AJIBU,NIYONZIMA NANI ATAMFUATA TAMBWE?
Mechi hiyo itapigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa pia ni ishara ya kufunguliwa kwa msimu wa Ligi Kuu Bara wa 2017/18, utakaoanza kutimua vumbi Jumamosi hii ya Agosti 26, mwaka huu.
Lakini pia mechi hiyo ni muhimu kwa timu hizo kwani ndiyo itakayotoa dira nzima ya usajili zilizoufanya kwa ajili ya ligi kuu kama utakuwa na manufaa au la.
Hata hivyo, pamoja na hali hiyo baadhi ya wachezaji wapya waliojiunga na timu hizo mbili wakitokea upande mmoja na kwenda mwingine nao watakuwa na kazi kubwa ya kuonyesha makali yao ili waweze kuingia kwenye vitabu vya rekodi kama ilivyo kwa wale waliowatangulia.
Wachezaji hao ni Ibrahim Ajibu ambaye msimu uliopita aliitumikia Simba lakini hivi sasa yupo na kikosi cha Yanga pamoja na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ambaye msimu uliopita alikuwa Yanga na sasa yupo na timu ya Simba.
Kutokana na hali hiyo, katika mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka hapa nchini watataka kuona ni mchezaji gani atakayeweza kuandika rekodi ya kuifunga timu yake zamani katika mchezo huo.
Rekodi kama hiyo kwa sasa inashikiliwa na Mrundi Amissi Tambwe ambaye baada ya kuondoka Simba na kujiunga na Yanga amekuwa akiitesa Simba mara kwa mara kila anapokutana nayo uwanjani.
Tambwe ambaye alijiunga na Yanga msimu wa 2014/15 anashikilia rekodi ya kuifunga Simba mfululizo katika mechi tatu alizoitumikia baada ya kujiunga na timu hiyo.
Tambwe ambaye ni raia wa Burundi lakini mkewe ni raia wa Tanzania mwenye asili ya mkoa wa Mbeya kwa mara ya kwanza alianza kuifunga Simba Septemba 26, 2015 ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kama haitoshi alifanya hivyo pia Februari 20, 2016 ambapo katika mechi hiyo pia Simba ilitandikwa mabao 2-0, kitendo cha Tambwe kuifunga timu hiyo kwa mara nyingine tena kilisababisha balaa.
Mashabiki wa Simba waliwajia juu viongozi wao wakiwashutumu kwa kumwacha mchezaji huyo wakati akiwa bado bora na badala yake anazidi kuwatesa kila wakati.
Hata hivyo, mashabiki hao walizidi kuumia zaidi Oktoba Mosi, 2016 ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 ambapo bao hilo alifunga likiwa gumzo kubwa kutokana na staili aliyoitumia wakati akilifunga.
Kabla ya kufunga bao hilo, Tambwe alipokea pasi ndefu iliyopigwa na Mbuyu Twitte na ‘kuukontroo’ kifuani kwake akiwa katikati ya mabeki wawili wa Simba, Novatus Lufunga ambaye kwa sasa hayupo kikosini hapo pamoja na Mganda, Juuko Murshid na baadaye akaushika mpira huo bila ya mwamuzi kuona kisha akaukwamisha mpira wavuni kwa ustadi wa hali ya juu.
Ukiachana na bao hilo katika mechi hizo nyingine, pia Tambwe alifunga bao mojamoja.
Kutokana na hali hiyo Ajibu ambaye alisajiliwa na Yanga kwa kitita cha Sh 70 milioni pamoja na Niyonzima ambaye alijiunga na Simba kwa Sh 115 milioni wana kazi kubwa ya kufanya kwenye mchezo huu wa Jumatano ili nao waweze kuandika rekodi kama alivyofanya Tambwe baada ya kutoka Simba na kujiunga na Yanga.
Post a Comment