SI KITU BILA PENZI LAKO-09

NYEMO CHILONGANI
0718069269
Alikuwa na umbo namba nane, uso wake ulikuwa mwembamba. Mwendo wake haukuwa wa kasi, alikuwa akitembea taratibu kana kwamba alikuwa akiogopa kujikwaa. Miguu yake ilikuwa ikimtamanisha kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia machoni mwake.
Uso wake ulikuwa mzuri kiasi ambacho hakukuwa na mvulana ambaye alidiriki kumwangalia mara moja msichana huyu ambaye alionekana kuwa na uzuri wa peke yake. Alipokuwa amenuna, alionekana mzuri, alipokuwa amekasirika bado alikuwa akionekana mzuri, kila alipokuwa akicheka, uzuri wake ulikuwa ukiongezeka maradufu.
Katika maisha yake alijitambua kwamba alikuwa mzuri na alijua sana kama angepata usumbufu mkubwa kutoka kwa wavulana mbalimbali ambao walikuwa wakiishi mtaani kwao. Mawazo yake ndiyo ambayo yalijenga picha kamili ya baadae. Wavulana wengi walikuwa wakimtaka kimapenzi msichana huyu ambaye alikuwa na vishimo viwili mashavuni mwake, vishimo ambavyo vilikuwa vikionekana kila alipokuwa akicheka au kutabasamu.
Msichana huyu hakuwa na doa lolote mwilini mwake, aliishi kama yai nyumbani kwao huku akipata malezi ambayo yalimfanya kujitenga kabisa na wavulana. Kusimamishwa na kutongozwa ndio ilikuwa sehemu ya maisha yake ambayo aikuwa akiishi lakini kamwe hakumtukana mwanaume ambaye alikuwa akimtongoza.
Kila alipokuwa akiambiwa maneno matamu ya mapenzi, alibaki akicheka na kutabasamu tu hali ambayo iliwapa moyo wavulana wengi, lakini kitu cha ajabu, jibu lake lilikuwa tofauti na tabasamu lake. Wavulana walitumia njia zote kuwa na msichana huyu shuleni lakini hakukuwa na mvulana yeyote ambaye alibahatikia kuwa rafiki yake.
Wanafunzi wengi wa kiume walikuwa wakitembelea shule ya sekondari ya Mbezi High huku sababu kubwa ikiwa ni kutaka kumuona msichana huyu ambaye alikuwa akisifika kwa uzuri kuliko msichana yeyote katika shule zote za Dar es Salaam.
Msichana huyu alikuwa akivutia kupita kawaida, alionekana kama msichana wa ndoto ambaye wala hakuwa akiishi katika ulimwengu huu. Kila mvulana ambaye alibahatika kukutana nae, hakika alikiri nafsini mwake kukutana na msichana mzuri ambaye kamwe asingeweza kukutana na msichana kama huyo maishani mwake.
Alijipenda na kujithamini, hakutaka kumpa mvulana mwili wake auchezee. Muda mwingi alikuwa akishinda chumbani kwake akijisomea hali ambayo ilikuwa ngumu sana kumuona mitaani. Halikuwa jambo la kushangaza kama tu wavulana wa mtaani kwao walikuwa wakimuona msichana huyo mara moja kwa wiki.
Kila siku alikuwa akiepelekwa shuleni kwa gari na kurudishwa na gari. Ni mara chache sana alikua akielekea dukani, sehemu ambayo wanaume walipata nafasi kumsimamisha na kuanza kuongea nae.
Wavulana walikuwa wakigombana mitaani kwa sababu yake ingawa hakukuwa na mvulana yeyote ambaye alibahatika hata kumshka mkono wake. Misele nyumbani kwao haikuisha, kila siku wavulana walikuwa wakipitapita nyumbani kwao ili mladi tu kumuona.
Msichana huyu alipata wakati mgumu pale alipofungua akaunti yake katika mtandao wa Facebook. Ingawa hakuwa ameweka picha yake, watu wengi walikuwa wakimuomba urafiki kiasi ambacho alipata marafiki zaidi ya elfu tano ndani ya mwezi mmoja tu huku idadi kubwa ikiwa wavulana.
Kila siku wavulana walikuwa wakimtumia meseji mbalimbali za kumtaka kuweka picha yake kwani wao walikuwa wakisikia sifa zake tu. Akaamua kuiweka picha yake ambayo kwake yeye aliiona kuwa picha mbaya kuliko zote.
Picha ile ikaonekana kuleta kizaazaa, kila mvulana alikuwa nayo katika kompyuta yake huku wengne hadi wakiiweka katika simu zao. Alionekana kuwa na uzuri wa tofauti kabisa kabisa, alionekaa kuwa kama mwanadamu ambaye hakuzaliwa katika dunia hii.
Alilelewa vizuri na wazazi wake. Baba yake alikuwa mchungaji wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Kinondoni alipokuwa akiishi huku mama yake akiwa Mhasibu katika Benki ya CRDB. Msichana huyu alikuwa akiishi katika mazingira ya dini, Biblia ndicho kikawa kitabu ambacho alikuwa akikipenda sana kukisoma.
Kila siku alikuwa mtu wa kusali chumbani kwake akimuomba Mungu Awe nae katika maisha yake, Amlinde na kumuongoza katika njia ambayo alipaswa kwenda. Dini ndio ambayo ilikuwa ikimuongoza msichana huyu ambaye kadri siku zilivyokuwa zikiendelea kwenda mbele na ndivyo uzuri wake ulivyozidi kuongezeka.
*****
Bado safari ya kuelekea Mwanza Mjini ilikuwa inaendelea. Muda wote mzee Masharubu alikuwa akionekana kuwa na furaha. Utajiri ulionekana kuanza kumnyemelea, maisha ya kimasikini ambayo alikuwa akiishi aliyaona kuwa na mwisho wake siku hiyo.
Mara baada ya kufika Mjini, moja kwa moja akawachukua Patrick na Azizi na kuanza kuelekea nao katika mghahawa ambao ulikuwa karibu kwa ajili ya kupata kifungua kinywa pamoja nao. Patrick na Azizi bado walikuwa wakiendelea kujiuliza maswali vichwani mwao juu ya furaha ambayo alikuwa nayo mzee Masharubu lakini hawakupata jibu lolote lile.
“Mnataka kazi?” Mzee Masharubu aliwauliza mara baada ya kumaliza kunywa chai.
“Ndio. Tunahitaji kazi mzee, tunaomba utusaidie” patrick alimwambia mzee Masharubu huko nyuso zao zikionyesha kweli kwamba walikuwa wakihitaji kazi.
Mzee Masharubu akaanza kuondoka nao kuelekea nao pembezoni mwa ziwa Viktoria, katika sehemu ambayo ilikuwa na mitumbwi mingi. Akawaambia wasubiri nje ya kibanda ambacho yeye akaingia ndani na baada ya muda, akatoka huku akiongozana na mwanaume mmoja aliyekuwa na ndevu nyingi nyeupe.
Mzee yule akaanza kuwaangalia na kujitambulisha kuwa aliitwa mzee Baku, mzee maarufu ambaye alikuwa akimiliki mitumbwi mingi ya kuvulia samaki usiku. Akawahakikishia kuhusu kazi ambazo walitakiwa kufanya na kupewa malipo mazuri.
Patrick na Azizi hwakuonekana kuamini hata kidogo, kupata kazi kwa haraka sana kulionekana kuwafurahisha kupita kiasi. Wakabaki wakikumbatiana kwa furaha, hawakuamini kama nao walikuwa wakielekea kufanya kazi na kuanza kulipwa mshahara.
Mara baada ya utambulisho ule, mzee Masharubu na mzee Baku wakarudi ndani ya kibanda kile huku wakiwaacha Patrick na Azizi wakiwa na furaha kubwa kupita kiasi. Wakaelekea mpaka katika chumba ambacho waliamini hakukuwa na mtu ambaye alkuwa akiwasikia.
“Kwa hiyo? Nimekuletea mizigo miwili ya bureeee...” Mzee Masharubu alimwambia mzee Baku.
”Chukua milioni mbili kwanza” Mzee Baku alimwambia.
“Acha biashara ya kitoto wewe. Kwani nimekuletea gunia la mkaa hapa!”
“Nitakupa nyingine baada ya kazi kufanyika”
“Mtaifanya lini sasa?”
“Leo usiku”
“Sawa”
Hayo yalikuwa mangezi mafupi ambayo yalikuwa yameongelewa ndani ya chumba kile. Walipokubaliana, mzee Masharubu akatoka na kuondoka huku akiwaacha Patrick na Azizi wakiwa kama waajiriwa wapya katika sehemu hiyo ambayo ilihusika katika uvuvi wa samaki katika ziwa hilo.
Mzee Baku alijitahidi kufanya kila kitu ambacho kilikuwa kinawezekana kuwafanyia ili wasiweze kugundua ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea mahali hapo. Kila mfanyakazi ambaye alifika mahali hapo, Patrick na Azizi walitambulishwa kama wafanyakazi wapya.
Uchangamfu ambao ulitolewa kwao na wafanyakazi wengine kuliwafanya kujisahau kabisa, wakaonekana kumzoea kila mtu kupita kawaida, hawakuwa na hofu hata kidogo, walimuona kila mfanyakazi kuwa kama ndugu zao ambao walitoka nao kutoka Shinyanga.
Siku hiyo ilionekana kuwa ya furaha kwao, walikula na kunywa mpaka kuacha chakula. Hawakuwahi kuishi maisha ya furaha katika maisha yao kama siku hiyo. Walijisikia kuwa katika hali ya tofauti sana ambayo wala hawakuwa wameitegemea kabla.
Muda ulizidi kwenda mbele, huku masaa yakizidi kusogea. Wote walitaarifiwa kwamba kazi ingeanza siku hiyo hiyo. Ili kuwavutia zaidi kazini, mzee Baku akawagaiwia shilingi elfu tano kila mmoja, fedha ambazo zilizichanganya akili zao kupita kiasi.
Walitaarifiwa kwamba nao walitakiwa kwenda ziwani usiku kwa ajili ya kuvua samaki pamoja na wavuvi waliokuwa chini ya mzee Baku. Ingawa mara ya kwanza walikuwa akiogopa, waliwekwa chini na kutolewa woga wote waliokuwa nao.
“Kwanza hakikisheni wanapanda mitumbwi tofauti” Mzee Baku aliwaambia vijana wake.
“Ndio”
“Na hakikisheni wasijue kitu chochote kile. Mganga alikuja na kunipa hii dawa. Kazi inatakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo. Damu zao zinahitajika sana” Mzee Baku aliwaambia.
“Sawa mzee”
Vijana wale wakaondoka na kuelekea nje ya nyumba ile ambako wakaachukua Patrick na Azizi na kuwapa makoti mazito. Wakapandishwa katika mitumbwi tofauti na kisha safair ya kuanza kuelekea ziwani kuanza.
Lugha ambayo ilikuwa ikitawala mahali hapo ni Kisukuma, lugha ambayo Patrick na Azizi hawakuelewa kabisa. Mitumbwi ikazidi kwenda zaidi na zaidi huku wakiziandaa nyavu zao kwa ajili ya kuzitupia ziwani. Taa zao za chemri zilikuwa zikiendelea kuwaka katika boti zile ambazo ziliuwa mbali mbali.
Kisukuma kilizidi kuongelewa mtumbwini mule, Patrick hakuwa akielewa kitu chochote kile. Nyavu zikashushwa, kijana mmoja akachukua mfuko wa nailoni ambao ulikuwa na vitu kadhaa ndani yake. Patrick alikuwa akifuatilia kila kitu, hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule, alionekana kumuamini kila mtu mtumbwini humo.
Mtumbwi ulifika mbali sana, kila upande ambao alikuwa akiangalia hakuona kitu. Mtumbwi ambao alikuwa Azizi pamoja na wavuvi wengine haukuwa ukionekana tena machoni mwake. Patrick akanza kuogopa, hali ya kutisha ziwani ikaonekana kuanza kumtia hofu.
Mawimbi yalikuwa yakipiga kwa mbali, hali ya ziwa ilionekana kuwa nzuri kuliko siku nyingine ambapo maimbi makubwa yalikuwa yakipiga. Wavuvi wale walikuwa wakimwangalia Patrick ambaye tayari alikuwa akionyesha wasiwasi mkubwa.
Kwa kutumia mwanga wa mwezi walikuwa wakionana vizuri katika mtumbi ule. Uso wa Patrick ambao ulikuwa umejaa wasiwai ulikuwa ukionekana vizuri kwa kila aliyekuwa akimwangalia. Mvuvi yule ambaye alichukua mfuko ule wa nailoni akaufungua na kutoa kikaratasi kimoja ambacho kilionekana kufungwa vitu fulani kwa ndani.
Ndani ya kikaratasi kile kulikuwa na unga mweusi. Akaumimina mkononi mwake na kisha kuanza kuongea maneno ya taratibu kwa sauti ya chini ambayo alihakikisha hakukuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kumsikia. Alipomaliza, akayapeleka macho yake usoni mwa Patick. Kwa kasi ya ajabu, akampulizia unga ule machoni na kisha kumsukuma ziwani.
Patrick akaanza kutapatapa kwa kurusha mikono yake katika kila upande. Kila alipotaka kuzama, alijitahidi kuulegeza mwili wake na kubaki juu. Mtumbwi ule ulikuwa umekwishaondoka mahai pale. Patrick alikuwa akipiga kelele lakini hakukuwa na dalili ya mtu yeyote au mtumbwi ziwani pale.
Patrick akaanza kuchoka, baridi lilikuwa likimpiga kupita kiasi. Akaonekana kukubaliana na hali ambayo ilikuwa ikimkumba mahali pale, ghafla akaanza kuzama. Patrick alijaribu kujirudisha juu lakini hakuweza, alizidi kuzama kwenda chini zaidi mpaka pale alipoanza kujiona akiishiwa pumzi.
Macho yake yakaanza kupoteza muelekeo, mara akaanza kuona giza na baada ya sekunde kadhaa, hakujua kitu chochote ambacho kiliendelea baada ya hapo, alikuwa nusu ya mfu.
*****
Kijana Hidifonce alikuwa akionekana kijana mtanashati kuliko vijana wote ambao walikuwa wakiishi Kinondoni. Kila siku alikuwa akionekana msafi pasipo kujalisha kama alikuwa akikaa nyumbani au alikuwa akielekea ofisini.
Hakuwa mtu wa kushinda nyumbani, kazi ya uasibu ambayo alikuwa akiifanya bandarini ndio ambayo ilikuwa ikimfanya kuwa bize kupita kiasi. Muda wake wa kukaa nyumbani ulikuwa ni Jumamosi na Jumapili tu. Kila kitu ambacho kilikuwa kikitokea mtaani kwao wala hakuwa akipata taarifa.
Ingawa muda mwingi alikuwa akiutumia kazini lakini Hidifonce alikuwa akijitahidi kuongea na vijana wenzake hasa alipokuwa akirudi nyumbani.
Utanashat wake pamoja na ucheshi ambao alikuwa nao ulimfanya kupata marafiki wengi mtaani kwao ambao mara kwa mara alikuwa akikaa nao na kubadilishana mawazo.
Hakuwa na mpango wa kuoa katika kipindi hicho, bado alihitaji muda wa kukaa peke yake zaidi, wasichana hawakuwa sehemu ya maisha yake kwani kila alipokuwa akielekea kazini, alikuwa akikutana nao na ambao walikuwa wazuri kuliko wale ambao alikuwa amewazoea kuwaona mtaani.
Kila alipokuwa akikaa na marafiki zake alikuwa akilisikia jina la msichana mmoja likitajwa sana katika midomo ya vijana hao, msichana huyu alikuwa Mary Christopher, binti wa mchungaji Christopher wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Kinondoni.
Sifa zilikuwa nyingi kiasi ambacho nae akatamani kumuona msichana huyo ambaye alikuwa ameteka mioyo ya vijana hao. Kushinda ofisini na kurudi usiku ndiko ambako kulimfanya kutokumuona msichana huyo ambaye aliuhisi uzuri wake kuwa mkubwa kupita kiasi.
Kila siku alikosa raha kila alipokuwa akisikia sifa za Maria. Akaanza kumtengeneza Maria wake kichwani kwake, umbo zuri la kuvutia pamoja na sura nzuri ilikuwa ni picha nzuri ya Maria ambayo aliitengenaza kichwani mwake.
Kila Jumamosi na Jumapili ambazo alikuwa akishinda nyumbani, Maria hakuwa akionekana mtaani jambo ambalo lilimfanya kila siku kuwa na shauku ya kumuona Maria. Tayari akili yake aliiona kuanza kumpenda msichana ambaye wala hakuwa amemuona machoni mwake.
Siku ziliendelea kukatika huku Maria akizidi kuzungumziwa kila siku. Kila siku Hidifonce ambazo alikuwa akirudi kutoka nyumbani, sifa za Maria zilikuwa zikiongezeka. Hakuwa na jinsi hali iliyompelekea nae kuanza kwenda kanisani katika kanisa lile ambalo alikuwa akisali Maria.
Huko napo wala haikuwezekana kumuona Maria, kwa kuwa alikuwa muimbaji wa kikund kimoja cha kwaya kanisani hapo, hakuwa akionekana kwa urahisi kwani mara kwa mara walikuwa wakiitwa katika makanisa mengine kwa ajili ya kumsifu Mungu.
Hidifonce bado alionekana kuchanganyikiwa, kiu aliyokuwa nayo ya kutaka kumuona Maria iliendelea kumkamata kila siku. Macho yake yalikuwa na kiu ya kutaka kumuona Maria ambaye alisadikiwa kuwa mzui kuliko wasichana wote ambao walikuwa wakiishi Kinondoni.
“Unasema haujawahi kumuona Maria?” Kijana mmoja alimuuliza Hidifonce ambaye alikuwa pamoja nao.
“Ndio. Kwani yuko vipi? Uzuri wake uko vipi?’ Hidifonce aliuliza.
“Hauelezeki. Yaani kama nikikwambia ni mzuri sana naona kama nakudanganya. Yeye ni mzuri hata zaidi ya sana” kijana yule alitoa jibu ambalo lilimfanya Hidifonce kuwa na hamu zaidi ya kumuona Maria.
Hidifonce alikuwa akijilaumu pasipo kuwa na sababu, kitendo cha kutokumuona Maria machoni mwake kilionekana kuwa kama kosa kubwa ambalo hakuwahi kulifanya maishani mwake. Akaanza kujitahidi kurudi nyumbani apema ili mladi tu amuone Maria lakini napo haikuwezekana.
“Maria mwenyewe huyo hapo” kijna mmoja alisikika akiwaambia wenzake.
Kwa kasi ya ajabu, Hidifonce akayainua macho yake na kumwangalia Maria. Mapigo ya moyo wake yalikuwa yakidunda kwa kasi kutokana na mzunguko wa damu yake kuwa mkubwa. Hidifonce hakuonekana kuamini kabisa kama msichana ambayealikuwa akipita mbele yake alikuwa binadamu au malaika ambaye alishushwa duniani.
Mshtuko ukampata Hidifonce, macho ya Maria yalikuwa hayajatoka usoni mwake. Walibaki wakiangaliana kwa muda huku Maria akiendelea kupiga hatua kulifuata geti la nyumba yao. Hidifonce hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea, Maria akalifungua geti na kabla hajalifunga, akayapeleka macho yake usoni mwa Hidifonce na kisha kufunga geti.
Kila mmoja alibaki akiwa ameduwaa. Hawakuelewa ni kwa nini Maria na Hidifonce walikuwa wakiangaliana namna ile, tena katika mwangalio ambao ulikuwa umejaa mahaba mazito. Hidifonce alibaki kimya kwa muda huku akianza kumfikiria Maria.
Kabla ya kumuon Maria, tayari alikuwa amemtengeneza Maria mzuri kichwani mwake lakini kwa Maria ambaye alikuwa amemuona, alikuwa mzuri hata zaidi ya Maria yule ambaye alikuwa amemtengeneza kichwani mwake.
“Mbona umeangaliwa sana Hidifonce?” Hamidu alimuuliza Hidifonce.
“Hata mimi mwenyewe nashagaa. Labda ananifahamu” Hidifonce alijibu.
“Hilo si tatizo, na wala sina tatizo na kukuangalia. Ila mimi najaribu kuutafakari ule muangalio. Macho yalikuwa yamekaa kimahaba kabisa alipokuwa akikuangalia” Hamidu alimwambia Hidifonce.
Siku ziliendelea kukatika. Hidifonce hakuweza kumuona tena Maria ingawa moyo wake ulikuwa na hamu kubwa ya kumuona. Majukumu kazini yalikuwa yamembana kupita kiasi. Kilasiku muda wake wa kurudi nyumbani ulikuwa usiku.
“Nitamtafuta tu, nimetokea kumpenda sana binti huyu” Hidifonce alijisemea.
Je, nini kitaendelea?
Post a Comment