Sheria ya Vyama vya Siasa kufanyiwa marekebisho: Mikutano ya hadhara kufutwa hadi wakati wa uchaguzi tu!
Rasimu ya Sheria ya Vyama vya Siasa inayotarajiwa kufanyiwa marekebisho kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, inapendekeza kufutwa kwa mikutano ya hadhara hadi wakati wa uchaguzi pekee.
Rasimu hiyo, ambayo imetumwa kwa vyama vya siasa kwa ajili ya kutoa maoni yao, pia inapendekeza ruzuku ilipwe mara moja na kwa vyama vyote kulingana na idadi ya kura za urais katika Uchaguzi Mkuu.
Iwapo mabadiliko hayo yatapelekwa bungeni, uwezekano wa kupitishwa kuwa sheria ni mkubwa kutokana na idadi kubwa ya wabunge kutoka chama tawala (CCM) kinachoongoza Serikali ambayo itawasilisha muswada wa mabadiliko hayo.
Rasimu hiyo imekuja wakati vyama vya upinzani vikipigia kelele kutoheshimiwa kwa Katiba na sheria na kuminywa kwa demokrasia iliyofanya vishindwe kupiga siasa kwa uhuru, hasa baada ya Serikali kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano.
Serikali imeruhusu mikutano ya ndani ambayo pia imesababisha viongozi kadhaa kukamatwa au kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupanga mikakati ya uchochezi.
Na tayari vyama vya upinzani vimeshaingiwa na hofu dhidi ya mapendekezo hayo, vikisema yanalenga kufuta sheria ya mwaka 1992, kwa mujibu wa viongozi waliozungumza na Mwananchi jana na juzi.
Katika Rasimu ya Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ambayo Mwananchi imeiona, Kifungu cha 45(2) kinaeleza kuwa mikutano ya vyama haitaruhusiwa katika kipindi ambacho hakuna uchaguzi, isipokuwa itakayoitishwa na wabunge, wawakilishi na madiwani katika maeneo yao.
Kuhusu ruzuku, rasimu ya muswada huo katika Kifungu cha 59 (1) inaeleza itatolewa mara moja katika mwaka wa fedha na waziri atazingatia hali ya kiuchumi na kifedha katika wakati husika.
“Sheria inayotungwa kwa kuangalia mtu au kundi la watu ni sheria mbaya,” alisema mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alipoulizwa maoni yake kuhusu mapendekezo hayo.
“Kinachofanyika sasa kinaturudisha miaka 25 nyuma. Uhuru alioupigania Mwalimu (Julius)Nyerere upo wapi? Uhuru wa kukusanyika, uhuru wa mawazo?”
Mbatia, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) alisema nchi inaendeshwa kwa matukio na kushauri kuwa maendeleo ya nchi ni lazima yawe shirikishi.
“Ajenda ya Malengo ya Milenia ya amani, haki na uimara wa taasisi unatoweka nchini,” alisema Mbatia, ambaye ni mbunge wa Vunjo.
“Zamani, mataifa ya nje yalikuwa yanakuja kujifunza siasa hapa kwetu, lakini kwa hali inavyoendelea sasa, watakuja kujifunza kitu gani? Tunapaswa kurejea katika mchakato wa Katiba ya Jaji Warioba, Katiba imara itatuondoa hapa tulipo na kwenda mbele zaidi.”
Serikali ilitangaza kupiga marufuku mikutano ya hadhara mwaka 2016, ikisema inataka watu wajikite kufanya kazi za maendeleo na kwamba yataruhusiwa mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Tamko hilo kwanza lilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, lakini alipoulizwa bungeni alisema ilihusu jimbo lake na baadaye likatolewa na Jeshi la Polisi wakati Chadema ilipotangaza mikutano ya hadhara ya kuishtaki Serikali, kabla ya Rais John Magufuli kuweka bayana wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma za polisi Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kwa wakati wote, vyama vya upinzani vimekuwa vikipinga marufuku hiyo kwa maelezo kuwa inapingana na Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotoa uhuru kwa watu kukusanyika na kuitishana kwa lengo la kujadili, kufanya mkutano au kupeleka ujumbe kwa jamii au Serikali kuhusu jambo lolote ilimradi wanafanya hivyo kwa amani.
“(Muswada huu) Umehalalisha makatazo ambayo hayakuwa kwa mujibu wa sheria na hasa tamko la kuzuia mikutano ya vyama vya siasa sasa yanawekwa kwenye sheria,” alisema mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema.
“Kama chama tutakaa kupitia kifungu kwa kifungu na kutoa msimamo kuhusu rasimu ya muswada huu.
“Muswada huu umeweka vifungu vingi ambavyo siasa sasa imefanywa kuwa kosa la jinai.”
Pamoja na vyama vya siasa, hasa vya upinzani kupinga mapendekezo hayo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameyatetea kuwa yametoka kwa wadau.
Akizungumza na Mwananchi juzi, Jaji Mutungi alisema mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu hiyo yametoka kwa wadau, akisema ndio waliowezesha kupatikana kwa rasimu hiyo.
“Yeyote mwenye hoja afike ofisini kwangu,” alisema Jaji Mutungi.
Katika Kifungu cha 47 cha mapendekezo hayo, vyama vya siasa vinazuiwa kuajiri, kusambaza, kuunda vikundi vya ulinzi au kuwa na muundo sawa na wa Jeshi la Polisi au chombo chochote cha ulinzi na usalama cha Serikali.
Chanzo: Mwananchi Online

Post a Comment