Baada ya Kumaliza Makala yake ya Diamond na Wanaompeleka Shimoni, Shigongo Sasa Ahamia Kwa Ali Kiba
Mara baada ya kumaliza makala yake aliyoiita My Confession, iliyokuwa ikieleza watu watatu wanaompeleka shimoni mwanamuziki Diamond Platnumz ambapo aliwataja na mameneja wake Bab Tale na Sallam kuhusika, sasa Mwandishi wa vitabu Eric Shigongo ameamua kuhamia kwa mwanamuziki Ali Kiba na uongozi wake.
Makala hiyo mpya kuhusu Ali Kiba ameianza kupitia ukurasa wake wa Facebook pamoja na kwenye akaunti yake ya Instagram na kuipa kichwa cha habari 'USHAURI WANGU KWA ALI KIBA NA MENEJA WAKE NA WATANZANIA WENZANGU!'., Shigongo ameanza makala hiyo kwa kummwagia sifa Ali Kiba na uongozi wake huku akimtaka ajiulize siku atakapokuwa si maarufu tena kama ilivyotokea kwa Mr Nice, Inspector Haroun na wengine wengi atafanya nini?
Soma mwenyewe alichoandika Shigongo hapa chini;
USHAURI WANGU KWA ALI KIBA NA MENEJA WAKE NA WATANZANIA WENZANGU!
Kwanza kabisa nianze kwa kukiri kuwa sikuwahi kukutana na Ali kiba ana kwa ana mpaka miezi miwili iliyopita nikiwa katika Hotel ya Double Tree, iliyopo Masaki, Jijini Dar Es salaam.
Nilikwenda pale kwa ajili ya chakula cha mchana na mke wangu. Muda mfupi tu baada ya sisi kuingia walifika Ali Kiba na Meneja wake Christine Mosha (Seven) wakaja moja kwa moja kwenye kona tuliyokaa na kutusalimia.
Kitu cha kwanza nilichojifunza na kukipenda kwa Ali kiba ni unyenyekevu, kijana huyu ni mnyenyekevu mnoooo! Kitu hiki peke yake ukiachana na muziki wake kilinifanya nimpende Kiba. Walipoondoka mimi na mke wangu wote tulikiri KIBA NI MNYEYEKEVU NA NDIYO SABABU AMEFANIKIWA SANA KATIKA MUZIKI.
Tunapoongelea mafanikio ya Kiba kamwe hatuwezi kuacha kumpongeza meneja wake, hongera Seven. Msichana huyu mdogo ni humble, smart, intelligent and clever! Bila Shaka ndiyo siri kubwa ya mafanikio ya Kiba katika muziki.
Wiki chache baadae Ali kiba alishinda Tuzo ya MTV huko Africa Kusini na kuliletea taifa letu sifa kubwa sana! Sikuwepo uwanja wa ndege wakati wa mapokezi yake lakini Globaltv Online, walitengeneza ‘Documentary’ nzuri sana iliyoonyesha jinsi kijana huyo alipokelewa kifalme na mamia ya vijana, kuliko ambavyo hata timu yetu ya taifa hupokelewa, BRAVO KIBA.
Makundi ya vijana walikuwepo uwanja wa ndege kuonyesha mapenzi yako kwa Kiba, vijana wa kawaida, wanaishi maisha ya kawaida, wafanyabiashara ndogondogo, wanafunzi n.k. Hapakuwa na mfanyakazi wa CRDB, BOT ana Standard Chartered mahali pale! Sikuona aliyefunga tai na shati jeupe mahali pale.
Gari ya Kiba ilisukumwa, vijana wale walijichangisha elfu moja moja mpaka kutimiza pesa ya mafuta ya gari la Kiba! Hakika hii ni ishara ya upendo mkubwa kwa Kiba.
Leo nitamshauri Ali Kiba! Si kila mtu atataka ushauri, si kila mtu anapenda kushauriwa. Hata ukimwambia mlevi acha pombe, atakuchukia, hata ukimwambia mvuta sigara aachane na sigara kwa kuwa inaua, atakuchukia, kuchukiwa ni sehemu ya maisha yetu, haikuanza jana, juzi, na haitoishia kesho, bado itaendelea kuwa hivyo vizazi mpaka vizazi.
Baada ya kumshauri Diamond leo nataka nimshauri Ali Kiba. Sijui kama atafurahi au atachukia, ninafanya hivi kwa kuwa sitaki waache muziki hapo baadaye huku wakiwa hawana kitu. Sitaki baadaye mtu aseme kwamba kuna watu waliwatumia, wakaingiza pesa halafu wamewakimbia.
Baada ya kusema hayo hebu niongee kilichonisukuma kuandika hiki ninachokiandika, ni ushauri, Kiba na meneja wake wanaweza kuuchukua ama kuuacha! Si lazima, kama mhamasishaji wa watu kujiondoa katika umasikini ninaona kama ninao wajibu wa kumshauri Kiba nikiwa kama kaka, anko au Mtanzania mwenzake, naamini kwa hekima walizonazo Ali Kiba na meneja wake bila shaka watapata la kuchukua, yasiyofaa wataniachia mwenyewe.
Nampenda Kiba sana tu na ninajivuna sana kuwa Mtanzania mwenzake na ningependa kuona anafanikiwa zaidi katika kazi yake. Kama siwezi kufurahi mafanikio ya Watanzania wenzangu basi hakuna haja ya mimi kuzunguka huku na kule ndani na nje ya nchi yangu kuhubiri injili ya mafanikio, watu watoke kwenye umasikini unaolitesa taifa langu.
Haikutokea tu Ali kiba akawa anapendwa vile, la hasha, ni matokeo ya vitendo fulani ambavyo amekuwa akivifanya maishani mwake mpaka Akawavuta watu kumpenda! Mambo hayo hayo akiyaacha hata followers wa Instagram wanaomfanya ajisikie anapendwa leo wataondoka!
Ali kiba, meneja wake na Watanzania wenzangu lazima mnisikilize hapa; MAFANIKIO MAISHANI HUJA NA KITU NYUMA YAKE, mara nyingi kitu hicho huwa kuwapuuza na kuwadharau waliokufikisha ulipo. Kuwatenga bila kufahamu hao ndiyo wanunuzi wa kazi zako ama wasikilizaji wa muziki wako na wakikuachia tu utatumbukia shimoni na huo ndiyo utakuwa mwisho wako.
Ali kiba anapaswa kufahamu kwamba hawezi kuwa Champion for life, hata akiwa bora kiasi gani lazima siku moja atakuja mtu bora zaidi yake. Kabla ya Chris Brown alikuwepo Usher Raymond, kabla ya Rihanna alikuwepo Beyoncé, kabla ya Floyd Maywether alikuwepo Mike Tyson, kila zama na bingwa wake. Leo ni Kiba kesho atakuwa mwingine, swali la kujiuliza ni kwamba: SIKU ALI KIBA ATAKAPOKUWA NJE NANI ATABAKI NAYE?
Sasa hivi gari lake linasukumwa na anazungukwa na watu kila anakokwenda, lakini ipo siku atakuwa si maarufu tena kama ilivyotokea kwa Mr Nice, Inspector Haroun na wengine wengi!
Atafanya Nini kiba siku atakapokuwa anakaa kwenye meza hotelini viti vingine vyote havina watu? Hakuna mpambe? Au Meneja? Haya mambo yatatokea ndugu zangu....
NITAENDELEA JUMATATU SAA NNE NA NUSU...
Ujumbe huu unamhusu mtu yeyote unayemfaa! Ndiyo maana nimeuweka hapa usomwe na watu wote.
Hivyo ndivyo alivyomalizia Shigongo na kuahidi kuendelea siku ya Jumatatu.
Post a Comment