ad

ad

Walianza Kama Utani... Sasa Wanapeta



WALIOSEMA wa mwisho atakuwa wa kwanza na wa kwanza atakuwa wa mwisho hawakukosea kwani katika dunia tunayoishi wapo watu walikuwa na maisha ya kifahari lakini kwa sasa wanaishi maisha ya kawaida au ya dhiki sana lakini pia wapo waliokuwa hawana chochote, yaani walikuwa maskini wa kutupwa lakini sasa wanaishi maisha mazuri ya kifahari.

 Katika ulimwengu wa mastaa, vivyo hivyo kuna wasanii waliokuwa maarufu kila kona kutokana na kazi zao iwe amefanya filamu moja au wimbo mmoja tu kwenye muziki lakini baada ya muda wakajikuta wakishuka na umaarufu wao kupotea kabisa, lakini pia wapo wengine wanaanza kazi ya sanaa kimzahamzaha lakini wanajikuta wakitoboa. 
 amberlulu
Katika makala hii tunakuletea baadhi ya warembo ambao walianza muziki kama utani lakini kwa sasa ndiyo habari ya mjini
kutokana na kazi zao kufanya vizuri kwenye redio na tv.

GIGY MONEY Jina lake halisi alilopewa na wazazi wake ni Gift Stanford lakini kwa mashabiki ni maarufu kama Gigy Money, alianza kuuza sura kwenye video mbalimbali za wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva kama video queen. Akiwa huko aliingia kwenye muziki huo
kama utani akaanza kuimba ambapo alitoa singo yake ya kwanza inayokwenda kwa jina la Majojorijo ikaja ile iliyotambulika kwa jina la Supu zote hizo hazikuhit kivile, akavuta pumzi


lakini kwa hivi sasa kila kona mtaani wanamtaja kutokana na ngoma yake mpya ya Papa kutikisa na kufanya vizuri na watu wengi kuipenda. Mwanadada huyu alikiri kwamba kutokana na ngoma hiyo amekuwa akipata mwaliko wa shoo nyingi za mikoa mbalimbali jambo ambalo linamuongezea kipato na kuweza kuendesha maisha yake. 

LULU DIVA
 Kama ilivyokuwa kwa Gigy, Lulu Diva ambaye jina lake halisi ni  Lulu Abbas, awali alikuwa mhudumu wa hoteli akaamua kuingia kwenye ulimwengu wa sanaa ya muziki ambapo alianza kwa kuuza sura kwenye video mbalimbali za wanamuziki wa Bongo Fleva ikiwemo Naogopa ya Mirror
pamoja na remix ya Burger Movie Selfie ya Belle 9.

Mwanadada huyu hakuchukua muda mrefu sana kwenye u-video queen akaingia kimchezomchezo kwenye uimbaji wa Bongo Fleva ambapo alitoa ngoma ya kwanza iliyokwenda kwa jina la Milele akimshirikisha Barnaba, lakini haikufanya vizuri sana, baada ya hapo aliachia Utamu kisha Usimwache. Hivi sasa anatamba na Ngoma ya Give It To Me ambayo inapendwa na inapigwa sana kwenye vyombo vya habari na sehemu mbalimbali za burudani huku vijana wengi wa bodaboda na bajaj wakiisikiliza kwa sana. 

SNURA 
Mwanamuziki Snura Mushi kwa sasa ni staa anayetambulika vilivyo na kujikuta akiwafunika hata waliomtangulia kwenye fani hiyo.

 Mwanamama huyu alianzia kwenye sanaa ya filamu alipoona haimlipi kama alivyotaka akaingia kwenye muziki wa Mduara ambapo alianza kama utani na ngoma iliyoanza kumpa umaarufu ni Majanga, akaja na Shindu na nyinginezo kibao. Sasa hivi Snura anatamba na wimbo wake wa Zungusha ambapo anafanya shoo mbalimbali ndani  na nje ya nchi huku baadhi ya watu wakishangaa kutokana na mwanzo wake ulivyokuwa wa kiutaniutani. 

SHILOLE
Kama ilivyo kwa Snura, Zuwena Mohamed ‘Shishi Baby’ mwanamke mpiganaji kutokana na jinsi anavyopigana kufanya mambo mbalimbali ili tu atoke kimaisha alianzia kwenye filamu baadaye akafungua baa na duka baadaye akaamua kuachana navyo na kuingia kwenye muziki. Shilole amejikuta akiwa maarufu ndani na nje ya nchi kutokana na muziki wake aliouanza kama masihara tu ambapo anapata shoo nyingi kwenye nchi mbalimbali zikiwemo Marekani, Ujerumani na kwingineko. Mwanamama huyu ngoma zilizompa umaarufu sana ni ile ya Chuna Buzi, Malele na Say My Name aliomshirikisha Barnaba ambapo licha ya kufanya vizuri kwenye muziki huo pia anajishughulisha na kazi ya mama lishe ambapo amefungua ‘café’ yake maeneo ya Morocco jijini Dar. 

AMBER LULU 
Lulu Eugen ndiyo jina lake halisi japo wengi wanamfahamu kwa jina la Amber Lulu. Mwanadada huyu alipata umaarufu kupitia kuuza sura kwenye video mbalimbali za wanamuziki wa Bongo Fleva ambapo naye aliamua kujifunza kuimba na kuanza kazi hiyo. Amber Lulu alianza muziki kama mchezo lakini sasa hivi anajulikana zaidi kimuziki baada ya kufanya ngoma yake ya Watakoma aliyoshirikiana na Country Boy inayokwenda kwa jina la Watakoma. Kwa sasa anabamba na Ngoma ya Only You

No comments

Powered by Blogger.