Nauli hizi bila nyongeza ya mshahara ni sawa?
NAWAAPIA sasa mtajiju. Wakati ule mliwacheka wenzenu wa Kigamboni walipoambiwa kama hawajui kuogelea imekula kwao siyo eh?
Sasa mtashangaa wale wanaotoka Songea kuja Bongo Dar es Salaam kama
nao watapiga mbizi kama kijana wangu Magufuli alivyowataka watu wa
Kigamboni wafanye walipolalamika maji yamezidi unga kwenye kivuko cha
Feri.
Narudia tena huko simo msije mkaninukuu vibaya watu wangu. Nani angependa kung’olewa meno bila ganzi? Huko simo kabisa.
Sasa si mmesikia hili sekeseke la nauli mpya? Kwa mtaji huu wapo watu
wataamua kuomba waache wenyewe kazi kwa hiari kwa manufaa ya miili
yao.
Ni wangapi watamudu kutembea kwa miguu toka Mbagala hadi Sitesenta
kusaka mia? Na ukiamua kukwea motokaa basi ujue kazi yako unaifanya ili
upate nauli ya kwenda na kurudi kazini.
Wacha tu nikubaliane na wale wanaosema kama kweli uchumi wa taifa
letu umekua basi ni namba kwenye makaratasi tu lakini sio kwenye waleti
zetu sisi wavuja jasho.
Wacha niweke pozi kidogo hapa kabla sijajitoa mzima mzima. Ila kwa mtaji huu lazima tutajiju.
Hivi mlipoongeza hizo nauli mna mpango gani na mishahara yetu? Mbona
tulidhani mngeanza kuongeza mishahara ndipo mje kwenye hilo la nauli?
Au kwa mahesabu yenu mwaona gharama zimekwenda juu kwa wamiliki wa
motokaa tu siyo eh? Niambie wamiliki wao wakikutana na kukoroma
mnawasikiliza, niambieni sisi wafanyakazi wengine tufanye nini?
Tukigoma si mnakimbilia pale Mahakama ya Kazi na kupata stopu oda
upesi upesi? Tumeliona hilo kwa walimu na madaktari, mnadhani tuna cha
kujiuliza wakati huu?
Kula yenyewe ni shida sasa na nauli ya kwenda kutafuta hicho kibaba
nayo mshaifanya iwe ishu watu wangu. Ila jambo moja ninalofahamu ni
kwamba aliyeshiba hamjui mwenye njaa ng’o!
Sasa kama mmepandisha hizo nauli, mmejaribu pia kuangalia ubora na
usalama wa huo usafiri? Najua wakubwa hamjui adha za usafiri wa umma
hasa daladala. Nauliza mmejipanga baada ya kuwapa wamiliki kapu la
kuchuma sasa nao wajue wana wajibu kwa walipa nauli?
Hatuwezi kula mlo mmoja kwa siku ili tupate vijisenti vya kudandia
daladala halafu bado ukiingiga huko ukutane na kero. Yale mambo ya
levo siti yalikufa siku Mwaibula alipowaachia Sumatra usukani siyo eh?
Hilo huwa hamlioni jamani? Kwamba gari ya watu ishirini inabeba watu arobaini kwenu hilo sio tatizo kabisa naona.
Na gari hilo linakutana na wale manesi wa barabarani wala hakuna
kinachotokea, utadhani ni haki ya kikatiba kujaza gari hadi watu wakose
pa kukanyaga. Wacha tu nijitoe kimya kimya nikipiga mluzi wangu.
Nasema huko simo kabisa.
Na kwenye magari mnayosema ya kwenda mikoani kwani hamjui kuna
mengine yanakuwa na abiria watu na abiria mifugo humo humo utadhani
kwenu mtu si afya? Tembeeni mjionee.
Kuna mikoa kusafiri na gari huku mbuzi na kuku wakiwa sehemu ya
abiria wala sio jambo la kushangaza kwao. Nyie mmeshupalia nauli tu
siyo eh?
Au hamjui kuna mabasi yanapakia mabati na mazagazaga mengine humo
humo na abiria?
Hamjawahi kujiuliza kwa nini ajali zetu vifio vinakuwa
vingi?
Endeleeni tu maana naona Afrika mmeamua sheria zimewekwa ili
zivunjwe, mnashtuka tu maafa yakitokea. Ukibisha hili nitakupa mfano wa
wanaojenga maghorofa kupitiliza idadi iliyo kwenye vibali vyao.
Mnadhani ghorofa isipoanguka kuna atakayemchukulia hatua? Na hapo
bado wanishangaa nikisema yaelekea huku kwetu sheria zimewekwa ili
zivunjwe?
Wacha tu ninyamaze maana machozi yangu mtoto wa mama yako karibu sana.
Ukiacha haya ya kujaza abiria na kupakia mifugo au bidhaa nyingine
hatari kwa usalama bado hamjui kwamba wapo madereva wengi wanaendesha
hasa daladala wakiwa wamevuta sigara kubwa?
Msiniulize mimi sigara kubwa ila namaanisha ile sigara isiyokuwa ya
kawaida ambayo kaka’angu Ndugai ana wasiwasi kuna wabunge wanaichoma
kisawasawa!
Huko simo nisije kuambiwa ninawakejeli wahishimiwa sana wanaoendelea
kupata zile posho za kukaa kitako huko wanakokuita makao makuu ya
nchi. Mimi wacha nikae kimya lakini nijitoe mwanawani.
Kiukweli kabisa ukiona namna hawa waendesha daladala au kule kwetu
kwa wakina Kibaki na Uhuru na Raila tunaita Matatuu wanavyoendesha
bila kuhofia ajali utapinga kabisa hawavuti sigara kubwa?
Kwenye hili mmejipanga vipi isije ikawa kazi yenu ni kuruhusu
mifuko ya wamiliki itune kwa unono wa nauli, lakini walipaji uhai wao
mmeamua kuuweka rehani?
Na hata kwenye haya magari ya safari ndefu kuna wambea wanasema
madereva wengi hupenda kutafuna miraa. Nasema haya nimeyasikia kwa
wambea msije kuniambia nitoe ushahidi hiyo ni tipu tu nimewapa mfanye
wenyewe upelelezi kama ni trafiki au Sumatra huko simo kabisaaaa!
Hata baada ya kupandisha nauli bado mnasema elimu ni bure? Si mmesema
mtoto atalipa nusu ya mtu mzima ambayo nauli ya chini kabisa kwa tripu
moja ni shilingi mia mbili?
Hivi nyie mnajua umaskini wa watu wetu au vitambi vinawazuia msione
mbele? Nauliza kwa dhati kabisa kwa kiwango hiki ni watoto wangapi hasa
kwenye miji mikubwa wataweza kwenda na kurudi shule?
Itaanza hadithi ya kwenda kwa miguu wanafika wamechoka halafu
wakimaliza shule na kufeli mnaunda tume! Hivi maskini sasa hivi ana
raha gani tena ndugu yangu?
Na ole wenu mseme wavizie lifti. Siwaambii kitakachotokea hadi muende kwanza mkasimuliwe hadithi za Sodoma na Gomora.
Kwa dunia ya leo nani anathubutu kumwacha mwanae apewe lifti na hii
mibaba ambayo hujui nani ni nani? Hamjui siku hizi kuna mijitu
inaonekana kwa nje ina heshima zao na wengine hawakosi nyumba za ibada
kumbe ni mibazazi isiyokuwa na utu?
Kama hujanielewa shauri yako ila mwenyewe najiondokea taratibu bila kutia neno.
Hili niliseme taratibu tena kimya kimya. Kuna porojo eti imeundwa
kamati kuchunguza nauli mpya. Nasema kama hii ni kweli basi Watanzania
tutafute aliyetuloga.
Tulipoanzisha Sumatra tulikuwa tumevuta ile nanihii au tumekunywa
pombe haramu? Narudia tena wacha tu niombe kusiwepo na hiyo tume au
kamati au kamisheni maana nitakuwa siwaelewi.
Zamani walikuwa wakisema kufa hatufi ila cha moto tutakiona, sasa kwa
mtaji huu nina wasiwasi kama tutamudu kubakia kuona hicho cha moto.
Wajanja washajaza nafasi zote za kula kwa mikono miwili sasa
wanatuchekishia tu wakisubiri muda ufike waje tena watudanganye
tuendelee kudanganyika kama kawaida yetu wao waendelee kula kama
kawaida yao.
Narudia tena kwa sauti kubwa simo tena simo kwenye hayo yote.

Post a Comment