ad

ad

Michirizi Ya Damu - 18 ....MWISHO MWISHO


Bado Fareed alikuwa akilia kwa maumivu makali, madaktari ambao walikuwa wakimwangalia hawakumgundua kama alikuwa Fareed, mwanaume aliyeua watu wengi kwa kuwalipua katika kituo cha treni.
Akafanyiwa vipimo na kugundulika kwamba alikuwa na kansa katika utumbo wake mkubwa.
Madaktari wakashangaa, hawakujua sababu iliyomfanya mtu huyo kupata tatizo hilo kubwa ambalo mara nyingi lilikuwa likiwapata watu wenye kula vitu vilivyokuwa na kemikali nyingi kupitiliza.
Walitaka kujua chanzo cha tatizo hilo, wakamwambia kwamba alitakiwa kuchunguzwa kwa ukaribu na kugundulika chanzo cha tatizo hilo ili wajue ni kwa namna gani wangeweza kumsaidia.
Uchunguzi ulifanyika kwa saa kadhaa na kugundua kwamba tatizo kubwa lilisababishwa na mapenzi ya jinsi moja aliyokuwa akiyafanya zamani. Kilichomletea matatizo ni mafuta ya vilainishi ambayo yalikuwa yakitumiwa na wanaume waliokuwa wakimuingilia kinyume na maumbile.
Mafuta yale vilainishi yalikuwa yakipenya moja kwa moja mpaka kwenye utumbo mkubwa na kuganda huko, utumbo ukaathiriwa na moja kwa moja kumletea tatizo ambalo lilisababisha utumbo huo kushambuliwa na virusi vilivyosababisha kansa.
Madaktari hawakutaka kumficha, walimwambia ukweli. Fareed alikuwa akilia, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama mchezo ule mchafu aliokuwa ameucheza kwa kipindi kirefu ndiyo ungemletea matatizo hayo.
Hakutaka kufa, hakutaka kuona akiondoka duniani na wakati kulikuwa na mambo mengi ya kufanya. Alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, alikuwa na pesa ambazo zilimfanya kuwa na maisha mazuri, leo hii, kwa mchezo uleule wa kufanya mapenzi na wanaume wenzake ukamletea matatizo makubwa kwa kupata kansa ya utumbo mkubwa ambao ndiyo uliunganishwa mpaka nyuma kulipopeleka haja kubwa.
Madaktari walihuzunika, walijua kwamba kwa lile lililokuwa likiendelea mwanaume huyo asingeweza kupona. Wakati wakiendelea kumuhudumia ndipo wakagundua kwamba mwanaume huyo ndiye yuleyule aliyekuwa akitafutwa na FBI kwa kosa la kulipua kituo cha treni na kuwaua mabilionea wawili.
Hawakutaka kumuonyeshea hali ya kugundua kilichokuwa kimetokea bali walichokifanya ni kumchoma sindano ya usingizi, alipolala, wakachukua simu na kuwapigia FBI na kuwaambia kwamba mtu aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba, walikuwa naye hospitalini hapo hivyo maofisa hao kuwaambia kwamba ndani ya dakika chache wangekuwa mahali hapo.
****
Fareed akayafumbua macho yake pale kitandani alipokuwa, alijikuta amezungukwa na watu waliokuwa na suti miilini mwao. Aliwashangaa, hakujua watu hao walikuwa wakifanya nini pale alipokuwa. Alipojaribu kuuinua mkono wake akakuta akiwa amepigwa pingu.
Thomson alikuwa na wenzake, nyuso zao zilikuwa kwenye tabasamu pana, kitendo cha kumpata kijana huyo kilimaanisha kwamba wangefanikiwa kujua mwanzo mpaka mwisho na sababu zilizomfanya kukishambulia kitu kile cha treni na kusababisha watu wengi kufariki dunia.
Hakuwajua watu hao, alijiuliza maswali mengi kwamba walikuwa wakifanya nini mahali pale lakini baada ya kuona vitambulisho vyao akagundua kwamba walikuwa ni maofisa wa FBI waliofika mahali pale kwa ajili ya kumkamata.
Moyo wake alikuwa na huzuni kubwa, hakujua kwamba maisha yake yangeishia kukamatwa na maofisa hao ambao mpaka muda huo hawakuzungumza kitu chochote kile.
Baada ya kumwangalia kwa sekunde kadhaa, wakawaambia madaktari kwamba walitakiwa kuondoka naye kwani kulikuwa na mambo mengi walitaka kumuhoji, mahojiano hayo yalitakiwa kufanyika sehemu maalumu na si hapo hospitali.
Hilo halikuwa tatizo, wakaruhusiwa na kuondoka naye. Ndani ya gari, Fareed alikuwa kimya, tumbo lake liliacha kuuma, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi kwa wakati huo.
Hawakuchukua muda mrefu, gari hilo likaingizwa ndani ya jumba moja kubwa, lilikuwa na bango kwa nje lililoandikwa Federal Bureau of Investigation (FBI). Liliposimama, wakateremka, wakamchukua na kuelekea naye ndani ya chumba kimoja ambacho kilikuwa na viti viwili, meza moja na pia kulikuwa na kioo kikubwa ambacho wewe haukuweza kumuona mtu wa upande wa pili lakini yeye alikuona vizuri tu.
Thomson ndiye aliyekuwa na wajibu wa kumuuliza Fareed maswali. Kwa jinsi alivyomwangalia, Fareed hakuonyesha dalili za kufanya matukio ya kigaidi, alionekana kuwa mtu mpole sana ambaye hakuwahi kuchinja hata kuku.
Thomson alimwanzia mbali na mwisho kabisa kumuuliza kuhusu kituo kile. Fareed hakutaka kuficha, alitaka kusimulia ukweli juu ya kila kitu kilichotokea.
Simulizi yake ilianza mbali kabisa, tangu alipokuwa ameanza mchezo wa kuingiliwa kimaumbile, alipokutana na Godfrey Kidatu mpaka siku ambayo alianza kujiuza nje ya nchi.
Thomson alikuwa kimya akimwangalia. Fareed hakutaka kuficha kitu chochote kile, alisimulia uchafu wote aliofanyiwa na mabilionea mpaka kufikia hatua ya kutaka kumuua. Alimwambia pia kuhusu magaidi waliokuwa wamemchukua na kumpa bomu na wakati hakuwa akitaka kwenda kufanya tukio lolote lile.
“Kwa nini ulikuwa unakimbia?” aliuliza Thomson.
“Nilikimbia kwa sababu niliacha bomu kule chooni. Sikutaka kufa kwa kuwa kulikuwa na kazi kubwa mbele yangu,” alijibu Fareed.
“Haukujua kama ulibeba bomu?”
“Sikujua! Nilitaka kuuliza lakini maneno yao yalinifanya kubaki kimya. Nilikwenda chooni ili nione kulikuwa na nini kwani begi lilikuwa na uzito usio wa kawaida,” alisema Fareed.
Alieleza kila kitu mpaka Bilionea Williams alivyotaka kumtumia kumuua Belleck. Mahojiano hayo yalichukua saa moja, akapelekwa katika chumba kimoja na kuambiwa kukaa huko.
Fareed alikuwa kimya ndani ya chumba hicho, alikaa katika pembe ya chumba kile, alionekana kuwa na mawazo tele lakini moyo wake ulifarijiwa na kile alichokuwa amekifanya. Alijipongeza kwa kuwa alifanikiwa kuwaua watu wote ambao walisababisha maumivu katika maisha yake.
Baada ya saa moja mlango ukafunguliwa, wanaume wawili wakaingia na kumtaka kuwafuata. Hakubisha, akafanya hivyo na kwenda mpaka katika kile chumba, akawekwa mezani ambapo kulikuwa na karatasi pamoja na kalamu na kuambiwa kwamba alitakiwa kuandika kila kitu kuhusu kile alichokuwa amekutana nacho katika suala zima la ugaidi pamoja na kuwataja watu waliompa bomu na mahali walipokuwa wakiishi hapo Marekani na Uturuki.
“Hii ndiyo nafasi yako,” alisema Thomson.
Hilo halikuwa tatizo, baada ya kuambiwa hivyo, akaanza kuwaambia kila kitu. Hakuwa mgeni nchini Marekani, alizifahamu sehemu nyingi hivyo hata kuwaambia mahali wale watu walipokuwa ilikuwa kazi nyepesi sana.
Huo ulikuwa msaada mkubwa kwa FBI, walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupata majina ya watu hao na mahali walipokuwa wakiishi hapo Marekani na Uturuki.
“Tunashukuru sana!” alisema Thomson.
Hakujua hatima ya maisha yake, alishukuriwa lakini watu hao hawakumwambia kwamba alitakiwa kuondoka au kubaki mahali hapo. Hakukuwa na mtu aliyeshughulika naye tena ila baada ya siku tatu akapewa taarifa kwamba kila kitu kilikuwa tayari, magaidi wote walikuwa wamekamatwa tena huku wakiwa na ramani ya Marekani kwa maana ya kutaka kulipua tena.
“So, what about me?” (kwa hiyo vipi kuhusu mimi?) aliuliza Fareed.
Hakukuwa na mtu aliyemjibu, aliendelea kuwekwa ndani ya chumba kile kwa siku kadhaa. Alipofikisha wiki ya pili akaanza kuumwa tena tumbo, akaanza kutapika damu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Wakati huu hali yake ilikuwa mbaya zaidi, alitapika madonge ya damu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma. Wakamtoa ndani ya chumba kile na kumpeleka hospitalini ambapo akaanza kupatiwa matibabu.
Hali yake haikutengemaa, utumbo ulishambuliwa sana na kansa kiasi kwamba mpaka madaktari wenyewe walishangaa na kusema kwamba ilikuwa ni vigumu sana kwa Fareed kupona, kwani utumbo wake ulibadilika mpaka rangi, ukawa na rangi nyeusi tii.
“This man is going to die,” (huyu jamaa anakufa) alisema daktari huku akimwangalia Thomson.
Kila mmoja alibaki kimya, utumbo ukapigwa picha, ulikuwa kwenye hali mbaya kupita kkawaida, ulishambuliwa kwa kiasi kikubwa na kusingekuwa na uwezekano wa kufanya muujiza wowote ule labda kama wangempokea kabla ya tatizo hilo kuanza wangemuwekea mpira, ila kwa pale alipofikia, hawakuwa na jinsi.
Siku ya tarehe 26.08/2016 ndiyo siku ambayo Fareed akafariki nchini Marekani huku akiwa kwenye maumivu makali. Ulikuwa msiba mzito kwa marafiki zake lakini hata maofisa wenyewe wa FBI walihuzunika, hawakutaka kabisa kumpoteza Fareed kwani aliwasaidia kupambana na magaidi kwa asilimia tisini.
Taarifa hiyo ikatolewa kwenye televisheni, mawasiliano yakafanyika na FBI wenyewe ndiyo walioshughulikia safari ya kuusafirisha mwili wake kuelekea nchini Tanzania ambapo baada ya kuwakabidhi ndugu, wakawaachia kiasi cha dola laki tano ambazo ni zaidi ya milioni mia tano kama shukrani kwa kila kitu alichokifanya Fareed kwao.
Huo ukawa mwisho wake, mchezo wa kuingiliana na wanaume wenzake ukayagharimu maisha yake, akafa katika maumivu makali. Akaunti yake ilikuwa na pesa nyingi, zaidi ya bilioni ishirini lakini zote akaziacha kwa ndugu ambao kwenye kugawana tu mpaka wengine wakauana, na pesa nyingi zilikuwa zile alizopewa kama zawadi na Bilionea Williams ambaye alikuwa akitumia kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kuhusika na mauaji ya Bilionea Belleck.
Huo ukawa mwisho wake, marafiki zake walimkumbuka, watu aliotembea nao wakamkumbuka, aliacha historia, mbali na mchezo mchafu aliokuwa ameufanya, wema wake, ucheshi na roho yake nzuri viliendelea kuwa mioyoni mwa watu wengi.

MWISHO

No comments

Powered by Blogger.