sifa kweli.
Kumpatia sifa ambazo hastahili, hasa zinapotolewa mbele ya watu
wengine ambao hawaifahamu hali halisi, kunaweza kumfanya mtoto ajione
kana kwamba anadharauliwa mbele ya watu.

Post a Comment