Tamko la serikali kuhusu kushambuliwa waandishi wa habari katika mkutano wa CUF
Serikali
imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya
waandishi wa habari katika mvutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam
kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi
(CUF). Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha
ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo waandishi ambao vifaa
vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi hilo.
Tunachukua
fursa hii kulaani kitendo cha kuumizwa wanahabari tena waliokuwa
wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni
taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na
kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.
Kifungu
cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016
kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa
kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa.
Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu
imeuridhia.
Tunawatakia
nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa na wenzao wengine waliopatwa
na jakamoyo katika tukio hilo. Kwa kuwa suala hili tayari limeripotiwa
polisi, tunawaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na
kuviachia vyombo husika vilifanyie kazi ili hatua stahiki za kisheria
zichukuliwe.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali
Post a Comment