Spika Wa Bunge Job Ndugai Atoa Nafasi ya Mwisho CHADEMA

Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetoa nafasi ya pili na ya mwisho
kwa ajili ya mchakato wa kuwapata wawakilishi wawili wa Tanzania katika
Bunge la Afrika Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Akitoa
taarifa yake bungeni leo , Spika wa Bunge hilo Job Ndugai amesema hadi
sasa nafasi hizo bado ni za CHADEMA na atahakikisha haki hiyo wanaipata
na kwamba Katibu wa Bunge atatoa taarifa ni lini mchakato huo
utafanyika.
Katika
hatua nyingine, Ndugai ametoa tahadhari kwa chama hicho kuwa yeye ndiye
mwenye mamlaka ya kutoa utaratibu wa kupatikana kwa wawakilishi wa
Tanzania kupitia vyama vya upinzani, hivyo endapo wasipotumia nafasi
hiyo, atatumia mamlaka aliyonayo kutangaza utaratibu mwingine ili
Tanzania isikose wawakilishi katika nafasi hizo.
“Ikumbukwe
kuwa maamuzi haya ya kuwatenganisha wabunge wa upinzani kwa kuangalia
vyama vyao ni maamuzi ya Spika, tukumbuke mabunge yaliyopita maspika
wenzangu hawakufanya hivyo, waliwaweka wabunge wote wa upinzani kwenye
kundi moja, mimi nikasema twende na demokrasia hii ya wawili, ambayo
katika kufanya hivyo, mimi yuleyule,....tuendelee....... Hatuwezi
kukubali nchi yetu ikose uwakilishi nchi yetu ikatekwa nyara kwa sababu
fulani fulani". Amesema Ndugai
Pia Ndugai amewatoa hofu watanzania kuwa hawatakosa uwakilishi kwa kuwa anajua cha kufanya. "Tutatoa
nafasi ya pili, lakini baada ya nafasi ya pili, tunajua hatua
itakayofuata, nawahakikishia watanzania kwamba hawatakosa nafasi katika
bunge hilo”
Katika
uchaguzi uliofanyika juzi, Bunge hilo liliwachagua wajumbe 7 kati ya 9
waliohitajika, huku wagombea wawili wa CHADEMA Ezekiah Wenje na
Lawrence Masha wakikataliwa kwa kupigiwa kura za hapana.
Post a Comment