Uteuzi wa Jokate Mwegelo UVCCM Waibua Mfarakano
Mjadala
mkubwa umeibuka kuhusu uteuzi huo, ambapo baadhi ya wanachama na
viongozi wa juu wa jumuiya hiyo wamedai kuwa haukufuata kanuni na
taratibu za umoja huo.
Vyanzo
vya kuaminika kutoka katika umoja huo vimedai kuwa baadhi ya viongozi
wa juu wa UVCCM hawakushirikishwa katika uteuzi huo uliofanywa na kigogo
mmoja wa umoja huo.
Taarifa
za ndani zinaeleza kuwa uteuzi huo haukushirikisha wajumbe wa Kamati ya
Utekelezaji wala Baraza Kuu la UVCCM, ambalo halikukutana kumthibitisha
Jokate kama kanuni zinavyoelekeza.
Kwa
mujibu wa kanuni za jumuiya hiyo, wajumbe wa kamati ya utekelezaji
hawazidi 10, ambapo miongoni mwao ni Mwenyekiti wa umoja huo Taifa,
Makamu Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na mjumbe mmoja
kutoka makao makuu ya chama.
Wajumbe wa baraza kuu ni wenyeviti na makatibu wa mikoa na mjumbe mmoja kutoka katika kila mkoa.
Kutokana
na kile kilichodaiwa kuwa ni mvurugano ndani ya umoja huo, Kaimu Katibu
Mkuu wa UVCCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka, amesema kuwa uteuzi huo
ulifuata taratibu zote za chama.
“Ni
kweli amekaimishwa kwa kufuata taratibu zote za chama, kikao cha Kamati
ya Utekelezaji kilikutana Aprili 18, mwaka huu, Dar es Salaam na ndicho
kimewakaimisha wakuu wa idara watano akiwamo Jokate.
“Hao
wanaolalamika hawajui kanuni na taratibu za jumuiya yetu, huwezi kupata
nafasi kama kikao cha Kamati ya Utekelezaji hakijakaa,” alisema Shaka.
Hata
hivyo alikiri kutoitishwa kwa kikao cha Baraza Kuu ili kuthibitisha
uteuzi huo, akisema ni gharama kubwa kuitisha kikao hicho.
“Kwa
kawaida Baraza Kuu huwa linakutana kila baada ya mwaka mmoja, kuita
baraza kuu ni gharama sana hivyo ikitokea kuna nafasi wazi Kamati ya
Utekelezaji ina mamlaka pia ya kumthibitisha,” alisema.
Kwa upande wake, Jokate alishukuru kwa uteuzi huo na kuahidi kuifanya jumuiya hiyo iwe karibu zaidi na vijana wa Kitanzania.
“Nashukuru
kwa imani waliyoonyesha viongozi wangu ila zaidi kuona nina uwezo wa
kuongoza idara hiyo nyeti na muhimu kwenye jumuiya.
“Kikubwa
ni kuifanya jumuiya iwe karibu zaidi na vijana wa Kitanzania na
kurudisha tumaini na kusimamia changamoto wanazozikabili vijana katika
kujiletea maendeleo,” alisema Jokate.
Jokate
pia alikuwa miongozi mwa wanachama 450 wa CCM waliojitokeza kuchukua
fomu za kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Jokate alianzia kwenye mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2006 ambapo aliibuka mshindi wa pili.
Hivi
sasa anajishughulisha na sanaa na ujasiriamali ambapo anamiliki Lebo ya
Kidoti Fashion inayojihusisha na uuzaji wa nywele na mavazi.
Post a Comment