Haki sasa itendeke katika kurudisha nidhamu bungeni
BAADA ya wabunge wa kambi ya upinzani kuzua tafrani bungeni wiki
iliyopita na kusababisha kuvunjika kwa kikao kilichokuwa kikiongozwa na
Naibu Spika, Job Ndugai, uongozi wa chombo hicho cha kutunga sheria
umeapa kuwapeleka mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Kabla ya kikao hicho kuvunjika, wabunge hao wa upinzani walisimama wote kwa pamoja na kuanza kupiga kelele za kupinga hatua ya Naibu huyo wa Spika kutaka iondolewe bungeni hoja iliyowasilishwa mapema na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, huku akiruhusu kujadiliwa kwa hoja ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliyetaka kuondolewa kwa hoja binafsi ya mbunge huyo wa Ubungo.
Katika hoja yake, mbunge huyo wa Ubungo alitaka Bunge liazimie kuitaka Serikali ichukue hatua za haraka za kuboresha mfumo wa upatikanaji wa majisafi na udhibiti wa majitaka katika Jiji la Dar es Salaam. Naibu Spika aliruhusu kujadiliwa kwa hoja ya Profesa Maghembe badala ya hoja ya Mnyika, hatua ambayo iliwafadhaisha wabunge wa upinzani ambao walisimama na kupiga kelele wakipinga kile walichokiita ukandamizaji wa kambi ya upinzani na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za Bunge.
Itakumbukwa kuwa, hasira za wabunge wa upinzani zilikuwa zimekolezwa mapema pale Spika Anne Makinda, huku akiungwa mkono na wabunge wa CCM alikuwa ameridhia kutojadiliwa kwa hoja ya Mbunge wa upinzani, James Mbatia aliyekuwa akisisitiza kwamba elimu ya sekondari na msingi imekuwa ikitolewa bila kuwapo mitalaa na kuitaka Serikali iwasilishe mitalaa hiyo bungeni kama ushahidi iwapo inadhani hoja yake siyo sahihi.
Hatua hiyo ya Spika ilichangia kwa kiasi kikubwa kukuza dhana ya wabunge wa upinzani iliyojengeka kwa muda mrefu kwamba Bunge linaendeshwa na kuongozwa kwa misingi ya kisiasa na kiitikadi. Kwa maneno mengine, kambi ya upinzani inaelekea kukata tamaa na imejenga dhana kwamba uongozi wa Bunge, yaani Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge ni wakala wa serikali na unaikandamiza kambi ya upinzani ili kukisaidia CCM kutimiza malengo yake ya kisiasa.
Dhana hiyo imejengeka zaidi wakati huu wa Bunge hili la Kumi, chini ya Spika Makinda na ndiyo maana tofauti na Bunge la Tisa lililokuwa chini ya Spika Samwel Sitta, hivi sasa tunashuhudia uadui mkubwa na matukio yanayoashiria kuwapo kwa hali ya kutoaminiana, kutoheshimiana na kutovumiliana kati ya kambi hizo mbili.
Vurugu zilizotokea bungeni mwanzoni mwa
wiki zimeibua hofu miongoni mwa wananchi kwamba hatua za makusudi
zisipochukuliwa kuondoa, hautapita muda mrefu kabla hatujaanza kuona
wabunge wa kambi hizo mbili wakichapana makonde katika ukumbi wa Bunge.
Sisi tunalaani vurugu zilizotokea bungeni mwanzoni mwa wiki na tunataka hatua zichukuliwe kuhakikisha utulivu na nidhamu vinarejea bungeni.
Sisi tunalaani vurugu zilizotokea bungeni mwanzoni mwa wiki na tunataka hatua zichukuliwe kuhakikisha utulivu na nidhamu vinarejea bungeni.
Hata hivyo, tunaushauri uongozi wa Bunge kuchukua tahadhari kubwa katika kufanikisha jambo hilo, kwani unaweza kuingia katika mtego wa kukurupuka na kufanya maamuzi ya kuegemea upande mmoja, hivyo kukuza tatizo.
Busara inahitajika na pengine ni bora kwanza kuangalia kiini cha tatizo. Tunadhani Spika na Naibu wake walikosea kwa kuwatuhumu na kuwahukumu baadhi ya wabunge hata kabla hawajapelekwa mbele ya kamati ya Bunge husika na hii pengine inatia shaka kama kweli haki itatendeka.
Tunasisitiza kwamba kipaumbele sasa kiwe kutafuta mwafaka ndani ya Bunge. Lazima uongozi wa Bunge utambue kwamba adhabu na kulipiza visasi vitachochea chuki zitakalolifanya Bunge lisitawalike.
Post a Comment