Mbunge ahoji wananchi kuzuiwa kuvua samaki
JIBU LA SWALI LA MBUNGE Bukoba vijijini
MBUNGE wa Bukoba Vijijini, Josson Rweikiza (CCM), amehoji mpango
wa serikali wa kuwazuia wananchi kuvua samaki katika Ziwa Victoria na
kusema kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuwanyima haki.
Rweikiza alihoji mpango huo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la
msingi, alihoji kwa nini serikali isiwaruhusu wananchi kuvua samaki
katika maeneo mengine au kwa wakati usiokuwa wa mazalio ya samaki.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Benedict ole Nangoro, alikanusha taarifa hiyo na kusema wananchi
wanaoishi kandokando mwa Ziwa Victoria hawajawahi kuzuiwa kuvua samaki
wa kitoweo wala wa biashara, bali wamehimizwa kuzingatia uvuvi endelevu
kwa mujibu wa sheria ya taifa ya uvuvi ya mwaka 1997.
Pia alisema kanuni husika zinazosimamiwa na serikali zimeainisha aina
ya zana zinazoruhusiwa kutumika kuvua aina mbalimbali za samaki.
Alifafanua kuwa kanuni Na. 58(1)(b) inakataza kuvua, kushusha,
kumiliki, kusafirisha nje ya nchi au kufanya biashara ya sato wenye
urefu chini ya sentimenta 25.
Aidha, alisema kanuni ya 66(1)(k) inakataza kumiliki, kutumia na
kusababisha mtu kutumia kwa uvuvi wa dagaa nyavu zenye macho chini ya
milimita nane.
Naibu Waziri huyo alisema serikali inawahimiza wananchi kutumia zana halali kama sheria na kanuni za uvuvi zinavyoelekeza.

Post a Comment