Azam yaipumulia Yanga
WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho
(CAF), Azam FC, wamezidi kuwapumulia vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga,
baada ya kuichapa Toto African ya Mwanza mabao 3-1 kwenye Uwanja wa
Chamazi Complex jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Azam walioshuka dimbani mara 15 wamefikisha pointi 30
nyuma ya mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga, wenye pointi
32 ndani ya mechi 14.
Katika mchezo wa jana, Azam FC, ndio waliokuwa wa kwanza kutikisa
nyavu za Toto, kupitia kwa mshambuliaji machachari, Brian Umony, kipindi
cha kwanza kabla ya Humphrey Mieno kuongeza la piliHadi mwamuzi Judith
Gamba kutoka jijini Arusha anapuliza filimbi kuashiria mapumziko, Azam
walitoka vifua mbele kwa mabao hayo mawili.
Kipindi cha pili, kilianza kwa kasi huku Azam wakiingia na nguvu zaidi
na kufanikiwa kupachika bao la tatu likifungwa na Mieno tena, kabla ya
Selemani Kibuta kuifungia Toto bao la kufutia machozi.
Mchezo huo pia ulishuhudiwa na Kocha Mkuu wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ Kim Poulsen.
Kikosi cha Azam FC: Mwadini Ally, Malika Ndeule, Samih Haji Nuhu,
David John Mwantika, Jockins Atuddo, Kipre Bolou, Brian Umony, Salum
Abubakar, Abdi Kassim, Humhrey Mieno/Mwaikimba na Khamis Mcha/Seif
Karihe.
Toto Africans: Nelson Kimati, Erick Muliro, Robert Mmagadula, Erick
Kyaluzi, Evarist Maganga, Peter Mutabuzi, Severine Costantine, Donald
Obimma, Ulugbe Chika, Kheri Mohamed na Mohamed jingo.
Katika mchezo mwingine uliopigwa dimba la Sheikh Amri Abeid jijini
Arusha, wenyeji JKT Oljoro waliendeleza makali yao baada ya kuichapa
Kagera Sugar mabao 2-0Mabao ya washindi yalifungwa na Paulo Nonga na Idd
Swaleh.

Post a Comment