Wema: Siasa bila kujipanga hutoki, ‘utakatwa’ tu!
Staa wa Bongo Movie, Wema Sepetu.
Leo
tunaye msanii wa filamu za Kibongo, Wema Sepetu ambaye hivi karibuni
alithubutu kugombea ubunge kupitia viti maalum mkoani Singida.
Kwa
bahati mbaya kura za msanii huyu hazikutosha. Mwandishi wetu alionana
na mwanadada huyo nyumbani kwake Kijitonyama jijini Dar na kumpiga
maswali 10 mujarabu. Ungana nami...
Ijumaa: Hongera kwa kujitosa kwenye siasa, nini kilikusukuma kuingia huko?
Wema: Nilikuwa nashauku ya kuwa mheshimiwa, hata baba yangu aliwahi kuniambia naweza hivyo nikajaribu bahati yangu.
Ijumaa: Ukiacha marehemu baba yako, nani alikupa sapoti kubwa na ukajiona unaweza?
Wema: Namshukuru mama yangu, alinipa sapoti kubwa nikajiona naweza kwani alinitoa hofu niliyokuwa nayo.
Ijumaa: Unadhani kipi kimekuangusha kwenye uchaguzi ule?
Wema: Uchanga wangu kwenye siasa lakini naamini muda ulikuwa bado.
Ijumaa: Ingawa hukufanikiwa kupata nafasi ya ubunge umejifunza nini kupitia siasa?
Wema:
Kwa kweli nimejifunza vitu vingi maana haviendani hata na umri wangu na
nimepata ujasiri mkubwa. Kikubwa ukiingia kwenye siasa ujipange sana.
Ijumaa: Je, kwa hatua uliyoifikia unategemea kuendelea na siasa?
Wema: Niache? Siwezi kwani itakuwa kazi yangu, kama gari ndiyo limewaka sasa.
Ijumaa: Najua siasa ni hela hasa kipindi cha kampeni, uliwezaje kumudu gharama zote?
Wema:
Ni rahisi sana ukiwa na watu wanaokupenda, walijitokeza watu
kunichangia kwa ajili ya kuhakikisha nafanikiwa. Siwezi kuwataja lakini
nawashukuru sana.
Ijumaa: Tulipata habari kwamba baada ya kushindwa uliangua kilio, kwa nini?
Wema:
Unajua unapoenda kufanya kitu lazima una matumaini japo kuna kushindwa
lakini kushinda ndiyo lengo sasa usipofanikisha lazima roho inauma.
Ijumaa: Ulijisikiaje ulipokuta nyomi la watu wakikusubiri kwa ajili ya kukupokea wakati hukuwa umeshinda?
Wema: Niliamini nina watu wengi ambao wananipenda na nilijifunza mengi kupitia ujio wao, pia walinitia moyo wa kuendelea na siasa.
Ijumaa: Kuna madai kuwa baada ya kushindwa una mpango wa kuhamia Ukawa, hilo unalizungumziaje?
Wema:
Ninachojua watu wa Ukawa wamenitafuta na ilikuwa tukutane jana
(Jumatatu) ila tutakutana Jumatano (juzi), nikijua wanachoniitia ndiyo
nitafanya uamuzi.
Ijumaa: Baada ya kuingia kwenye mambo ya siasa tumtegemee Wema wa aina gani?
Wema: Mtarajieni Wema wa tofauti na yule mliyemzoea, mambo ya skendoskendo hayatakuwa na nafasi kwenye maisha yangu.

Post a Comment