ad

ad

SI KITU BILA PENZI LAKO-08

 
NYEMO CHILONGANI
0718069269

Watu wote waliokuwa na mapanga. Marungu na fimbo walikuwa wakimwangalia kijana ambaye alikuwa ametoa mguno. Mguno wake haukuwa wa kawaida hata kidogo ulisikika katika hali ambayo ilimaanisha kwamba kulikuwa na kitu.
Akaichukua tochi yake ambayo alikuwa ameifunga katika mkanda wake kiunoni na kuiwasha kisha kummulika Victoria, kila mwanaume akaonekana kuogopa, hawakuamini kama mtu ambaye walikuwa wakimshambulia alikuwa msichana. Kila mmoja akaonekana kuogopa.
Damu zilikuwa zikiendelea kumtoka Victoria, pale chini alikuwa kimya, hakutingishika hata kidogo. Wanaume wote walibaki kimya kwa muda huku wote wakionekana kupigwa na butwaa kubwa. Mmoja mmoja akaanza kupiga hatua kurudi nyuma.
“Sasa mnakwenda wapi? Mnataka kukimbia?” Mzee Mkude ambaye alikuwa mwenyekiti wa kijiji kile aliwaambia wanaume ambao walikuwa wakipiga hatua kurudi nyuma.
“Hakuna mtu yeyote kuondoka. Tumbebeni tumpeleke katika hospitali ya kijiji” Mzee Mkude aliwaambia na kisha kumbeba Victoria na kuanza kumpeleka katika hospitali ya kijiji.
Wala hakukuwa mbali sana kutoka mahali hapo, ni ndani ya dakika tano wakawa wamekwishafika katika hospitali hiyo ambapo moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu ya mapokezi. Hakukuwa na mtu yeyote katika sehemu ile ya mapokezi, wakaanza kuiya ambapo baada ya dakika kadhaa, dada aliyekuwa amevalia nguo nyeupe tupu akatikea mahali hapo.
“Karibuni” Dada yule aliwakaribisha huku akiwasha taa.
“Asante” Mzee Mkude alijibu.
Mshtuko mkubwa ukampata dada yule wa mapokezi mara baada ya macho yake kutua katika mwili wa Victoria. Mwili ulikuwa unatisha ambao hakuweza kuuangalia mara mbili. Aliuhisi mwili wake ukitetemeka kwa hofu. Ni kweli alikuwa amewaona watu wengi wakiwa wamejeruhiwa, lakini kwa Victoria ilikuwa ni zaidi ya kujeruhiwa.
Mwili wake ulikuwa umechanwachanwa na fimbo pamoja na mapanga ambayo alikuwa ameshambuliwa nayo. Mwili ulikuwa umevimba, marungu ambayo alikuwa amepigwa pasipo mpangilio, yalionekana kumvimbisha kupita kiasi.
“Kuna nini tena? Mbona huyo binti yuko hivyo?” Yule dada wa mapokezi aliuliza huku akionekana kushangaa.
“Ajali. Ajali mama” Mzee Mkude alimwambia dada yule wa mapokezi huku akionekana kuogopa.
“Ajali! Ajali ya nini?”
“Si unajua mambo ya kulinda mifugo yetu usiku. Tulivyomuona tulifikiri mwizi na ndipo tukaanza kumshambulia” Mzee Mkude alimwambia dada yule.
Bado yule dada alionekana kusisimka mwili wake kupita kiasi. Victoria alionekana kuumia kupita kawaida kiasi ambacho ingekuwa ngumu sana kupata matibabu katika hospitali ile. Kitu alichokifanya ni kuondoka moja kwa moja kwenda kwenye chumba kimoja, aliporudi, alirudi na mwanaume mmoja mweusi aliyekuwa na ndevu nyingi.
“Naomba uwapeleke Nzega” Dada wa pale mapokezi alimwambia mwanaume yule.
Japokuwa ilikuwa ni moja ya kazi yake, mwanaume yule wala hakuwa na kipingamizi japokuwa alikuwa akionekana kuchoka kupita kiasi. Aliwaangalia mzee Mkude na wenzake, hasira zikamshika kwani aliona kama anasumbuliwa.
Macho yake alipoyaamisha na kuyapeleka kwa Victoria ambaye alikuwa amelazwa benchini, yeye mwenyewe akaanza kufanya haraka haraka. Hali ya Victoria ilionekana kumtisha kila mtu. Akawaambia wambebe na kisha kumpeleka katika gari aina ya Pick Up na kisha kuwasha gari lile.
“Ninaokwenda nao ni nani na nani?” Mwanaume yule dereva aliuliza.
Mzee Mkude na wanaume wengine wawili wakajitokeza na kuingia garini huku watu wengine wakiondoka mahali hapo. Kila wakati walikuwa wakimwangalia Victoria ambaye alionekana kuwa katika hali mbaya kupita kawaida, damu ambazo zilikuwa zikimtoka zikaanza kuchuruzika katika bodi la gari lile.
Kwa kawaida kutoka katika kijiji cha Ukenyenge mpaka Nzega mkoani Tabora ilikuwa ni lazima utumie masaa matatu kama tu ungetumia gari. Barabara haikuwa nzuri hata kidogo, kila sehemu kulikuwa na mashimo. Dereva hakuendesha gari lile katika mwendo wa kawaida, alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi huku lengo lake likiwa ni kufika Nzega haraka.
Ndani ya masaa mawili ndio wakaanza kuingia Nzega huku ikiwa imetimia saa kumi alfajiri. Walipoingia katika barabara ya lami, dereva aliongeza kasi zaidi mpaka wakaingia katika hospitali ya Nzega. Kutokana na kutokuwa na mtu nje ya eneo la hospitali, wakamteremsha Victoria na kuanza kuelekea nae ndani ya hospitali ile.
“Mmmhh! Mbona hivyo jamani” Dada aliyewapokea mapokezi aliwauliza.
“Kwanza jaribu kutusaidia halafu maswali baadae dada” Derva alimwambia dada yule ambaye akaufungua mlango na wao kumuingiza Victoria. Moja kwa moja wakampeleka mpaka chumbani ambako akalazwa na kisha mzee Mkude kuelekea Mapokezini kumwandikisha.
Masaa yalikuwa yakisogea mpaka datari mkuu kuingia. Moja kwa moja akapewa taarifa juu ya mgonjwa ambaye alikuwa ameletwa alfajiri. Daktari akaanza kuelekea katika chumba kile ambako baada ya muda akarudi huku uso wake ukiwa umejaa huzuni.
Mwili wa Victoria na kwa jinsi ambavyo alikuwa amejeruhiwa ulionekana kumshtua kupita kiasi. Micharazo ilikuwa ikionekana vizuri mwilini mwake huku alama za kukatwa katwa na panga zikionekana kwa mbali. Akaanza kuwaangalia mzee Mkude pamoja na wenzake na kisha kuwaita ofisini.
Mzee Mkude alielezea kila kitu kilichotokea lakini huku akidanganya kuhusu kijiji walichotokea. Daktari alibaki kimya akimsikiliza, alipoona ameridhika na maelezo yake, akawaambia waende wakasubiri benchini.
“Mbona umemdanganya kuhusu sehemu tulipotokea?” Kijana mmoja kati ya wale wawili aliokuja nao aliuliza.
“Hii kesi. Tena kesi kubwa. Hapa ni lazima tuondoke haraka iwezekanavyo” Mzee Mkude aliwaambia.
Huo ndio uamuzi uliofikiwa, hawakutaka tena kubaki hospitalini pale, tayari waliona kuwa kesi ilikuwa ikiwajia kama tu wangediriki kusubiri kujua ni kitu gani kingeendelea. Hakukuwa na yeyote ambaye alikuwa tayari kusubiri, kwa mwendo wa haraka haraka wakatoka katika jengo lile na kukimbia huku wakimwacha Victoria akiwa hana mtu yeyote anayemfahamu pale Nzega.
*****
Bado mvua ilikuwa ikiendelea kunyesha, mawingu mazito yalikuwa yametawala angani. Ardhi ilikuwa na matope mengi kupita kiasi lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyesimama. Bado walikuwa wakiendelea kukimbia kwa kasi, hawakutaka kutiwa mikononi mwa wale Polisi ambao waliwaokoa kutoka katika mikono ya wauaji.
Zilipita dakika thelathini, mvua ile ikakatika. Wakaanza kutembea kwa mwendo wa kasi mpaka kufika katika sehemu ambayo ilikuwa na kilima kimoja ambacho hakikuwa kikubwa sana. Wakaanza kupandisha kilima kile kwa mwendo wa kasi.
Giza nene bado lilikuwa limetanda huku kadri walivyokuwa wakikipandisha kilima kile na ndivyo ambavyo baridi lilivyozidi kuongezeka. Walitamani kama wangekuwa na makoti mazito ambayo yalikuwa na kazi ya kuzuia baridi, lakini walikuwa na fulana tu.
Wakafika pale kilimani na kuanza kuangalia kwa chini. Ni miti mirefu ndiyo ambayo ilikuwa imetawala huku giza kubwa bado lilikuwa limetanda katika eneo hilo. Wakaamua kuufuata mti ambao ulikuwa katika kilima kile na kupumzika huku wakipaona mahali hapo kuwa salama kwa ajili ya maisha yao.
Waliendelea kubaki kilimani pale, masaa yaliendelea kukatika huku kiubaridi kikizidi kuwapiga mahala hapo. Kila mmoja alikuwa akitetemeka kwa sababu ya baridi lile ambalo lilizidi kuwapiga zaidi na zaidi. Hakuna aliyepata usingizi ingawa walikuwa wamechoka kupita kiasi.
Kwa mbali mwanga ukaanza kuonekana, wakaangalia tena chini ya kilima kile, kwa mbali walikuwa wakiona mwanga wa taa za gari ambazo zilikuwa zimesimama.
“Unaoa mianga ile?” Patrick alimuuliza Aziz ambaye alianza kuangalia vizuri.
“Naiona. Nafikiri zile zitakuwa nyumba”
“Zile sio nyumba Azizi, ile ni mianga ya taa. Itatubidi tuondoke mahali hapa kuelekea kule, nadhani pale tutaomba msaada wa kufikishwa mjini” Patrick alimwambia Aziz na kisha kuanza kushuka kilima kile.
Kutokana na kilima kile kuwa na miti mingi pamoja na kona ambazo zilionekana kuwa kama njia zilizosahaulika kupitwa, walitumia zaidi ya dakika arobaini hadi kufika chini ya kilima kile na kuanza kuelekea kule ambako waliyaona mataa yale ya gari.
Umbali ulikuwa ni tofauti na jinsi ambavyo walijua kabla. Walitembea zaidi na zaidi huku kila mmoja akiwa na uhakika wa kufika pale ambako taa za gari zilipoonekana. Walitembea kwa mwendo mrefu kupita kawaida. Mwanga ukaanza kutokeza, bado walikuwa wakizidi kutembea. Kila mmoja alionekana kuchoka, masaa mawili walikuwa wameyatumia lakini kitu cha ajabu hawakuwa wameifikia sehemu ile iliyokuwa na magari yale.
Kila mmoja alionekana kukata tamaa huku wakiona labda walikuwa wamekosea njia. Patrick akaanza kuufuata mti mrefu ambao ulikuwa katikakati ya miti mingi mifupi na kisha kuanza kuuparamia. Alienda juu zaidi na zaidi huku Azizi akimsubiria chini.
“Inaonekana si mbali sana kutoka hapa” Patrick alimwambia Aziz mara baada ya kuteremka.
“Unasema kweli?”
“Ndio. Nimesikia honi kadhaa. Nafikiri si mbali sana kutoka hapa” Patrick alimwambia Azizi na kuendelea na safari yao.
Miili yao ilikuwa michafu kupita kawaida. Matope yalikuwa yamezitawala suruali zao. Bado waliendelea kupita katika matope lakini hakukuwa na yeyote aliyeonekana kujali. Kwa kipindi hicho, kitu ambacho walikuwa wakikitaka ni kufika Shinyanga Mjini, sehemu ambayo wangetafuta kazi yoyote ya kufanya ili wajiingizie fedha.
Wakajikuta wakitumia masaa matatu kutoka kilimani mpaka kufika katika sehemu ambayo wakaanza kusikia sauti za watu wakiongea huku wengine wakipiga kelele. Wakaonekana kupata nguvu, wakaanza kupiga hatua za haraka haraka kusogea kule kulipokuwa na kelele zile.
Wakatokea katika sehemu ambayo ilikuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu. Daladala zilikuwa katika kila sehemu mahali hapo. Wakinamama walikuwa wameshika matenga makubwa yaliyokuwa matupu. Utingo wa daladala tofauti walikuwa wakiendelea kuitia abiria ambao walikuwa wakiingia katika magari hayo mmoja baada ya mwingine.
Jua lilikwishaanza kuchomoza mahali hapo, kitu ambacho walikuwa wakikitaka ni kujua kwamba walikuwa wapo katika kijiji gani na kwa namna gani ambayo wangeweza kufika Shinyanga mjini. Wakapitisha macho yao katika sehemu mbalimbali maeneo hayo, watu walikuwa wakionekana kuwa bize kupita kawaida.
Kadri sekunde zilivyoendelea kwenda mbele na ndivyo ambavyo idadi ya watu ilipozidi kuongezeka mahali hapo. Macho yao yakatua katika mzee mmoja ambaye alikuwa amesimama nje ya hiace yake huku mkononi akiwa na sigara akivuta. wakaanza kupiga hatua na kumfuata.
“Tunaomba kuuliza. Hivi hiki ni kijiji gani?” Patrick aliuliza mara baada ya kumsalimia.
Mzee yule hakujibu kitu, alibaki akiwaangalia kwa macho yaliyoonekana kukasirika, alionekana kutokuwa na haja ya kuwajibu. Hisia zake zote alikuwa amezipeleka katika sigara ile ambayo alikuwa akiingiza moshi mdomoni na kuutoa. Patrick alibaki akimshangaa mzee yule ambaye bado alikuwa akiendelea kuvuta sigara kwa staili ile ile ya kuuingiza moshi na kuutoa hali iliyoonekana kukumpa raha.
“Tunataka kufika Shinyanga mjini. Nauli shilingi ngapi?” Patrick aliuliza mara baada ya kumuona mzee yule akiwa amenyamaza.
“Umesema mnataka kufika wapi?” Mzee yule aliuliza huku akionekana kuwa na mshangao.
“Tunataka kufika mjini” Azizi alijibu.
“Hivi mnajua huu ni mkoa gani?”
“Shinyanga” Azizi alitoa jibu ambalo lilionekana kumshangaza mzee yule.
“Shinyanga! Hapa si Shinyanga” Yule mzee ambaye alikuwa akijulikana kama mzee Masharubu alijibu.
“Hapa si Shinyanga?”
“Ndio. Hapa ni Mwanza. Na hapa mko katika kijiji cha Misungwi” Mzee Masharubu alijibu.
Kila mmoja akaonekana kushtuka, hawakuamini kama masaa nane ambayo walitembea porini, walikuwa wametembea mpaka katika jiji la Mwanza. Kila mmoja akabaki akiwa ameduwaa.
“Tunataka kwenda mjini” Patrick alimwambia mzee Masharubu.
“Mna nauli?”
“Kwani ni shilingi ngapi?”
“Elfu moja kwa kila kichwa” Mzee Masharubu alijibu.
Patrick akamvuta Aziz pembeni na kuanza kuongea nae huku yule mzee akiwaangalia. Patrick akaanza kujipekua mfukoni mwake, akajikuta ana shilingi mia mbili tu. Tayari akaona mambo kuwa magumu kwa upande wake. Azizi akajipekua mfukoni, alijikuta kuwa na shilingi mia nne tu. Jumla walikuwa na shilingi mia sita.
Tayari waliona ugumu wa kupanda daladala. Wakapanga kwenda kumuomba msaada mzee Masharubu ambaye alionekana kutokuwa na mzaha na kazi yake.
“Tunaomba utusaidie. Tuna shilingi mia sita” Patrick alimwambia mzee Masharubu kwa sauti iliyojaa unyenyekevu.
“Shilingi mia sita! Hili gari ni la baba yenu?”
“Hata ukitushusha njiani, tutashukuru mzee wetu” Patrick alimwambia mzee Masharubu ambaye alibaki akiwaangalia kwa hasira.
“Hivi mnajua kwa nauli hiyo mtaishia wapi?”
“Hapana”
“Nitawashushia Kigongo, kilometa thelathini hadi mjini”Mzee Masharubu aliwaambia.
“Kilometa thelathini kutoka hapo Kigongo hadi Mjini?” Azizi aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Ndio” Mzee Masharubu aliwaambia.
Wote wakaonekana kukatishwa tamaa. Walikuwa wametembea porini kwa takribani kilometa themanini, tena kwa kukimbia muda mwingi hadi kufika mahali hapo. Kila mmoja alionekana kuchoka. Kama wangepanda katika daladala hiyo na kushushiwa Kigongo basi ingewachukua kutembea kwa miguu mpaka mjini hali ambayo waliiona kutowezekana kabisa kwa jinsi walivyokuwa wamechoka.
Walijaribu kumuomba mze Masharubu awasaidie lakini akaonekana kuwa mgumu kufanya hivyo, yeye kitu alichokuwa akikiangalia ni fedha tu. Kama angewasaidia Patrick na Azizi kwa kile kiasi cha fedha ambacho walikuwa nacho basi alijiona angepata hasara sana kwa sababu tu mafuta yalikuwa yamepanda bei.
“Tunaomba utusaidie mzee” Patrick alimuomba mzee Masharubu ambaye alionekana kukasirika zaidi.
“Hebu tokeni hapa kabla sijawafanya kitu kibaya” Mzee Masharubu aliwaambia kwa hasira.
Patrick na Azizi hawakuwa na jinsi, wakaanza kupiga hatua kuondoka mahali hapo kuyafuata magari mengine ambayo yalikuwa yakipakia abiria. Mara wakasikia sauti ya mzee Masharubu akiwata, wakageuka na kumwangalia.
“Mnasema mnakwenda wapi?” Mzee Masharubu aliwauliza.
“Mjini” Patrick alijibu.
“Nitawapelekeni” Mzee Masharubu aliwaambia.
Uso wa mzee Masharubu ulikuwa ukionekana kuwa na tofauti kubwa. Hasira zote ambazo alikuwa nazo katika kipindi kichache kilichopita hazikuonekana tena, kwa wakati huo uso wake ulikuwa umetawaliwa na tabasamu pana.
Patrick na Azizi wakaonekana kuishangaa hali ambayo alikuwa nayo mzee Masharubu, hawakujua furaha yake ilikuwa imetokea wapi na wakati kipindi kichache kilichopita alikuwa amefula kwa hasira. Moja kwa moja akawachukua na kuwaingiza katika daladala yake huku akiwa amewaweka katika viti vya pale mbele.
Muda wote uso wake ulikuwa ukionyesha tabasamu. Akamuita mwanamke ambaye alikuwa akiuza mandazi na kuwanunulia mandazi Patrick na Azizi. Wote wakabaki wakishangaa, kila walipokuwa wakijiuliza juu ya furaha ya ghafla aliyokuwa nayo mzee Masharubu, walikosa jibu.
“Msijali. Nitawasaidia kama watoto wangu”Mzee Masharubu aliwaambia huku akiongeza zaidi tabasamu.
Abiria walizidi kuongezeka ndani ya daladala ile. Matenga yaliwekwa juu ya gari lile huku garini kukiwa kumetawaliwa na harufu kali ya shombo ya samaki. Abiria walipojaa ndani ya daladala ile, dereva, mzee Masharubu akawasha gari na kuliondoa mahali hapo. Kadri sekunde zilipokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo furaha ya mzee Masharubu ilivyozidi kuongezeka.
“Siamini.........!” Mzee Masharubu alijisemea moyoni huku tabasamu pana likizidi kuonekana usoni mwake

Je, nini kitaendelea?
Je, mzee Masharubu ana lake lipi?
Tukutane Ijumaa hapahapa.

No comments

Powered by Blogger.