Prettykind Sitaki Mwanaume Kijana, Wanasumbua
KAMA ilivyo ada ya safu hii ya Mpaka Home, huwa inatembelea maeneo tofautitofauti kuangalia jinsi mastaa wanavyoishi wakiwa nje ya kazi zao.
Leo tumetembelea maeneo ya Kijitonyama jijini Dar. Ni nyumbani kwa msanii wa filamu za Kibongo, Suzan Michael ‘Prettykind’ ambaye anaeleza jinsi anavyoishi na ratiba yake nzima ya kila siku, ungana naye;
MPAKA HOME: (inakaribishwa ndani) hongera kwa kuwa umepangilia chumba chako vizuri, unaishi na nani hapa?
PRETTYKIND: Asante, hapa ninaishi na mwanangu, yaani mtoto wa dada yangu.
MPAKA HOME: Vipi kuhusu mwenza wako, yuko wapi?
PRETTYKIND: Sina mwanaume, niko singo, japokuwa nimechoka kuishi hivi, ninatafuta wa kunioa.
MPAKA HOME: Wewe ni mrembo sana, ina maana hakuna wanaume wanaokutokea kimapenzi?
PRETTYKIND: Wananitokea wengi sana, ila ninawakataa kwa sababu wengi ni matapeli, wanataka ngono tu!
MPAKA HOME: Wewe unahitaji mwanaume wa aina gani kama wanaokuja unawakataa?
PRETTYKIND: Ninapenda mwanaume mwenye hofu ya Mungu, ambaye umri wake umeenda, yaani mkubwa, sitaki vijana maana wana utoto mwingi sana, tutasumbuana.
MPAKA HOME: Ratiba yako hapa nyumbani kwa siku inakuwaje?
PRETTYKIND: Nikiamka asubuhi huwa ninakaa kwanza kitandani kwa dakika tano, ninawaza cha kufanya kwa siku nzima. Baada ya hapo ninatandika kitanda. Ninafanya usafi ndani na nje ya chumba changu, ninaoga, ninakunywa chai ndiyo ninaanza ratiba nyingine za kutoka.
MPAKA HOME: Je, huwa unapika?
PRETTYKIND: Ndiyo, ninapika.
MPAKA HOME: Ni chakula gani unachokipenda hasa?
PRETTYKIND: Mimi ni Msukuma hivyo ninapenda sana wali mandondo (maharage) na chapati.
MPAKA HOME: Ninashukuru kwa ushirikiano.
PRETTYKIND: Karibu sana.
Post a Comment