ad

ad

‘Mtoto wa Nyani’ Apigwa Kifungo Cha Maisha Jela



Dar es Salaam. Baraka Joshua, maarufu kwa jina la ‘Mtoto wa Nyani’, jana hakuwa na la kujitetea katika kesi ya kulawiti mtoto wa miaka tisa na mahakama ikampa kifungo cha maisha jela.

“Sina cha kujitetea,” alisema Joshua mwenye umri wa miaka 23 baada ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Ilala, Catherine Kiyoja kumtaka ajitetee ili chombo hicho cha haki kimfikirie kumpa adhabu nafuu.
‘Mtoto wa nyani’ alipatikana na hatia ya kubaka na kulawiti mtoto wa miaka 9, ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Kimanga.


Katika shtaka la kwanza la kulawiti, Joshua atatumikia kifungo cha maisha jela huku kwa shtaka la pili la kubaka atatumikia kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kuchapwa viboko sita.


Hukumu hiyo ilitolewa jana mahakani hapo na Hakimu Kiyoja baada ya kuridhishwa na hoja za ushashidi zilizotolewa na upande wa mashtaka ambao ulikuwa na mashahidi watano pamoja na kielelezo kimoja.


Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Kiyoja alisema adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa wengine na kwamba Joshua alifanya kosa hilo akiwa na akili timamu.


“Ulifanya vitendo hivyo ukiwa na akili zako timamu na siyo kwamba ulifanya ukiwa umerukwa na akili kwa kisingizio cha kuishi na wanyama,” alisema Hakimu Kiyoja.
“Pia ni kitendo ambacho umekifanya mara nyingi kwa mtoto huyo hivyo ulikuwa ukitambua vyema.”
Kabla ya adhabu hiyo kutolewa wakili wa Serikali, Munde Kalombola aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwa kitendo cha unyanyasaji wa kijinsia kilichomsababishia mtoto huyo kuathirika kisaikolojia ili iwe fundisho kwa wengine .


Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Joshua alikuwa akikabiliwa na makosa mawili ambayo ni kumbaka na kumlawiti mtoto wa miaka tisa, ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kimanga.
Joshua alitenda kosa hilo Mei 17, 2016 akiwa eneo la Shule ya Msingi Tabata Kimanga, ambako alimbaka na kumlawiti mtoto huyo wa miaka tisa.


Ushahidi ulieleza kuwa, Joshua alikuwa akimwingilia kinyume na maumbile mtoto huyo mara kwa mara.
Eveline Nzagwi (42), ambaye ni daktari msaidizi wa Zahanati ya Tabata Shule, alidai kuwa alibaini misuli inayokaza sehemu ya haja kubwa ya mlalamikaji ikiwa imelegea kutokana na kuingiliwa.
Shahidi huyo, ambaye ana uzoefu wa miaka mitano katika fani ya udaktari, alieleza kuwa uchunguzi wake ulionyesha kuwa uke wa mtoto huyo ulikuwa umefunguka kutokana na kuchezewa.
“Yule mtoto tulimpima vipimo vyote, ikiwamo kipimo maalumu cha kupima sehemu za siri na kukuta hana maambukizi na hajaingiliwa ukeni.


“Lakini tulivyompima sehemu ya haja kubwa tuligundua kuwa sehemu hiyo ina uwazi mkubwa kiasi kwamba hata ukiingiza vidole viwili vinapita bila tatizo lolote na hapo tukabaini kuwa mtoto huyo alikuwa anaingiliwa kinyume na maumbile yake kila mara,” alidai shahidi huyo.
Naye shahidi wa pili, Christina Temu ambaye ni Mwalimu wa Shule hiyo, alisema kuwa siku moja alikuwa akipita katika moja ya majengo ambayo hayajamalizika kujengwa shuleni hapo na kumuona, Joshua akiwa amemkumbatia mtoto huyo huku akimbusu na mara baada ya kuwaona wote wawili walikimbia huku akikiri kumuona Joshua.


“Niliahirisha safari na kurudi shuleni ambapo niliwashirikisha walimu wenzangu na kisha baada ya hapo niliwaagiza wanafunzi kuwatafuta Joshua pamoja na mtoto huyo na kweli mara baada ya kuwahoji mtoto alikiri kufanyiwa kitendo hicho na Joshua,” alisema Shahidi huyo.




CHANZO: MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.