HIV: KWANINI UPIME? (Faida za Kupima HIV.)
Daktari siko tayari kupima labda mpaka mwakani;Hapana doctor heri nife
kuliko kupima HIV.Hayo ni baadhi ya majibu unayopata unapomshauri
mgonjwa kupima HIV. Kuna sababu nyingi zinazowafanya wagonjwa kutokuwa
tayari kupima maambukizi ya VVU. Mojawapo ni woga kwani kwa watu wengi
kuwa na maambukizi ya VVU ni sawa na kifo. Sababu nyingine ni baadhi ya
wagonjwa kuamini kuwa baadhi ya watoa huduma wamekuwa na tabia ya kutoa
siri za wagonjwa kwa watu wasiohusika.
Hata hivyo ukiweka hizo sababu kando,kuna faida kubwa za kuweza
kukusukuma kufanya maamuzi ya kupima leo. Afya njema ni jukumu la kila
mmoja wetu na hivyo tunawajibu wa kutunza na kujua hali za afya zetu.
Zifuatazo ni faida za kupima HIV.
Kujua hali ya afya.
Ni vizuri ukipima HIV kwani ndio njia pekee ya kujua kama una maambukizi
au laa. Watu wanaonekana kuwa wazima kabisa wanaweza kuwa wanavirusi
vya UKIMWI katika miili yao. Ukiitambua hali ya afya yako utachukua
hatua sahihi kulingana na hali uliyonayo .
Kumkinga mwenziwako na wengine
Baada ya kupima HIV na kujua hali yako ya afya itakusaidia kumkinga
mwenziwako pamoja na wengine mlionao katika mahusiano. Ni wajibu wako
kuhakikisha kuwa ulionao katika mahusiano hawapati maambukizi. Ni vyema
ukiwalinda hasa kwa kutumia kondomu.
Kujikinga usipate maambukizi mapya
Iwapo utachukua jukumu la kupima itakusaidia kujikinga usipate
maambukizi mapya. Kama utakuwa una VVU,maambukizi mapya yatachochea
kuzaliwa kwa aina nyingine(strain) ya virusi ambayo inaweza kuwa sugu au
kushambulia kinga kwa haraka zaidi
Kuanza matibabu mapema
Huwezi kuanza matibabu kama hujui hali yako. Tafiti mbalimbali
zimeonesha faida za kuwahi kuanza matibabu. Hii itasaidia kupunguza
hatari ya kupata magonjwa nyemelezi.
Hivyo basi ni vyema kuamua na kuchukua hatua leo ya kupima. Kuna vituo mbalimbali vinavyotoa huduma ya ushauri na kupima.
Habari na www.paulmasua.com

Post a Comment