CCM Yatangaza Kufuta Uchaguzi Kata 41
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kupeleka salamu kwa wagombea wa nafasi
mbalimbali, wanaokiuka Katiba na Kanuni za Uchaguzi, baada ya kufuta
uchaguzi wa ndani ya chama hicho katika kata 41 kati ya kata 4,420
zinazoshiriki katika uchaguzi huo, kutokana na kubaini mchezo mchafu na
kuagiza mchakato kurejewa upya.
Hayo
yalibainishwa jana Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alipozungumza na waandishi
wa habari.
“Hii
ni awamu ya kwanza tunapeleka ujumbe kwa sababu wanaCCM wanataka CCM
mpya inayosimamia haki, haya ni maelekezo na yanapaswa kuzingatiwa ili
kurejesha hali ya uchaguzi katika eneo husika katika namna inayoheshimu
Katiba na Kanuni ya Uchaguzi na Uongozi na Maadili,” alifafanua Polepole.
Polepole
alibainisha kuwa kufutwa kwa uchaguzi huo ni agizo la viongozi wa juu
wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli na
Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana baada ya kusikiliza kwa kina kero na
malalamiko ya kiuchaguzi ya wanachama wa CCM.
Akifafanua
kuhusu suala hilo, alisema baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Dk
Magufuli alimuelekeza Kinana kuchukua hatua na kwa mamlaka aliyopewa,
ameagiza kufutwa na kurejewa upya hivyo wanachama na viongozi wanatakiwa
kufuata maagizo hayo.
Alizitaja
kata hizo ambazo ni 20, ni za Mkoa wa Dar es Salaam na nafasi
zinazotakiwa kurejewa katika mabano ni Kata ya Buguruni (Mwenyekiti na
Katibu), Kata ya Liwiti (Katibu), Kata ya Kariakoo (Mwenyekiti, Katibu
na Katibu Mwenezi), Kata ya Manzese (Mwenyekiti, Katibu na Katibu
Mwenezi), kata za Makuburi, Mabibo na Kigamboni.
Nyingine
ni Kiburugwa, Mchafukoge, Gerezani, Segerea (Mwenyekiti na Katibu),
Pugu Stesheni (Mwenyekiti, Katibu na Katibu Mwenezi), Kata ya Mianzini,
Kata ya Pugu (Katibu Mwenezi), Kata ya Ndugumbi, Kata ya Kilungule, Kata
ya Makumbusho, Kata ya Kitunda (Katibu na Katibu Mwenezi), Kata ya
Ukonga na Kata ya Msasani.
Polepole
alieleza kuwa kata nyingine ni kutoka mikoa mingine ni 18 kutoka kata
zote za Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara, Kata ya Seria kwa vijana
Wilaya ya Kondoa Mjini Mkoa wa Dodoma nafasi ya Katibu pamoja na Kata ya
Mapinga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Alizitaja
changamoto zilizojitokeza katika maeneo hayo na kusababisha uchaguzi
huo kufutwa ni: Kuwepo kwa wanachama wanaoendeleza makundi yaliyokuwepo
wakati wa Uchaguzi Mkuu, ambao wamekuwa wakipanga safu za uongozi na
kuamua nani atakuwa kiongozi wa chama, jambo ambalo halikubaliki.
Pia
alisema wapo viongozi ambao walishindwa kutoa usimamizi mzuri wa mali
za chama na kusababisha upotevu mkubwa wa fedha na mali, lakini
wamerejea katika nafasi hizo, jambo ambalo pia halikubaliki.
Aidha,
alisema wapo wanachama waliokiuka misingi ambayo inamtaka mgombea kuwa
mkazi wa eneo ambao unaomba dhamana ya uongozi, lakini kama siyo mkazi
wa eneo hilo hupaswi kugombea, lakini wapo ambao si wakazi wameomba
dhamana katika maeneo hayo, jambo ambalo halikubaliki.
Katibu
huyo wa Itikadi na Uenezi CCM aliongeza kuwa katika uchaguzi huo, pia
kumebainika kuwepo kwa vitendo vya uonevu na kutokutenda haki katika
mchakato wa uchaguzi, kama ambavyo Katiba ya CCM inavyosema kuwa haki ni
asili ya chama hicho.
Alisema
changamoto nyingine ni kukiukwa kwa Katiba na Kanuni, baada ya maeneo
mengine kutokutoa taarifa sahihi kuhusu wagombea, jambo ambalo limetajwa
kama kupotosha vikao.
Machi
mwaka huu, Rais Magufuli alionya kuwa mwanachama yeyote atakayebainika
kutumia rushwa kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho, jina lake
halitarudi. Aliwataka wanachama wa chama hicho, bila ya kujali uwezo wao
kifedha, wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali.
Alisema
chama kitafuatilia kwa ukaribu mchakato wa uchaguzi wote kuanzia ngazi
ya chini ili kujihakikishia kuwa watakaoshiriki kwenye vitendo vya
rushwa, watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa Katiba, Kanuni za
Uchaguzi na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM.
Post a Comment