Diamond anavyojiharibia, Anavyojiangusha kutaka kulazimisha makosa ya viongozi kuwa utamu kwa wananchi
Na Saleh Ally
NARUDI
nyuma kidogo, nataka kukumbusha namna ambavyo niliwahi kuandika
kuhusiana na namna ambavyo mwanamuziki Nasibu Abdul, maarufu kama
Diamond, kwamba ameanza kukosea vitu kadhaa, hasa kuiga video za wasanii
wengine.
Nilieleza
kwa mifano ya picha namna ambavyo Diamond aliiga karibu kila kitu
kutoka katika video ya msanii mmoja, kuweka kwenye video yake. Halafu
akarudia namna hiyo baadaye, jambo nililoliona ni la kustaajabisha
kabisa kwa kuwa wimbo huo aliouiga haukuwa hata na miaka miwili sokoni!
Baada
ya kuandika, nikaweka kila kitu kwa mifano. Kilichofuata ni baadhi ya
watu walio na Diamond kuanza kulalama kwamba ninamsakama.
Mbaya
zaidi, mwandishi mmoja wa Mwananchi ambaye ni kati ya watu
niliowafundisha namna ya uandishi bora wa uandishi wa burudani
alinifuata na kuhoji mbona “natumiwa”, kumsakama Diamond. Nilimuuliza
maswali kupitia makala niliyoandika, hakuna alichojibu!
Baadaye niligundua ameingia kwenye mkumbo wa zile “Team”, jambo ambalo ni baya kabisa kwa mwandishi.
Lakini
hivi karibuni, Diamond alikosolewa kwa nia njema kabisa kuwa vizuri
akawa anafanya shoo za nyumbani kwa ajili ya watu wake ambao ndio
wanaomfanya leo asikike kote duniani.
Mhamasishaji
na mjasiriamali, Eric Shigongo alishauri hivyo akitaka Diamond na
uongozi wake, kupunguza bei za shoo kwa mapromota ili nao watoze
viingilio vya chini kwa Watanzania. Nalo hilo likawa kosa, Meneja wake
Babu Tale, akacharuka kwamba kazi yake inaharibiwa akiamini eti, Diamond
anashambuliwa!
Baada
ya hapo akaanza vitisho eti atamuandika vibaya Shigongo mtandaoni, kwa
madai yeye ni maarufu huko mtandaoni kwa kuwa ana watu milioni 1
wanaomfuatilia! Akafanya hivyo, hakukuwa na faida yoyote kwake, zaidi ya
yeye kushambuliwa, watu wakiamini hakuelewa!
Tale
hakuwa amejibu hoja hata kidogo kuhusiana na kilichoandikwa kama
ilivyokuwa awali, zaidi ya kusema maneno mengi akitoa data za uongo huku
akitengeneza filamu eti katishiwa kuuawa.
Hii
inaonyesha kiasi gani Diamond amezungukwa na watu wanaoweza
kumtengenezea mazingira ya kuwa hawezi kushauriwa, hawezi kuhojiwa, ni
mtu anayejua sana na wao wanajua kila kitu cha muziki wakati rekodi
zinaonyesha waliofaulu zaidi ni waliokubali kukosolewa.
Picha
inayotengenezwa, kumueleza jambo Diamond kwa nia nzuri ni kumshambulia.
Picha inayotangulizwa, chochote atakachofanya Diamond aachwe, “yeye ni
yeye.” Mimi ninaamini hilo halitakuwa na nafasi na kwa kuwa ni msanii wa
Tanzania, ataambiwa na mimi safari hii naendelea kumuambia bila ya hofu
ya huo mtandao wa watu milioni moja wa Babu Tale na vizuri atakayetaka
kuzungumza na mimi, twende kwa hoja ili tujenge.
Kutishiana
mtandaoni eti watu watakutukana ni mambo ya kipuuzi ambayo wakati
mwingine hupaswi kuyasikia yakizungumzwa na mtu unayeamini amefikia
kiwango cha kuitwa kiongozi.
Diamond ametoa wimbo mpya uitwao “Acha Nikae Kimya”. Tayari mashabiki wengi wa muziki wameanza kumshambulia Diamond mitandaoni.
Nimeona
wakishambulia katika hali ambayo inaonyesha wazi kuwa wamekerwa na
uamuzi wake wa kutoa wimbo ambao ukiusikiliza kwa makini umelenga
kumsafisha mkuu wa mkoa ambaye yuko katika sakata la vyeti.
Lengo
ni kuona mkuu wa mkoa huyo anarejea katika heshima aliyopewa na
wananchi hapo awali, lakini baadaye wakaichukua wananchi hao baada ya
kuona hawastahili kumpa hasa baada ya kushindwa kulimaza suala
walilohoji naye akashindwa kujibu na zaidi ikawa ni kutishiana tu.
Ndani
ya wimbo huo unaoonyesha wazi unalenga kutengeneza mazingira ya kupoza
hali iliyopo mfano, kama kile kipande anachosema: “Nyumbani nafungua
geti, niende kwa Mangi kununua supageti, napewa za chini ya kapeti, kuna
redio imevamiwa eti.”
Najua ukimuuliza atasema alikuwa anatafuta vina, lakini baada ya redio imevamiwa, neno eti, linamaanisha hakuna uhakika.
Hii
yote ni kuonyesha kuwa hakuna redio iliyovamiwa kama ambavyo wengi
wamekuwa wakifikiria. Kwa waliovamiwa na walio karibu yao au
waliounganisha machungu katika hili ni sawa na kuwatonesha kidonda.
Najua
ndani ya waandishi wenyewe wako walio tayari kugawanya machungu. Lakini
ukweli mwenye akili timamu hakuna anayeweza kuunga mkono chombo cha
habari kuvamiwa kwa visingizio visivyokuwa na msingi. Hata Diamond,
amekuzwa kufikia alipo na vyombo vya habari hata anavyovidharau akaamini
vinazidiwa na mtandao, ndiyo vilimpa nafasi watu wakamjua!
Kama hiyo haitoshi, kuna sehemu anaimba hivi;
“Napita
kwenye magazeti, nakuta rundo la watu wameketi, badala ya kutafuta
senti, wanabishana tu mambo ya vyeti. Acha nikae kimyaaa.”
Hii ni kuonyesha kwamba hakuna sababu ya watu kubishana mambo ya vyeti na yeye anawashangaa.
Lakini
hakumshangaa kiongozi ambaye ameshindwa kuweka vyeti vyake hadharani
baada ya kuonekana kuna walakini. Kiongozi ambaye ameshindwa kuonyesha
ni kiongozi thabiti ambaye alipaswa kuwa wazi na kuwathibitishia
wananchi wake wanachohoji.
Kama
unataka watu wawe safi, unataka watu wafuate taratibu, kanuni na
sheria. Vipi wewe umeshindwa kuthibitisha unavyo, uonyeshe? Vipi Diamond
anakubali kujiangusha aonekane anafurahia visivyo sahihi? Uko wapi
uongozi wake na unashindwa kuona hili? Kwa nini unaachia haya yapite na
kunipa mimi nafasi ya kuandika ili kesho wadai ndiye nilimshusha
Diamond?
Je,
Diamond yuko tayari kuwakandamiza wananchi wote ambao ndiyo wamekuwa
wakimsapoti yeye miaka yote kwa ajili ya kumfurahisha mtu mmoja?
Wale wanaomshambulia mitandaoni ni kuonyesha kuwa ni kosa kubwa kuamini una akili nyingi kuliko kila mtu.
Alichotakiwa Diamond ni kukemea vyanzo vya tatizo na si kuwakemea au kuwashangaa wale wanaotaka kuchukua chanzo cha tatizo.
Kama
Diamond ameamua kuingia kwenye “siasa nyepesi”, vipi Babu Tale haoni
kuwa anaharibu biashara yake? Vipi halalamiki au naye hayuko katika
kampeni ya kushika taulo na kufanya usafi wa waliojichafua wenyewe?
Halafu jiulize, huu mjadala si ulifungwa? Sasa Diamond anapouamsha anataka nini? Naye anatumika?
Mimi
nataka kuwa huru, nataka kuwa mwandishi ninayesema ukweli bila ya hofu
ya kutekwa au kuwekwa ndani eti kwa kuwa nimemuambia mtu fulani ukweli.
Nataka
kuwa huru na kusema ukweli kwa lengo la kuweka mambo sawa na
kurekebisha taifa langu bila ya kuogopa eti mtu mzima mwenye akili zake
atanitishia kuniweka nitukanwe mtandaoni.
Nasema
sitaogopa kwa sababu viongozi wa mikoa waliopewa dhamana ya kutuongoza
wanataka kututisha kwa kuwa wana uwezo wa kukuweka ndani mwandishi hasa
wale wanaoonyesha si wapambe wao.
Diamond
aachane na “siasa nyepesi”, anatakiwa kuusoma upepo na kuwa
“intelligent” badala ya kukubali kutumiwa kusafisha mkono wa wenzake
huku wa kwake ukijaa masizi.
Kuna
ule msemo wa sanaa usemao hivi: “Music expresses that which cannot be
said and on which it is impossible to be silent.”. Muziki unaweza
kufafanua kile ambacho hakiwezi kuzungumzwa, tena katika kipindi ambacho
haiwezekani kuwa kimya.
Huenda
ulikuwa wakati mzuri kwake Diamond kuchagua kukaa kimya kweli, kuliko
kusema yuko kimya huku akijaribu kuonyesha Watanzania hawawezi kuelewa.
Badala
ya kukimbilia udhaifu ili kufurahisha nafsi ya mtu, kama angetaka
kusema, angeonyesha ni imara kueleza kile ambacho hakielezeki katika
kipindi ambacho watu wako kimya.
Wanaokasirika wanajua wanataka kufanywa wapuuzi. Waliolalamika wanakasirishwa na kuonyesha wanacholalamika wao ni kazi bure.
Mimi
nashangazwa na Diamond anayetaka kubomoa matofali ya ukuta wa nyumba
yake aliyoijenga kwa shida huku akitaka kujenga ukuta wa jirani
aliyeubomoa wa kwake baada ya kulewa sifa.
Muziki
kila mmoja ana mwisho wake, hakuna aliyewahi kutamba milele. Nimepata
bahati ya kuwaona wanamuzi wengi maarufu nikiwa mwandishi chipukizi na
mwandishi bora wa burudani wa nchi hii.
Nakumbuka
ufalme wa Mr 2, wakati huo tukimuita 2Proud, usimsahau Profesa Jay.
Nakumbuka ufalme wa miaka ya Juma Nature, baadaye makundi ya TMK na East
Coast. Nakukumbusha umalkia wa Lady Jaydee. Najua hautakuwa umemsahau
Mr Nice.
Ufalme
unaweza kuwa wa muda mrefu au ukaporomoka haraka kulingana na mmiliki
wa ufalme mwenyewe. Ninaamini siku moja atakuja mfalme mpya au kipenzi
kipya cha Watanzania. Lakini ni vizuri Diamond akaepuka kuharibu kazi ya
Babu Tale na ikiwezekana kuhakikisha anajenga misingi mizuri ili
ukifika wakati wa kuondoka, aondoke kwa heshima. Wakati huo, Watanzania
watakuwa wakiendelea na mfalme mwingine na hayo ndiyo maisha bora.
SOURCE: CHAMPIONI

Post a Comment