ad

ad

Dhana Ya Uchawi Katika Mapenzi

NI Ijumaa nyingine ninapokukaribisha msomaji wangu katika ukurasa wetu huu mzuri, lengo likiwa ni kujuzana, kuelimishana, kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Mada ya leo ni ngumu kama inavyojieleza hapo juu! 


Umewahi kuona mwanaume anateseka kwenye mapenzi, mkewe, mchumba wake au mpenzi wake anamfanyia kila aina ya vituko lakini hana kauli, anakuwa kama zezeta, hawezi kufanya chochote, hawezi hata kufumbua mdomo wake kuzungumza chochote, yeye kwake kila kitu ni sawa tu? 

Umewahi kusikia kuhusu hiki kinachoitwa limbwata? Kwamba mwanamke anamuendea kwa mganga mwanaume anayempenda na kumfunga akili, kwamba asiwe na kauli juu yake, atekeleze haraka kila anachoambiwa bila kuhoji chochote? Vipi kuhusu wanaume kulalamika kwamba wanawake zao wamewaendelea kwa waganga kwamba wakitaka kupiga ‘mechi za nje’ jogoo ashindwe kuwika kuashiria mapambazuko? Bila shaka kama haijakutokea wewe, umewahi kumuona mtu wako wa karibu akitokewa na mambo ya aina hii au akilalamikia kuhusu hali hii. Lakini si kwa wanaume tu, umewahi kumsikia mwanamke akilalamika kwamba mwanaume wake amemuendea kwa mganga ili asimtamani mwanaume mwingine awe anamuwaza yeye tu? 

Kwa wewe mwenzangu na mimi, uliyelelewa na kukulia kwenye maisha ya ‘Uswahilini’ utakuwa unanielewa kwa ufasaha ninachokimaanisha. Sitaki kupuuza imani ya mtu yeyote kwa sababu suala hili linagusa zaidi imani za watu. Utaonekana wa ajabu kusema hakuna uchawi kwenye mapenzi wakati mtaa wa tatu baba Yusuf kila siku ndiye mwenye kazi ya kuosha vyombo, kufua nguo, kupiga deki na kulea watoto wakati mkewe akishinda kwenye ngoma! Utaonekana pia wa ajabu kusema uchawi upo wakati jirani yako ni muumini safi wa dini asiyekosa kuhudhuria kwenye nyumba za ibada! Ndiyo maana nasisitiza sitaki kuingilia imani ya mtu yeyote, yule anayeamini kwamba ndumba zipo katika mapenzi, sawa! Na wewe unayeamini kwamba hazipo, pia sawa! Mara nyingi, mijadala inayogusa imani za watu fulani, huwa haifiki mwisho, kama mtu anaamini ndumba zipo, huwezi kumbadilisha, na kama mtu anaamini hazipo, pia huwezi kumbadilisha fikra. 

Kwa kuwa lengo la mada hii siyo kubishana, lazima tukubaliane katika kutokukubaliana! Mambo magumu si ndiyo? Tutaelewana tu. Kinachoitwa uchawi kwenye mapenzi ni nini? Labda mjadala wetu uanzie hapo. Ukisikia uchawi katika mapenzi unaelewa nini? Ni tunguli, hirizi na madawa anayopewa mtu kwa ajili ya kupumbazwa akili na mpenzi wake? Je, mwanaume anayemsikiliza na kumheshimu mkewe, anayemtimizia kila anachokitaka, anayemsaidia kazi za nyumbani, amerogwa au amepewa limbwata?

 Dalili za mtu aliyepewa limbwata ni zipi? Limbwata lenyewe ni nini? Ni dhahiri kwamba mtu anayeamini na ambaye haamini katika uchawi, wakianza kujiuliza maswali haya, wote watafikia katika jibu ambalo linafanana na hapo tutafikia muafaka. Je, mwanamke kumpenda mwanaume kiasi cha kushindwa kuachana naye hata kama anamfanyia mambo mabaya, ni ishara kwamba amemuendea kwa mganga? 

Je, kushindwa kucheza mechi za nje, ni dalili kwamba mkeo amekuendea kwa mganga? Mimi si mjuaji wa kila kitu, naamini na wewe msomaji wangu unajua mambo mengi kuhusu mada hii na ili tufikie muafaka mzuri, ni lazime tushirikishane kile tunachokijua kwa lengo la kuwasaidia wale wanaolalamika kwamba wamerogwa, wamepewa limbwata au wameendewa kwa waganga. Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii

No comments

Powered by Blogger.