FUTA MACHOZI MPENZI-32
NYEMO CHILONGANI
Polisi walikuwa na akili, walijua fika kwamba ilikuwa ni lazima muuaji arudi tena ndani ya hospitali hiyo na kukamilisha kile alichokitaka kwani mara ya kwanza alipotaka kumuua Godson, hakufanikiwa.
Walichokifanya katika usiku wa siku hiyo ni kumtaka Dk. Sam amuhamishe Godson ndani ya chumba kile na kumpeleka katika chumba kingine kabisa pasipo madaktari wengine wala wazazi wake kufahamu.
Hilo likafanyika kwa haraka, hakukuwa na nesi aliyemwambia, daktari aliyemsaidia kumuhamisha Godson ndani ya chumba kile alikuwa Dk. Mshana ambapo wakaifanya kazi hiyo na polisi mmoja kuagizwa kwenda ndani ya chumba kile, alale kitandani, atakaposikia mlango unafunguliwa, basi ajifunike na kushika bastola yake.
Hilo ndilo lililofanyika kwa siku mbili. Wazazi wake hawakuruhusiwa kumuona kwa kisingizio kwamba hakuwa katika hali nzuri baada ya tukio la kutaka kumuua kufanyika.
Siku ya kwanza ikapita, ya pili ikaingia na ndipo siku ya tatu vijana wale wakarudi kwa ajili ya kufanya kile walichotaka kukifanya. Mpaka msichana huyo anaanguka, polisi alijua kwamba ulikuwa ni mchezo, alihisi kwamba alifanya hivyo kwa kuwa kuna mtu alitaka kuingia ndani ya chumba hicho, hakutaka kulizuia hilo, alichokifanya ni kumsaidia msichana huyo kisha kumpeleka sehemu.
Huku nyuma kijana yule akaingia ndani ya chumba kile, akakisogelea kitanda, mgonjwa aliyekuwa kitandani, alijifunika shuka mwili mzima, kijana yule hakujua kama mtu aliyelala alikuwa polisi, akamsogelea na kisha kuchukua sindano yake kwa lengo la kumchoma lakini kabla hajafanya lolote lile, akashtukia akidakwa mkono, shuka likatolewa, akapigwa na mshtuko baada ya kuona mdomo wa risasi ukimwangalia.
“Tulia hivyohivyo! Ukipiga kelele tu, nakumwaga ubongo,” alisema polisi huyo huku akimwangalia muuaji aliyekuwa akitetemeka.
“Nisamehe bro!” alisema huku akitetemeka.
Kabla hajafanya kitu chochote, akampiga pingu kijana yule, mkono mmoja ulifungwa pingu na sehemu nyingine ya pingu kufungwa kwenye kitanda kisha polisi yule kupiga simu.
“Nimempata!” alisema huku akimwangalia kijana yule kwa hasira.
“Muulize wenzake walipo tuwafanyie kazi sasa hivi,” ilisikika sauti upande wa pili na hivyo polisi yule kuanza kumuuliza mwanaume yule.
Alimwambia, hakutaka kumficha kwani aliambiwa kwamba kama angemficha basi ingekuwa hatari zaidi katika maisha yake. Akamwambia kwamba wenzake walikuwa nje, kwenye gari moja, Vitz yenye rangi ya bluu wakiwa wanamsubiri.
Polisi yule akawapa maelekezo wenzake ambapo wakaelekea huko na kweli kulikuta gari hilo ambapo wakalizunguka na kuwakamata vijana wawili waliokuwa wamebaki ndani ya gari hilo.
Kule ndani, kijana yule akatolewa, akafungwa pingu mikono yote kwa nyuma na kushikwa na kuanza kutolewa nje. Wazazi wa Godson na Melania walibaki wakishangaa, hawakuamini kile walichokiona, ilikuwaje ndani ya chumba alicholazwa kijana wao watoke wanaume wengine ambao hawakuwa wakiwafahamu?
“Imekuwaje?” aliuliza baba yake Godson.
“Huyu ndiye alitaka kumuua mwanao!” alijibu polisi.
“Mwanangu?”
“Ndiyo!”
Vijana wale wakachukuliwa na kupelekwa katika kituo cha polisi na kuambiwa kwamba kitu walichotakiwa kufanya kilikuwa kimoja tu, kumtaja mtu aliyekuwa amewatuma kufanya mauaji hayo.
Hawakusema, walibanwa sana lakini wakanyamaza, kila walipoulizwa swali hilo walibaki kimya kitu ambacho kwa polisi wa kituo hicho waliona kama wakidharauliwa.
“Kamuite Kunta Kinte,” aliagiza mkuu wa kituo hicho.
Ndani ya dakika mbili, kipande cha mwanaume kikaingia, alikuwa mweusi tii kama mtu aliyejipaka masizi, alijazia vilivyo, mikono yake ilikuwa mipana, uso wake ulikuwa mbaya mithili ya sokwe mtu.
Alisimama mbele ya mkuu wa kituo kile kwa heshima kubwa, alipiga saluti na kuibana mikono yake vilivyo. Akaambiwa kwamba vijana watatu waliokuwa mbele yake hawakutaka kujibu kile walichokuwa wanauliza.
“Acheni utani,” alisema mwanaume huyo huku akionekana kushangaa.
“Kweli tena!”
“Wanakataaje sasa?”
“Hata sisi tunashangaa!”
“Eti ni kweli mmekataa kujibu maswali?” aliuliza mwanaume yule huku akiwaangalia lakini vijana wale walikuwa kimya.
“Naombeni dakika tano tu! Watasema kile tunachotaka kukifahamu!” alisema mwanaume huyo, hakutaka kuwachukua wote, akamchukua kijana mmoja na kuingia naye kwenye chumba kilichoandikwa ‘Usipige Kelele’ mlangoni.
Ndani ya chumba hicho kulionekana kutokuwa sehemu salama, kulikuwa na michirizi ya damu, nyundo, mapanga, fimbo, beseni la maji, plaizi, taulo, kiti kilichokuwa na tundu kubwa sehemu ya kukalia na vitu vingine vingi kwa ajili ya kuwatesea watu waliokuwa makaidi.
Mlango ukafungwa na kilichosikia ndani ya dakika moja ni kelele za maumivu makali kutoka kwa kijana yule. Alikuwa akipiga kelele huku akimwambia mwanaume huyo kwamba alikuwa tayari kumwambia mtu aliyekuwa amewatuma.
“Najua utaniambia, ila sitaki uniambie sasa hivi, kwanza tuendelee kufanya mazoezi ya kijeshi,” alisikika mwanaume huyo lakini kijana yule alisisitiza kwamba alikuwa tayari kumwambia juu ya mwanaume aliyekuwa amewatuma kufanya mauaji yale.
Baada ya dakika kadhaa, wakasikia jina la Nicholaus likitajwa. Mwanaume huyo akaridhika, akafungua mlango na kisha kumtoa kijana huyo ambaye alipotolewa ndani ya chumba kile, akalala chini, mwili ulitapakaa damu na hata kusimama hakuweza.
“Mleteni mwingine!” alisema mwanaume huyo huku akichukua sigara yake na kuiwasha.
Wote watatu walipoingizwa ndani ya chumba hicho, kwa jinsi walivyopewa mateso, walimtaja mtu aliyekuwa amewatuma kufanya mauaji yale. Jina la Nicholaus likatajwa na kila mmoja hivyo walichotakiwa kufanya ni kuhakikisha kwamba mwanaume huyo anapatikana haraka iwezekanavyo.
****
Kila mtu alikuwa akimshangaa William, hakuwa akikumbuka kitu chochote kile na kila alipokuwa akizungumza, alizungumza kuhusu msichana Melania tu. Walimshangaa, alisahau kila kitu, hakumkumbuka mtu yeyote katika maisha yake zaidi ya watu wawili ambao alikuwa nao kwa karibu sana alipokuwa nchini Tanzania, mama yake na msichana huyo.
Mkewe alikuwa akilia, hakuamini kama mumewe alimsahau kwani kila alipomwangalia, hakuonekana kumkumbuka hata kidogo na kila wakati alikuwa akimuuliza kwamba alikuwa nani na kwa nini alikuwa mahali hapo.
“Mama! Nataka kuondoka! Nataka niende nikamwambie Melania kwamba anisamehe, labda ndiye mwanamke wangu sahihi, mama naomba nikaonane na Melania,” alisema William huku akiinuka kitandani pale.
Kila kitu alichokiona kilikuwa kipya, hakujua sababu iliyomfanya kuwa mahali hapo, na hata alipoambiwa kwamba alikuwa nchini Marekani, alishangaa, alifikaje na wakati alikuwa nchini Tanzania?
“Marekani? Nimefikaje?” aliuliza William.
“Ulikuja!”
“Hapana! Sikuwahi kuja Marekani! Mama! Hivi tuna hela kiasi gani za kuja nchini Marekani? Nilikuwa na mpango wa kuhack barua pepe ya Chuo Cha Harvard lakini sikuwahi kufika! Sasa nimefikaje? Mama! Nataka nikachukue hela, jana nimewachezea mchezo mchafu sana wale watu wa benki, ngoja nikaangalie kama hela imeingia,” alisema William.
Maneno yote hayo alikuwa akiyazungumza harakaharaka. Hakutaka kubaki humo ndani, akatoka. Hakuijua sehemu yoyote ile, alikuwa akishangaa, nje, akakutana na waandishi wa habari na kuanza kumpiga picha.
Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alishangaa, wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiota kwani hakuwahi kufikiria kama angefika nchini Marekani, na kitu kilichomshangaza zaidi ni jinsi alivyokuwa akipigwa picha.
“Who are you?” (nyie ni wakina nani?) aliuliza William huku akishangaa.
Alichokifanya daktari ni kuwatuma watu wamchukue William na kisha kumpeleka ndani. Hilo likafanyika, baada ya kupelekwa ndani na kuambiwa atulie, Dk. Pham akawaita wazazi na Linda kwa ajili ya kuzungumza nao.
Akawaambia kwamba hawakutakiwa kushangaa kile kilichokuwa kikiendelea kwani ndiyo hali iliyomkuta William hivyo walitakiwa kukubaliana naye na baada ya miezi michache hali yake ingerudi kama kawaida kama alivyokuwa na angekumbuka kila kitu.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Nendeni naye Tanzania! Naamini akifika huko, mazingira atakayokutana nayo yanaweza kumsaidia kukumbuka, kwa hapa Marekani, ni vigumu sana kutokea,” alisema Dk. Pham huku akiwaangalia.
Hicho ndicho walichokifanya, baada ya siku mbili wakaondoka na kurudi nchini Tanzania. Marekani, kila mmoja alishangaa, hawakuamini kama ajali ile aliyoipata William ingemfanya kuwa kwenye hali ile ya kupoteza kumbukumbu zake.
Ndani ya ndege alikaa na mkewe, Linda, alikuwa akimuongelesha lakini William hakusema kitu chochote kile, hakumfahamu, ndiyo kwanza alikuwa amemuona na kila alipotaka kumkumbusha, alimnyamazisha kwa kumwambia anyamaze kwani hawakuwa marafiki.
“Lakini nata...”
“Wewe mwanamke nimesema nyamaza. Tangu hospitalini unanifuatilia tu, nimesema nyamaza na sitaki uniongeleshe kitu chochote kile,” alisema William huku akimwangalia Linda.
Linda aliumia lakini hakuwa na jinsi. Safari iliendelea na baada ya saa ishirini na mbili, ikatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo wakateremka na kuchukua teksi ambayo iliwapeleka mpaka nyumbani kwao.
Walipofika William alionekana kukasirika kwani kila walipokwenda, Linda alikuwa pamoja nao. Alimchukia, kila alipomwangalia na mtoto yule aliyekuwa amemshika ambaye alionekana kuwa mdogo wa miezi miwili, moyo wake ulimkasirisha mno na wakati mwingine alitamani hata kumfukuza.
Linda hakutaka kumuacha William, aliamini kwamba kuna siku kumbukumbu zake zingerudi na kuanza kukumbuka kila kitu kilichotokea. Nchini Tanzania, kila mtu alimshangaa, alikuwa kijana mdogo mwenye sura mbaya lakini kila mmoja alikuwa akimfahamu.
Watu hawakukauka nyumbani kwake, walifika hapo na kuanza kumpiga picha kitu kilichomshangaza, kwa nini apigwe picha na wakati hakuwa mtu maarufu au kiongozi wa nchi?
“Mama! Nini kinaendelea? Mbona sielewi kitu chochote kile? Yaani nashangaa watu wanakuja na kunipiga picha kana kwamba mimi ni maarufum” aliuliza William huku akimwangalia mama yake.
“Mwanangu! Wewe ni maarufu sana!”
“Maarufu! Kivipi?” aliuliza William.
Kwa msaada wa maelezo, Linda akaanza kumwambia William kila kitu kilichokuwa kimetokea, siku ya kwanza alipofika Marekani mpaka alipopata ajali mbaya ya gari. Hakuamini, alibaki akimsikiliza Linda, hakumuelewa kabisa hasa pale alipomwambia kwamba alikuwa mpenzi wake.
Alimwangalia, hakumkumbuka hata kidogo, alishangaa kwani maishani mwake hakufikiria kuwa na msichana wa Kizungu. Hakukumbuka kitu chochote kile, hata alipomwangalia William Jr hakuwa akimfahamu kabisa, kwake alimuona kuwa mtoto wa kigeni na si wake.
“Na huyu ni mtoto wako,” alisema Linda huku akimwangalia William usoni, kama kulia, alilia sana lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika.
“Mtoto wangu?”
“Ndiyo!”
“Sijawahi kuwa na mtoto. Kwanza sijawahi kuwa na demu,” alisema William huku akimwangalia Linda.
Alimaanisha, alichokuwa akikisema kwake kilionekana kuwa sahihi kabisa. Hakukumbuka kama alikuwa na msichana, hakupendwa kwa kuwa alikuwa na sura mbaya, alimwangalia Linda, alipomwambia kwamba alizaa naye, alishangaa kwani hakuwahi kufikiria kupendwa na msichana mzuri kama alivyokuwa Linda.
Wakati hayo yakiendelea ndipo alipofungua televisheni na kuona habari ambayo ilimshtua sana, ilikuwa ni ya harusi ya mtoto wa bilionea, Melania na kijana aliyejulikana kwa jina la Godson.
Akashtuka, alichokikumbuka ni jana tu alitoka kuzungumza na msichana huyo kwenye mgahawa, iweje leo tangazo litokee na kuona kwamba msichana huyo alikuwa akitarajia kuolewa.
Alihuzunika moyoni mwake, alihisi kwamba Melania alimwambia kwamba alitaka kuwa naye kwa ajili ya kumuumiza tu na ndiyo maana kesho yake harusi yake ilikuwa ikitangazwa.
Hakutaka kubaki nyumbani, siku iliyofuata alikuwa kanisani. Humo, alikuwa gumzo, kila mtu alikuwa akimwangalia, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, watu walimshangaa na hawakujua sababu iliyomfanya kurudi nchini Tanzania ghafla namna hiyo na wakati alikuwa mtu maarufu sana.
Kanisani, watu hawakutulia, kila mtu alimsogelea, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwani alijiona kuwa mtu wa kawaida, hakuwa maarufu, sasa ilikuwaje watu waendelee kukusanyika mbele yake kiasi kile?
“William! Pole sana kaka! Nimesikia majanga uliyopata miezi miwili iliyopita,” alisema mwanaume mmoja aliyekaa karibu naye, William akashangaa kwani aliamini kwamba hakukuwa na mtu aliyekuwa akimfahamu, huyo alimfahamu vipi?
“Unanifahamu?” aliuliza William huku akionekana kushangaa.
“Sasa nisikufahamu wewe kaka? Kila mtu anakufahamu! Mpaka rais,” alisema kijana huyo.
“Hapana! Hakuna mtu anayenifahamu!”
“Wewe huoni jinsi watu wanavyokushangaa?”
“Kwa nini wananishangaa? Au kwa sababu mimi mbaya?”
“Hapana! Ni kwa sababu wewe ni maarufu,” alijibu kijana huyo.
Haikuwa mara ya kwanza kuambiwa hivyo, aliambiwa mara kadhaa kwamba yeye alikuwa maarufu na hakujua umaarufu wake ulitokana na nini. Aliendelea kukaa kwenye kanisa lile mpaka maharusi walipoanza kuingia. William akasimama, akaanza kumwangalia Melania, uso wake ulikuwa kwenye furaha kubwa, siku hiyo msichana huyo alionekana kuwa mrembo sana.
Melania alipokutanisha macho yake na William, alishangaa, ilikuwaje mwanaume huyo kuwa kanisani kipindi hicho na wakati alikuwa nchini Marekani akiendelea na maisha yake?
Hakuzungumza kitu zaidi ya kumuonyeshea tabasamu na kisha kuelekea mpaka mbele ya kanisa lile ambapo huko, harusi ikafungwa na kuwa mke wa Godson.
“Melania....Melania...” aliita Godson huku akimfuata msichana huyo aliyekuwa akijiandaa kuingia ndani ya gari la maharusi.
“William! Mbona upo hapa?” aliuliza Melania.
“Nimekuja kwenye harusi yako. Jana tulipoagana, nikajikuta nikiwa Marekani,” alisema William.
“William! Upo sawa?”
“Ndiyo! Hivi kwanza niambie kuhusu yule jamaa!”
“Jamaa gani?”
“Niliyemfutia picha zako!”
“Ni stori ndefu, ila kwa kifupi ni kwamba amekamatwa na polisi. Amefikishwa mahakamani na kufungwa miaka mitano kwa sababu alitaka kumuua mume wangu,” alisema Melania.
“Mume wako?”
“Ndiyo! Huyu hapa!”
“Alitaka kumuua kivipi? Mbona unanichanganya! Si alikuwa nchini Australia! Au walikutana huko?” aliuliza William huku akimwangalia Melania aliyebaki akiwa na mshangao.
Wakati wakizungumza hayo, waandishi wa habari walikuwa wakiwapiga picha tu. Wengi walishangaa kitendo cha William kuwa nchini Tanzania na wakati alikuwa nchini Marekani.
Harusi ikafungwa, alifurahi kwa sababu alipomkataa Melania alimwambia kwamba kuna siku angepata mwanaume sahihi na si yeye. Akaondoka kanisa, akasimama kituoni na kupanda daladala.
Alishangaa, watu waliendelea kumwangalia, waliopata taarifa za kupoteza kumbukumbu zake walimuonea huruma kwani alipokuwa akijiangalia, alijiona kuwa mtu wa kawaida sana ambaye hakuwa na umaarufu wowote ule.
Ndani ya daladala kila mtu alitaka kupiga naye picha. Kuonana na William halikuwa jambo jepesi hata mara moja, alikuwa mtu wa kuishi Marekani, bilionea mwenye pesa ndefu ambaye alitakiwa kufanya kila kitu alichotaka kukifanya.
Alipofika nyumbani, alishangaa kumkuta Linda akilia, hakujua ni kitu gani kilimliza, alimsogelea na kuanza kumbeleza huku akimlaumu Mungu kwa sababu gani alikuwa akipitia maisha hayo.
“Pole sana,” alisema William.
“Nashukuru!”
“Hivi unarudi lini kwenu?” aliuliza William.
“Unasemaje?”
“Unarudi lini kwenu? Nashangaa umekuja na kukaa hapa, hakuna mtu anayekufahamu, upoupo tu, hivi unaishi wapi? Naona tumekuja wote lakini sikujui! Huwezi kuondoka hata kwenda kuishi hotelini dada yangu?” aliuliza William maswali yaliyomfanya Linda kulia sana.
“Unataka niondoke?”
“Ndiyo! Ikiwezekana hata sasa hivi! Wewe nenda tu kwani hapa hakuna mtu anayekujua,” alisema William na kuelekea chumbani kwake, akaingia humo na kutulia kitandani. Sauti pekee aliyokuwa akiisikia kutoka sebuleni ni ya Linda tu aliyekuwa akilia kama mtoto, japokuwa mama yake alijaribu kumbembeleza lakini mwanamke huyo hakunyamaza.
“Mama muache asepe! Unamng’ang’ania unamjua? Kung’ang’ania watu utakuja kung’ang’ania majini,” alisema William kwa sauti, akajifunika shuka na kuziba masikio yake kwani hakutaka kabisa kuisikia sauti ya Linda wala mtoto wake, William Jr ambaye alikuwa akilia tu kana kwamba alikuwa akifahamu kilichokuwa kikiendelea.
Je, nini kitaendelea?
Je, William ataweza kurudiwa na kumbukumbu zake?
Tukutena Alhamisi hapahapa.
Post a Comment