Mchezaji soka wa Scotland atiwa mbaroni kwa tuhuma za kuiba ndani ya 'supermarket'
Leigh Griffiths mshambuliaji machachari na mtambo wa kupachika
mabao wa klabu ya soka ya Hibernian nchini Scotland ametiwa mbaroni
baada ya kupatikana akiiba kwenye duka la Tesco mjini Edinburgh.
Griffiths alitiwa mbaroni na walinzi wa duka hilo.
Polisi ya Scotland imethibitisha juu ya kutokea tukio hilo la kutiwa
mbaroni mshambuliaji wa klabu ya Hibernian mwenye umri wa miaka 22. Hata
hivyo Polisi imeeleza kuwa, Leigh atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma
hizo katika siku zijazo. Polisi imeeleza kwamba uongozi wa klabu yake
umeshapewa taarifa juu ya tukio la mchezaji wao, ingawa wamesema kwamba
suala hilo liko mikononi mwa polisi.
Griffiths ambaye alichukuliwa kwa mkopo kutoka klabu ya Wolverhampton
Wanderers tayari ameshaipachikia timu yake mabao 15. Mchezaji huyo
alianza kuvaa jezi ya timu ya taifa ya Scotland mwaka jana wakati
iliposhuka dimbani dhidi ya Luxembourg mwaka jana.

Post a Comment