Stars uso kwa uso na Ethiopia
TAIFA Stars inatarajiwa kujipima nguvu dhidi ya wenzao wa
Ethiopia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaochezwa Januari 11
mjini Adis Ababa.
Katika kujiandaa na mchezo huo, Stars inaingia
kambini kesho, alisema Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Boniface Wambura.
Ethiopia inajiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakayoanza Januari 19 nchini Afrika Kusini ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1982.
Nchi hiyo ya pembezoni mwa Bara la Afrika, iko
Kundi C pamoja na mabingwa watetezi Zambia, Nigeria na Burkina Faso.
Ethiopia itacheza mechi yake ya kwanza Januari 21 dhidi ya Zambia.
Wambura alisema mazungumzo yanaendelea kuhusu wachezaji wa Yanga na Simba waliozuiwa na timu zao kujiunga na Stars.
Aidha Wambura alikanusha madai kuwa klabu hizo hazikupewa taarifa mapema.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Sunday
Kayuni ameondoka jana kwenda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kuzungumza na uongozi klabu ya TP Mzembe ambako wanacheza washambuliaji
wa kimataifa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Kayuni anakwenda huko ili kujua ukweli wa tatizo na kufanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo ili kutatua utata unaojitokeza kila wachezaji hao wanapoitwa.
Wambura aliwataja wachezaji wanaotakiwa kambini kuwa ni, Makipa: Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula na Mwadini Ally (Azam).
Walinzi: Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar),
Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).Viungo: Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji: John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Post a Comment